Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel:
0712461976
UWANJA wa kumbukumbu ya Sokoine uliopo jijini
Mbeya ni moja ya viwanja vikongwe nchini Tanzania, lakini kwasasa umeanza
kurudi katika ubora wake kutokana na marekebisho makubwa yanayofanyika.
Meneja wa uwanja huo, Modestus Mbande Mwaluka siku
zote anasisitiza kuwa wamiliki wa uwanja huo, CCM kwa kushirikiana na wadau wa
soka wanahakikisha wanaukarabati mpaka kufikia hadhi ya kimataifa.
Lengo la watu wa Mbeya ni kuona uwanja huo
unatumika katika mashindano makubwa ya kimataifa, hasa kama Mbeya City fc au
Prisons watafuzu michuano ya Afrika mwakani.
Kwa miaka mingi viwanja vya Uhuru, Taifa na CCM
Kirumba vimekuwa vikitumika katika mechi za kimataifa kwa ngazi ya klabu na
timu ya Taifa.
Japokuwa uwanja wa Uhuru bado upo katika
matengenezo, lakini kabla ya kujengwa kwa uwanja wa kisasa wa Taifa, ulikuwa
unatumika zaidi kwa mechi za kimataifa.
Uwanja wa CCM Kirumba mara nyingi unatumika kama
mbadala wa viwanja vya Dar es salaam. Pia Shk. Amri Abeid ni uwanja ulikuwa
unatumika katika mechi za kimataifa miaka ya nyuma kabla ya kudoda.
Kwa maana hiyo, mpira wa Tanzania kwa ngazi ya
kimataifa ulikuwa anaonwa zaidi katika viwanja hivyo, lakini Dar es salaam ndio
kitovu cha soka la Tanzania.
Kwasasa kumekuwa na mabadiliko hasa baada ya
kuiona Taifa stars ikicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Malawi mei
4 mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Stars kuchezea uwanja wa sokoine Mbeya, hivyo
ilikuwa fursa muhimu kwa wakazi wa jiji
hilo.
Mwenyekiti wa chama cha soka mkoani Mbeya, MREFA, Elias Mwanjala alikaririwa na mtandao
huu akisema kuwa fursa waliyoipata ni muhimu sana, na watahakikisha wanaboresha
zaidi ili kuwavutia TFF.
Mwanjala alisisitiza kuwa hawatawavutia TFF kwa
maneno bali ni kwa vitendo zaidi ambapo wataendeleza nguvu yao ya kuuboresha
uwanja huo wenye historia ndefu.
Watu tuliofika katika uwanja wa Sokoine, hakika
ilikuwa rahisi kugundua kuwa hawa jamaa wamejipanga vizuri. Uwanja upo katika
hali nzuri na unavutiwa kwa wachezaji na watazamaji.
Ubora wa uwanja unaangaliwa katika vitu vingi,
lakini sehemu ya kati `pitch` ni muhimu zaidi. Macho ya wengi yalilenga
kutazama sehemu ya kati iliyovutia kwa nyasi za asili.
Sokoine hakuna nyasi za bandi kama ilivyo kwa viwanja
vingine kama Karume jijini Dar es salaam, lakini `pitch` yake ipo katika hali
nzuri.
Baada ya msimu wa 2012/2013 kumalizika, uwanja huu
ulikuwa miongoni mwa viwanja vilivyofungiwa na TFF na kuwataka wamiliki kufanya
marekebisho.
Tanzania Prisons ndio walikuwa wenyeji wa uwanja
huo katika michuano ya ligi kuu, wakati
Mbeya City walikuwa wanautumia kwa mechi zao za ligi daraja la kwanza.
Kwa wakati ule uwanja wa Sokoine ulikuwa katika
hali mbaya kuanzia sehemu ya kati, majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo na
vyoo.
Wengi waliulaumu sana uwanja huu, na kama una
kumbukumbu nzuri, kocha wa zamani wa Yanga, Mbelgiji, Tom Saintfiet aliuponda
sana uwanja wa sokoine wakati walipocheza na Tanzania Prisons na kulazimisha
suluhu ya bila kufungana.
Kulikuwa na ukweli kwasababu uwanja ulikuwa mbovu
hasusani sehemu ya kati `Pitch`.
Baada ya msimu huo kumalizika, TFF waliufungia
uwanja huo na kuwataka wamiliki kufanya marekebisho. Hapo ndipo mambo yalianzia.
Meneja wa uwanja aliwahi kukaririwa akisema sasa wanajipanga kufanya mambo
makubwa.
Kizuri wamekuwa watendaji na wamekwepa siasa. Kwa
muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi kuufanya uwanja uwe bora.
Kwa mwenye kumbukumbu nzuri, Prisons waliathirika
mechi za kwanza za msimu wa 2013/2014 kwasababu uwanja wa Sokoine haukuwa
tayari baada ya kupandwa nyasi.
Hakika ilitakiwa subira, lakini baadaye kidogo
uwanja ukawa bora na kuendelea kutumika.
Baada ya hapo wakaanza kuhangaikia kuboresha
miundo mbinu ya uwanja kama vile majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo, vyoo
na maeneo mengine. Kwasasa wamefikia sehemu nzuri mpaka kufikia kukidhi mechi
ya Taifa stars.
Jana shirikisho la Tanzania TFF limetangaza
kusimamisha mechi za ligi ya mabingwa wa mikoa zilizotakiwa kupigwa uwanja huo kutokana
na marekebisho
yanayofanyika kwa ajili ya ukaguzi wa CAF.
Mechi za RCL za kituo cha Mbeya sasa zitachezwa
kwenye Uwanja wa CCM Vwawa uliopo Mbozi mkoani Mbeya.
Ukaguzi huu wa CAF ni mafanikio makubwa kwa watu
wa Mbeya kwasababu muda wowote uwanja huo unaweza kupewa hadhi ya kutumika
katika mechi za kimataifa.
Tayari kuna taarifa za chini kwa chini kuwa Taifa
stars inaweza kuchezea uwanja wa Sokoine dhidi ya Zimbabwe mei 18 mwaka huu katika
mechi yake ya awali kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini
Morocco.
Kama watapewa hadhi hiyo, basi yatakuwa mafanikio
makubwa kwa chama cha soka mkoani Mbeya na wamiliki wa uwanja huo,CCM.
Rais wa TFF Jamal Malinzi alifurahishwa sana na
wapenzi wa soka walivyojitokeza kuishangilia Taifa stars dhidi ya Malawi.
Zilikusanywa milioni 31 kutokana na kiingilia cha
shilingi 5,000/=. Haikuwa haba kutokana na mazingira ya Taifa stars.
Licha ya kufika uwanjani kushangilia, kulikuwa na
utofauti mkubwa sana wa ushangiliaji kwa watu wa Mbeya. Kwa muda mwingi walikuwa
wanaishangilia Taifa stars tofauti na ilivyozoelekea Dar es salaam ambapo
mashabiki wakati fulani wanaizomea timu.
Mashabiki walikuwa kivutio kikubwa, na wachezaji wa stars walijisikia vizuri na
kutamani kucheza mechi zao mikoani.
Kwa mafanikio haya ya Mbeya, ipo haja ya Rais
Malinzi kufanya jitihada za kuwasaidia Mbeya kupata nyasi za bandia ili uwanja
huo uwe bora zaidi na wa kisasa.
Tayari wataalamu wa nyasi za bandia kutoka FIFA
walishafika nchini na kwenda kukagua viwanja vya kanda ya ziwa.
Malinzi ajaribu kutoa kipau mbele kwa uwanja wa
sokoine kwasababu hata yeye alijifunza kitu kwenye mechi ya Stars. Alishituka
na kufurahia sapoti kubwa ya mashabiki na kuahidi kuwaombea fedha FIFA ili
uwanja huo upate nyasi za bandia.
Hilo ni suala zuri, lakini utekelezaji uwe wa
haraka ili kubadilisha mazingira kwa Taifa stars. Hii ni timu ya watanzania na
si timu ya Dar es salaam na Mwanza. Kuna haja ya kuwa na viwanja tofauti vyenye
ubora wa juu ili kufikia mafanikio ya watanzania wengi kuiona Stars katika
maeneo yao.
Mbeya mmestahili kupewa heshima hii kwasababu
mnapenda mpira na ushangiliaji wenu ni wa hadhi ya kimataifa.
Tumewaona mkiwa na Mbeya City fc, hakika ni
wazalendo wakubwa mno. Cha msingi endelezeni utamaduni wenu na itafika wakati
mtapata mechi nyingi za kimataifa.
Hapo mlipofika kutengeneza uwanja msiridhike,
endeleeni kuufanya bora zaidi.
Hongera meneja Mwaluka, hongereni uongozi wa
MREFA. Kazeni mfikie malengo yenu.
0 comments:
Post a Comment