Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
RAIS wa shirikisho la soka nchini Tanzania, Jamal
Malinzi imepigana kiume kuwasiliana na mwenyekiti na mmiliki wa klabu ya TP
Mazembe, Moise Katumbi na taarifa njema
juu ya mawasiliano hayo ni kwamba washambuliaji wawili wa kimataifa wa
Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Ulimwengu watawasili jumamosi mchana
kwa ajili ya mchezo wa jumapili.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya TFF zinaeleza
kuwa Rais Malinzi amethibitisha ujio wa wanandinga hao tegemeo kwa Taifa stars
na kuibua matumaini ya Taifa stars kufanya vizuri kwasababu Samatta na
Ulimwengu ni wachezaji mahiri zaidi kwa sasa.
Nyota hao wawili watatumiwa kwa mara ya kwanza na
kocha wa Taifa stars, Mart Nooij katika mechi ya raundi ya awali kuwania kufuzu
fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco dhidi ya Zimbabwe kwenye
uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
TP Mazembe aliwazuia wachezaji hao kuja Tanzania kwasababu
wanawahitaji katika michezo ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Matajiri hao wa DRC walipo kundi A wanatarajia kucheza mechi ya
kwanza dhidi ya El Hilal Omduran siku ya
ijumaa mjini Khartoum nchini Sudan, hivyo baada ya mechi hiyo wachezaji hao wa
Tanzania watatua nchini jumamosi na kucheza mechi siku ya jumapili.
Hata hivyo baada ya mechi hiyo watakwea pipa kuelekea
Lubumbashi DRC tayari kwa maandalizi ya mechi ya pili dhidi ya mahasimu wao AS
Vita mei 25 mwaka huu.
Baada ya mechi hiyo na AS Vita ambapo wiki
iliyopita walikutana nao katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya DRC na
kushuhudia vurugu kubwa ziliosababisha watu zaidi ya 15 kupoteza maisha,
Samatta na Ulimwengu wataweza kupata nafasi ya kucheza mechi ya marudiano na
Zimbabwe mjini Harare.
0 comments:
Post a Comment