Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
MOJA ya kilio kikubwa cha watanzania ni kutaka
kuona timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa
stars inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Tangu iliposhiriki kwa mara mwisho fainali za
kombe la mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria, Taifa Stars haijafanikiwa
kupata nafasi kama hiyo.
Kuelekea fainali za mataifa ya Afrika, AFCON
zitakazofanyika mwakani 2015 nchini Morocco, uongozi wa shirikisho la soka
Tanzania TFF umeanza kampeni za kuisaidia Stars ifuzu kushiriki fainali hizo.
Kabla ya kuondoka kwake, kocha wa Taifa stars
aliyevunjiwa mkataba mwaka huu, Kim Poulsen aliweka mikakati ya kuivusha Taifa
stars kucheza fainali za AFCON mwakani.
Mara zote Kim alikuwa anasema ndoto zake zinaweza
kutimia kwa kutumia wachezaji waliopo sasa Taifa stars na kutafuta wengine
wapya wanaoshiriki michuano ya ligi kuu.
Moja ya mkakati wa Kim ilikuwa ni kutafuta
wachezaji wengi zaidi na akalazimika kuwa na timu mbili za Taifa.
Moja ilibaki kuwa Taifa Stars iliyozoeleka, lakini
akaongeza nyingine ya `Young Future Taifa
Stars`.
Timu hii ya `Young Future Taifa stars` ilijumuisha wachezaji wanaotoka klabu za ligi
kuu, lakini hawakuwa na nafasi timu ya Taifa.
Lengo la Kim lilikuwa ni kupata uwanja mpana wa
kutafuta wachezaji wa kumsaidia kufuzu AFCON mwakani.
Hakika mpango huu uliungwa mkono na wadau wa soka
na wengi wao walijenga hoja yao kuwa ungewashitua wachezaji waliopo Stars kuwa
kuna wenzetu wapo nyuma yetu kama watazembea.
Chini ya Kim, Taifa stars ilibadilika kiuchezaji,
japokuwa haikufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano makubwa.
Lakini iliweza kuzifunga timu kama Morocco, Zambia,
Gambia, Cameroon na kuonesha kiwango kizuri.
Baada ya mabadiliko ya uongozi ndani ya TFF, Rais
mpya wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi alikuja na mipango yake.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi |
Moja ya vitu alivyofanya siku za kwanza ni
kubadili watu katika maeneo mengi ya uongozi wake.
Malinzi aliwaondoa watendaji wengi waliokuwa chini
ya Rais aliyemaliza muda wake, Leodger Chila Tenga.
Rungu hili la mabadiliko lilimwangua kocha wa Taifa stars, Kim Poulsen ambaye
alivunjiwa mkataba kwa madai ya kushindwa kuifanikisha Taifa stars na amelewa
Mholanzi, Mart Nooij.
Kilio kikubwa cha makocha wengi na wapenda soka nchini
Tanzania ni kukosa mfumo mzuri wa soka la vijana.
Makocha wengi wanadai wachezaji wengi wa
kitanzania wamekosa mambo ya msingi katika mpira kwasababu wengi wao wameanza
kujifunza mpira ukubwani.
Kwa misingi hiyo, makocha wengi wanapendekeza
nguvu kubwa kuwekezwa katika maendeleo ya soka la vijana.
Malinzi alikuja na mpango mzuri wa soka la
Tanzania, na moja ya vitu vikubwa alivyoahidi kuwekea mkazo ni kuifanikisha
Taifa stars kufuzu AFCON mwakani nchini Morocco.
Pia alisema anataka kujenga vituo kadhaa vya
kukuza viapji vya vijana yaani akademi.
Lengo si kuandika ahadi zake, lakini makala hii
inajaribu kuona mpango wa Malinzi na Taifa stars.
Rais huyo aliwashitua wengi baada ya kuja na
mpango mpya wa maboresho ya Taifa stars.
Alitumia makocha wengi wa soka waliocheza soka
zamani kujadili namna ya kuboresha Taifa stars.
Kwa pamoja, makocha hawa walikubaliana kuwa Tanzania
kuna vipaji vingi vilivyofichika, hivyo
liundwe jopo la kuzunguka mikoani kutafuta vijana wa kuwaingiza Taifa stars.
Toka mwanzo, makocha wengi wa kisasa walikuwa na
mashaka na mfumo huu, lakini TFF wakasisitiza utasaidia sana kuipeleka Stars
AFCON.
Malinzi alisema watatafutwa vijana wengi na
kuchujwa ili kupata wachache watakaojiunga na Stars. Na kweli zoezi likaanza na
kupatikana vijana hao.
Wachezaji hawa wa maboresho ya Taifa stars
waliwekwa kambini mjini Tukuyu na kwa mara ya kwanza waliletwa jijini Dar es
salaam kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya
Burundi.
Taifa Stars ya maboresho iliyochapwa mabao 3-0 na Burundi aprili 26 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam |
Mechi hii ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 50
ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar aprili 26 mwaka huu, na hamu ya wapenzi
wengi wa soka ilikuwa kuiona Stars ya maboresho iliyosifiwa na baadhi ya wadau
walioshauriana na Malinzi.
Kama kawaida, vijana hawa walitandikwa mabao 3-0,
na si kufungwa tu, hata mpira walichezewa.
Katika mechi hiyo walioonekana kucheza ni wale
wanaocheza ligi kuu kama akina Saimon Msuva, Frank Domayo na wengine wachache,
lakini vijana wa maboresho kila mtu aliona walichofanya.
Baada ya mechi hiyo, jambo jipya likalipuka ambapo
TFF walikosolewa kwa mpango huu na nadhani wao pia waliona hakuna walichofanya.
Mechi dhidi ya Malawi kule Mbeya, Kocha mkuu, Mart
Nooij aliwabwaga wachezaji wote wa maboresho ya Taifa stars na kuwadhihirishia
TFF na makocha waliopanga mfumo huu na watanzania wote kuwa tumepoteza pesa
bure.
Wadau wengi wamekuwa wakikosoa mfumo huu wa
Malinzi na kupendekeza wakae tena na makocha wao kubuni njia mbadala ya
kuisaidia Taifa stars.
Kila binadamu ana udhaifu wake, na kwa bahati
mbaya Watanzania wengi huwa hatukubali kirahisi kukosolewa.
Mnapokaa makocha 40 kujadili namna ya kuendeleza
soka la nchi ndani ya chumba, mnaweza kukubaliana mfumo fulani utumike kama huu
wa mabaoresho kwasababu tu mnafafana mawazo.
Lakini kuna jambo moja la msingi sana hapa, sidhani kama makocha wote kwa moyo
mmoja waliunga mkono mfumo huu. Naamini wapo walioona kabisa ni kupoteza muda,
lakini walishindwa kushauri kwasababu zao .
Inawezekana walikuwa waoga kwasababu walikuwa
nyuma ya mwamvuli wa watu fulani. Labda kuna watu yatari waliingia na majibu
yao kwa maana ya mpango kupangwa na makocha kuitwa ili waubarik na kuanza
kusaidia kuzunguka kuzunguka mikoani.
Lakini kama kweli walikuwa na nia ya dhati ya
kuisaidia Stars ifuzu AFCON, hatudhani kama wangekuja na mpango huu wa
maboresho.
Haya sasa, ukweli umeonekana, cha msingi ni TFF
kukubali kukosea na kujipanga upya.
Kukosea jambo la kawaida, lakini kukabiliana na
kosa ni jambo jema zaidi.
Nadhani TFF ni wasikivu na wanasikia kilio cha
watanzania kuwa mfumo wa huu wa maboresho ya Taifa stars ni mzuri, lakini
unahitaji muda na si mpango wa haraka.
Huwezi kutafuta wachezaji wa timu ya taifa mikoani
zaidi ya timu hizi za ligi kuu.
Wachezaji ni hawa hawa akina Ngassa, Domayo,
Bocco, Canavaro, Yondan, Nyoni, Singano, Msuva, Kiemba, Samatta, Ulimwengu na
wengineo. Hawa wa maboresho si wakutupeleka AFCON mwakani.
Waongezwe wengine kutoka timu za ligi kuu au
waliopo waandaliwe vizuri.
TFF mkipata nafasi ya kujadili tena na kutathimini
mavuno ya mpango wa maboresha ya Taifa stars, fikirieni upya juu la wazo lenu
ili mje na njia sahihi.
Ongezeni makocha wa kisasa waje na mipango mipya
na msitumie historia kuwa fulani alitolewa mkoani akaja kuisaidia Taifa stars.
Maisha yamebadilika na soka la kisasa linahitaji
utaalamu, lakini kwa haraka haraka kazaneni na mpango wa akademi, hapo nadhani
kutakuwa na jambo zuri la kuzungumza.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager ikiwa chini ya Kocha mpya, Mart Nooij tayari ipo jijini Mbeya kujiwinda
kwa mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya
Zimbabwe itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.
Kukubali kosa si dhambi hata kidogo. Asubuhi njema
kwako msomaji wetu.
0 comments:
Post a Comment