
KOCHA wa Manchester City, Manuel Pellegrini
amewaonya wachezaji wake kuwa kitu kibaya watakachofanya ni kufikiria kuwa
tayari wameshatwaa ubingwa wa ligi kuu nchini England baada ya kuwafunga
Everton mabao 3-2.
Ushindi wa jana uliwafanya City wakalie usukani wa
ligi hiyo kwa wastani mzuri wa mabao dhidi ya Liverpool, huku wakisaliwa na
mechi mbili kumaliza msimu.
Man City wanaweza kutwaa ubingwa kama watashinda
mechi zote mbili za mwisho dhidi ya Aston Villa na West Ham, lakini Pellegrini
amesema mbio za ubingwa hazijakamilika bado.
“Nadhani kitu kibaya zaidi tutakachokifanya ni
kuanza kuwaza kuwa tumemaliza mbio za ubingwa sasa”. Pellegrini amewaambia waandishi
wa habari.
“Tutakutana na timu ambazo hazina presha, lakini
ni michezo muhimu sana. Kuanzia kesho (leo) tunaanza kuifikiria mechi ijayo
dhidi ya Aston Villa-kila mchezo tunauchukulia uzito wa hali ya juu”.
“Nadhani ni muhimu kuendelea kufanya vizuri kama
tufanyavyo sasa-mechi na Everton ilikuwa ya mwisho ugenini na tulianza msimu
huu kwa kuvuna pointi nne kwa mechi sita za kwanza ugenini, kwa mazingira haya
nadhani timu inafanya vizuri”.
Mabao mawili ya Edin Dzeko na moja la Sergio
Aguero liliwapa ushinda Man City dhidi ya Everton, lakini Pellegirini amekiri
kuwa ulikuwa mchezo mgumu kwa timu yake.
“Everton walicheza mpira mzuri toka mwanzo,
unaweza kuona kuwa walitaka kushinda tangu mwanzoni mwa mchezo, hakika ulikuwa mchezo mgumu sana
kwetu”.
0 comments:
Post a Comment