
Na Baraka Mpenja, Dar es saalaa
Tel:
0712461976
MWANASHERIA Damas Ndumbaro amepewa jukumu la kuongoza kamati ya
uchaguzi wa Simba sc kwa lengo la kupata warithi wa viongozi wasasa
wanaoongozwa na mwenyekiti, Ismail Aden Rage.
Kamati ya uchaguzi imeanza kazi hiyo baada ya
serikali kukabidhi katiba iliyofanyiwa marekebisho kwa uongozi wa Simba sc.
Uchaguzi wa Simba ulitakiwa kufanyika wiki
iliyopita, lakini mapungufu katika vipengele kadhaa katika katiba yao
yalikwamisha .
Lakini jana katibu mkuu wa Simba sc, Ezekiel
Kamwaga alitangaza kuwa tayari serikali imemaliza zoezi lake na kukabidhi
katiba.
Kwa misingi hiyo, Kamati ya uchaguzi haina cha
kupoteza zaidi ya kuanzisha rasmi mchakato mzima wa kupata viongozi wapya wa
klabu.
Tangu Rage aingie madarakani miaka miwili
iliyopita kumekuwepo na changamoto nyingi na mivutano isiyoisha.
Si rahisi kujua kama Rage alikuwa mbaya katika
uongozi wake kwasababu inasemekana kuna watu wachache walikuwa hawampendi ndani
ya uongozi na kupandikiza chuki kwa wanachama ili aonekane hafai.
Majaribio kadhaa ya kutaka kumpindua Rage
yameshuhudiwa bila mafanikio.
Katiba ya Simba imekuwa ikimlinda kwa wakati wote,
hivyo wale wanaojaribu kumpindua kugonga mwamba.
Unakumbuka sakata la aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa
Simba, Joseph Itang`are `Mzee Kinessi` na baadhi ya wajumbe wa kamati ya
utendaji.
Kinessi alitangaza kumsimamisha mwenyekiti Rage,
lakini mwanaume huyo aliyekuwepo nje ya nchi alirudi na kuita kikao chao kama kikao
cha harusi na yeye atabaki kuwa mwenyekiti.
Hata TFF walitangaza kumtambua na akaendelea na
majukumu yake klabuni.
Pia wanachama wa baadhi ya matawi walishakutana
mara kadhaa kutaka kumpindua Rage, lakini waliishia kuzodolewa na mkuu wao huyo.
Rage aliweza kuyafanya hayo kwa misingi ya katiba
ya Simba waliyoiandika wanachama wenyewe.
Wakati Rage anaingia madarakani, alikuja na
mipango mizuri ili kuiweka Simba klabu ya kisasa.
Aliahidi kujenga uwanja mzuri wa klabu, lakini
ndoto zake ziliyeyuka baada ya kutokea migogoro.
Inasemekana kuna watu walimsaliti Rage na kufanya
kazi ya kueneza sumu kwa wanachama. Ni ngumu kubaini hayo kwasababu mambo
mengine yapo chini ya kapeti.
Inawezekana Rage ana mapungufu yake kama ilivyo
kwa binadamu yeyote, lakini namna ya kujua mapungufu haya lazima uwe na hoja
iliyojengwa kwa umakini mkubwa.
Rage kaifanyia mengi klabu yake, lakini kwasababu
watu wengi wanaamini hafai, basi yanaokena mabaya zaidi kuliko mazuri.
Hakuna haja ya kuumiza kuzungumza juu ya Rage
ambaye tayari ameshatangaza kutogombea tena katika uchaguzi ujao.
Wanachama wa Simba umefika muda wa kumtoa
madarakani Rage ambaye wengi wenu mnaona hafai kwa mujibu wa katiba.
Klabu zinazoendeshwa na wanachama kama ilivyo kwa
Simba na Yanga, wa mwaka au mkutano mkuu wa uchaguzi ndio kila kitu.
Sasa Rage anaondoka, kazi kubwa ni kumpata mrithi
wake wa kuendeleza mazuri yake na kufuta mabaya yake.
Kama kwa muda mrefu mlikuwa mnataka mpiganaji Rage
aondoke Simba, umefika wakati wa yeye kukaa pembeni.
Kumbukeni soka limebadilika nchini Tanzania. Kwa
mipango mibovu, Simba imemaliza nafasi ya nne msimu uliopita.
Msimu wa mwaka juzi mlimaliza nafasi ya tatu. Kwa
misimu miwili mnakosa michuano ya kimataifa.
Najua mnaikumbuka Simba yenu ya 2003 na ile ya
akina Okwi misimu miwili iliyopita.
Simba ilikuwa hatari sana, lakini siku za karibuni
imekuwa na matokeo mabaya na sasa kuanza kuonekana timu ya kawaida.
Zamani timu kukutana na Simba ilikuwa shughuli
pevu, lakini msimu uliopita watu walikuwa wanajipigia kirahisi.
Ni kweli Simba mpo kwenye mpito kwasasa. Lakini wakati
wa mabadiliko umeshawadia.
Kwa muda mrefu wachezaji wa Simba wamekuwa
wakilalamika chini kwa chini kuwa uongozi wa Rage umeshindwa kuboresha
mishahara yao.
Pia ucheleweshaji wa mishahara na posho imekuwa
tatizo. Hata siku wakienda Zanzibar kujianda na mechi ya Yanga, wachezaji kwa
saa kadhaa waligoma kuingia kwene boti kwa kushinikiza kulipwa pesa zao.
Zacharia Hans Poppe aliokoa jahazi na tuliona
mpira wenu mkubwa uwanja wa Taifa na Yanga ambapo wanajangwani walihangaika
kuchomo o bao na kulazimisha sare ya 1-1.
Pia kumekuwepo na mabadiliko ya mfufulizo katika
benchi la ufundi, hivyo kuleta athari kubwa.
Simba imekuwa ikienda mbele na kocha huyu, lakini
ghafla analetwa mwingine na falsaya mpya na kuanza upya.
Bahati nzuri kocha wa sasa, Dvrako Logarusic
ameaminiwa na ataandeleza pale alipofikia mwaka huu na tayari ameshakabidhi
ripoti yake na mapendekezo ya usajili.
Tayari kamati ya usajili chini ya mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe ipo
kuijadili ripoti hiyo kuanzia jana jumatatu na itamaliza kesho jumatano.
Wakati kamati ya usajili ikiwa katika majadiliano,
nayo kamati ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wake Damas Ndumbaro inakutana leo
hii kupanga mchakato wa uchaguzi na tarehe ya kufanyika.
Hatua hizi mbili ni kubwa sana. Usajili na
uchaguzi.
Simba inategemewa kuleta sura mpya katika kikosi
na uongozi.
Watu wapya na mambo mapya. Kikubwa umakini uanzie
kwenye mambo haya mawili.
Watu wa usajili wafanye kazi nzuri na kutekeleza
mipango ya kocha wao ili kuimarisha kikosi chao.
Kama watasajili vizuri, Simba itarudi katika kasi
yake msimu ujao.
Pili, uchaguzi ni jambo lingine nyeti sana. Hapa
wanachama imebaki kwenu.
Kama kwa muda mrefu mnamlaumu Rage, sasa imefika
wakati wa kuchagua viongozi wapya.
Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya viongozi na timu
kufanya vizuri uwanjani.
Viongozi wakiwajibika vizuri kulinda maslahi ya
makocha na wachezaji, mpira lazima uonekane.
Kuweni makini na watu wenye nia ya kuomba uongozi.
Chunguzeni na pimeni sera zao.
Kuna watu wanaitwa wachumia matumbo. Hawa
wanaingia katika klabu kusaka tonge.
Kwa viongozi kama hawa, bado hamtafanikiwa malengo
yenu.
Chagueni watu wenye malengo na mapenzi makubwa na
klabu ili kuifanya Simba iwe mpya.
Mkifanya makosa, kumbukeni mtakuwa na safari
nyingine ya miaka miwili.
Yapo mengi yanatakiwa kufanyika katika klabu,
hivyo ni lazima kupata viongozi wenye mitazamo mizuri na uzalendo kwa timu.
Zipo changamoto za klabu, tafuteni watatuaji wa
matatizo yenu na si watu wa kuongeza matatizo.
Kila la heri Simba katika usajili na uchaguzi
wenu.
0 comments:
Post a Comment