Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
SHIRIKISHO la soka Tanzania limeshauriwa kutokata
tamaa na mpango wake wa maboresho ya Taifa Stars kupitia mkakati wake wa kusaka
vipaji mikoani ulioanzishwa hivi karibuni.
Taifa stars ya maboresho iliweka kambi mjini
Tukuyu mkoani Mbeya na kwa mara ya kwanza ilionekana aprili 26 mwaka huu uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi
kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mechi hii iliyowavutia wadau wengi wa soka kwa
lengo la kuona vipaji vipya kutoka mikoani, Stars ilipigwa vidude vitatu kwa
bila, (3-0).
Taifa Stars ilikuwa imesheheni vipaji vipya
vilivyopatikana katika mkakati wa maboresho ya Taifa stars ambapo jopo la
makocha waliteuliwa na TFF na kuzunguka nchi nzima kusaka vijana wa kuingizwa katika
timu.
Wakati mkakati huu ukitangazwa, wadau
waliuchukuliwa kwa mitazamo miwili tofauti ambapo na kundi moja liliunga mkono
na lingine likapinga kwa madai kuwa hautakuwa na tija kwa wakati huu ambao timu
inajiandaa kufuza AFCON mwakani nchini Morocco.
Rais wa TFF, Jamal
Malinzi alisema mkakati huu ni kuisaidia Stars ifuzu fainali za mataifa
ya Afrika mwakani, na wachezaji watakaopatikana katika maboresho haya wataweka
kambi Tukuyu jijini Mbeya na baadaye nchini Uholanzi.
Baada ya Taifa stars ya maboresho kuchapwa na
Burundi katika mechi ya kirafiki, maoni mengi yametolewa na wengi wanaponda
mfumo huu kuwa hauna msaada kwa sasa.
Wengi wanaeleza kuwa kumchukua mchezaji ambaye hachezi
ligi yoyote ile halafu unamleta Taifa stars , hawezi kukupatia matunda
unayotarajia.
Mtandao huu umehojiana na Mbwana Makata, Stephano
Mwasyika na David Bugoya kwa nyakati tafouti.
Makata ambaye alikuwa kocha wa JKT Oljoro na JKT
Ruvu kabla ya kuziacha timu hizo kwa nyakati tofauti miaka ya karibuni, amesema
mkakati huu ni mzuri, lakini lazima mipango iwe imara.
Makata amefafanua kuwa kama TFF wanataka kufanikiwa katika
mkakati huu, basi wahakikishe unakuwa
endelevu na wajenga mazingira mazuri kwa wachezaji wanaopatikana.
“Kwa upande wangu naona si vibaya japokuwa una
changamoto kubwa mno”.
“Naona itakuwa vizuri kama TFF wataharakisha
ujenzi wa vituo vya soka angalau mikoa mitano nchini ili kuwalea vijana hawa
katika akademi hizo”.
“Lakini kwa mazingira ya sasa, sina imani kama
mfumo huu utasaidia sana”. Alisema Makata.
Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la
Tanzania aliongeza kuwa ili kufanikiwa mpango huu kuna mambo yanatakiwa
kuzingatiwa;
Mosi; lazima watanzania wawe na subira kwasababu
si rahisi kufanikiwa kwa njia hii.
Makata alisema vitu kama hivi vinahitaji muda
kwasababu hata mataifa yalitumia mfumo huu yalitumia miaka kadhaa kufikia
malengo.
Pili; TFF na mashabiki wa soka wasiwe na matarajio
ya kikosi hiki cha maboresho kuipeleka nchi katika fainali za AFCON mwakani
kwasababu aina ya wachezaji waliopatikana hawana uzoefu wa kutosha na
wanahitaji miaka zaidi ya mitatu ili kuwa sawa.
Tatu; Makata alisema watanzania wasiwakatishe
tamaa vijana kwa kuandika na kuongea vibaya kwasababu watashindwa kujiamini na
kila wanapocheza watakuwa katika hali ya kukosa utulivu.
Makata alisisitiza kuwa uvumilivu ni muhimu kwa
hili, na lazima TFF wasije na nguvu ya soda.
“Tatizo letu watanzania ni wepesi wa kupanga,
lakini inapofikia utekelezaji inakuwa tofauti”.
“Zoezi liwe endelevu na inapobidi kwa pamoja
tushauriane njia sahihi ya kwenda na sio kukosoa kila kitu”. Aliongeza Makata.
Naye meneja wa Mtibwa Sugar, David Bugoya
alionesha wasiwasi wake juu ya mfumo huu kama kweli utafanikiwa mapema.
Bugoya alisema ni jambo zuri kutambua vipaji vya
mkoani, lakini ni ngumu sana kufikia malengo kwa haraka.
“Mini nadhani TFF wangetumia mashindano mengi ya
vijana yanayoendelea kusaka vipaji”.
“Sisemi mfumo ni mbaya, lakini nadhani unahitaji
muda wa kutosha kufikia malengo”.
“Kwa jinsi ninavyoona mimi, labda kwa kuwa ni
mapema. Nadhani kuna haja ya kuuangalia upya mfumo huu”.
“Kwenda AFCON kwa mfumo huu sina imani sana
kwasababu mpira unahitaji muda na mipango” Alisema Bugoya.
Naye beki wa zamani wa Yanga, Moro United, Prisons
na sasa Ruvu Shooting, Stephano Mwasyika amewashauri watanzania kutokuwa na
malengo ya kufanikiwa kwa mwaka mmoja baadaye.
“Vijana hawa ni wazuri. Taifa stars labda itakuwa
sawa miaka ya 2018/19 , kwasasa sidhani kama kweli mafanikio ya haraka
yatapatikana”
“Tusiwakatishe tamaa vijana wetu, tuwape muda wa
kujirekebisha na kujiimarisha zaidi. Uvumilivu uwepo na waaminiwe kwa asilimia
kubwa”. Alisema Mwasyika.
0 comments:
Post a Comment