Na Baraka Mbolembole
Nani atathubutu kumwita tena Robinho De Souza ni '
Pele Mpya'? Wakati, Pele ' mfalme wa kandanda duniani ' alianza kucheza katika ligi
kuu ya Brazil akiwa na miaka 16 katika klabu ya Santos, mechi yake ya kwanza tu
akafunga goli. Mwaka mmoja baadaye akiwa kinda wa miaka 17 akaitwa katika timu ya
Taifa ya Brazil, ' Selecao- Wateule' ambako alifanya ' maajabu' makubwa ambayo hayajafikiwa
na mchezaji yeyote Yule hadi sasa.
Licha ya kuwa na umri mdogo, na ikiwa mara yake ya
kwanza kucheza katika fainali za kombe la dunia, Pele aliisaidia, Brazil kutwaa
ubingwa huo katika fainali zilizofanyika nchini, Sweden, 1958, huku akiibuka mfungaji
bora wa pili akiwa amefunga magoli sita.
Alishinda mara tatu ubingwa wa dunia, na hadi anastaafu
soka akiwa na miaka 28, Pele alifanikiwa kufunga jumla ya magoli 1281 katika michezo
1363 za kimashindano akiwa na klabu ya Santos na timu ya Taifa.... Katika msimu
mmoja, Pele aliwahi kufunga magoli 127 , mwaka 1959 akiwa na Santos katika michuano
yote, alifunga magoli 110, mwaka 1961, na alifunga magoli 101, mwaka 1961.
Mfalme huyo wa kandanda duniani alifunga magoli matatu matatu katika mchezo mmoja
' hat-trick' mara 92, na aliifungia Brazil jumla ya magoli 97.
Moja kati ya matukio ya kukumbwa daima kwenye fainali
za kombe la dunia, 2002, ilikuwa ni kitendo cha winga, Denilson kukokota mpira mpaka
kwenye kona ya uwanja na kuzunguka nao akiwapiga chenga za maudhi mabeki, huku akikabwa
na nusu ya wachezaji wa timu ya Uturuki. Selecao, walikuwa mbele kwa goli 1-0
katika mechi ya nusu fainali huku zikiwa zimebaki dakika chache mpira umalize,
watangazaji wa mpira na mashabiki walipagawa kwa furaha, wakisifu kipaji cha
winga huyo wa zamani, Denilson kama kielelezo halisi cha soka la Brazil.
Katika hali ambayo ni vigumu kuamini, mwaka mmoja baadaye
aliibuka kijana mahiri mwenye kipaji kikubwa cha kupiga chenga za maudhi,
Robinho de Souza. Alikuwa kinda wa miaka 18 wakati alipoisaidia klabu ya Santos
kufika fainali ya klabu bingwa Amerika Kusini na kufungwa na Boca Junior.
Wakati, Pele alitumia muda wake mwingi kucheza soka katika klabu ya Santos,
Robinho alitangaza kipaji chake na haraka timu kubwa barani Ulaya zilianza kumfukuzia.
Alijunga na Real Madrid, mwaka 2005 akiwa ameifungia Santos magoli 73 katika kipindi
cha miaka mine.
TAMAA YA PESA AU AMEANGUSHWA NA KUKIMBIA
CHANGAMOTO?.
Akiwa na miaka tisa kwasasa barani Ulaya, Robinho ameshindwa
kufanana na Pele, kitabia, kiuwezo, na kimafanikio, alionekana kuwa mbioni kufikisha
walau michezo 100 ya kimataifa akiwa na Selecao, lakini ameishia kuiwakilisha nchi
yake mara 92 na kufunga magoli 27. Ni mafanikio makubwa kuiwakilisha nchi yenye
vipaji vingi vya uhakika kama Brazil. Lakini kama mchezaji ambaye alifananishwa
na Pele kiuchezaji ni aibu kutumia kipindi kirefu barani Ulaya na kushindwa kufika
walau katika orodha ya wachezaji watano bora katika tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Katika misimu yake miwili ya mwanzo, Madrid,
Robinho aliweza kuwa mchezaji tishio, alionekana kuwa na kipaji kikubwa ndani ya
uwanja. Akiwa amepewa jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na gwiji, Luis Figo,
nyota huyo wa Brazil alifanikiwa kufunga magoli 14 katika michezo 37, msimu
wake wapili alifanikiwa kuisadia Real kutwaa ubingwawa La liga huku akiibuka mfungaji
bora watatu nyuma ya Raul Gonzalez na aliyekuwa mfungaji bora, Ruud Van
Nistelrooy, huku pia akionesha kipaji kikubwa katika upigaji wa pasi za mwisho,
jambo ambalo lilimfanya kuwa nyuma ya kiungo Gutti katika vinara wa pasi za magoli
katika La Liga.
Baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika michuano
ya Copa Amerika, mwaka 2007, Robinho alionekana kama mchezaji bora duniani nyuma
ya Mbrazil mwenzake, Ricardo Kaka' lakini miaka miwili baadaye alipigana kulazimisha
uhamisho wa kuondoka, Madrid kwa madai ya kuchukizwa na kitendo cha rais wa klabu
hiyo kumfanya chambo ili amnase, Cristiano Ronaldo kutoka, Manchester United.
Robinho aliiwakilisha, Brazil kwa mara ya kwanza
mwaka 2003 akiwa na miaka 19 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya
Mexico, mara ya mwisho aliitwa na kocha wa sasa, Luiz Fillipe Scorali katika michezo
miwili ya kujipima nguvu dhidi ya Honduras na Chile. Scorali alimuita nyota huyo
kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011. Wapenzi wengi wa soka wanasema kuwa kitendo
cha nyota huyo kuhama, Madrid na kukataa ofa ya kwenda Manchester United,
Chelsea na kuichagua, Manchester City kilisukumwa na mambo ya kifedha zaidi ya kimpira.
United ilikuwa ikitamba barani Ulaya na kwa stahili
yake ya uchezaji, Robinho angeweza kutamba na kung'ara zaidi barani Ulaya, ila mshahara
wa pauni 300,000 kwa wiki ulihitimisha matarajio ya ' Pele Mpya'. Alitua, City
kwa ada ya rekodi, England, pauni milioni 32 na alifanikiwa kuonyesha makali yake
mwanzo mwa msimu wa 2008/09 lakini taratibu alianza kushuka kiwango chake cha
umakini, uchezaji na kujituma. Aliamua kurudi, Santos kwa mkopo ili kujiweka sawa
na fainali za kombe la dunia mwaka 2010. Baadaye alihamia, AC Milan na hadi sasa
bado yupo katika kikosi hicho ambacho alikisadia kushinda ubingwa wa Seria A,
msimu wa 2010/11.Amefungia Milan magoli 27 tu katika michezo 107 ndani ya misimu
minne.Aliifungia Real Madrid magoli 25 katika michezo 101
ndani ya misimu mitatu.
Baada ya kucheza michezo zaidi ya 360, kufunga magoli
199, kushinda mataji matatu makubwa barani Ulaya katika kipindi cha miaka tisa,
nani atathubutu tena kumuita Robinho De Souza ‘ Pele Mpya’? Kwasasa klabu ya Flamengo
inamuwinda nyota huyo ili kumrudisha nyumbani. Je, Robinho anaweza kuibuka tena?
Ameachwa na kocha Scorali katika kikosi cha Brazil ambacho kitashiriki katika kombe
la dunia mapema mwezi ujao katika ardhi ya nyumbani kwao. Ana miaka 3o kwasasa hivyo
kurejea ni jambo linalowezekana kwa kuwa yeye ni Mbrazil, na amekosa nafasi kutokana
na sababu hizo za yeye kuwa Mbrazil, nchi yenye vipaji kila kona.
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment