Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976
KWA mara ya kwanza tangu Frank Domayo na Didier
Kavumbagu waondoke kwenda Azam fc, mwenyekiti wa Young Africans, Yusuf Manji ameunguruma
makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya Twiga na Jangwani, Kariokoo jijini Dar
es salaam.
Manji katika mazungumzo yake na waandishi wa
habari jana alisema kuondoka kwa wachezaji wao wawili Kavumbagu na Domayo sio
mwisho wa timu ya Yanga, kwasababu uongozi wake unaendelea na mipango ya
kuhakikisha wanasajili wachezaji wengine wazuri kwa kufuata maelekezo ya Benchi
la Ufundi.
Mwenyekiti huyo alisema yameongelewa mengi sana
kwa kipindi cha mwezi mmoja ambao hakuwepo nchini kwa ajili ya kazi zake
binafsi, lakini sasa amerejea na maandalizi ya msimu ujao yameshaanza.
“Kuondoka kwa Kavumbagu ni kutokana na kuchelewa
kwa majibu ya TFF juu ya idadi ya wachezaji wa kigeni kwa msimu mpya, huku Domayo ambae tangu mwaka
jana aliombwa kuongeza mkataba alikua akisema anamsubiria mjomba wake ndipo
aweze kufanya hivyo”. Alikaririwa Manji.
Kwa jinsi Manji alivyozungumzia suala la Domayo
unagundua kabisa kwamba huyu jamaa ni mwepesi wa kukiri makosa. Ni jambo zuri
kukubali makosa unapokuwa kiongozi. Kuna watu huwa hawawezi kikiri udhaifu kwa
jambo lolote.
Hakuna mtanzania yeyote awe wanachama au si
mwanachama wa Yanga asiyejua umuhimu na ubora wa Frank Domayo katika timu. Ni
kijana mdogo mwenye kipaji cha hali ya juu na viongozi wa Yanga chini ya
mwenyekiti wao Manji wanatambua hilo.
Baada ya kuondoka kwa Domayo, walisikika viongozi,
wanachama na wapenzi wa Yanga wakisema Domayo si chochote. Lakini moyoni
walikuwa wanaumia kwasababu wanajua ni mchezaji bora.
Wengi wao walikuwa hawakubali kufanya makosa zaidi
ya kutamba kutafuta wachezaji wakali zaidi. Kwa bosi wao imekuwa tofauti
kabisa, kwani ameanza kwa kukiri uzembe kufanyika, hivyo kujipanga upya.
Manji anajua kuwa viongozi wamefanya makosa
kuondoka kwa Domayo, lakini haina jinsi kwasababu imeshatokea. Kwa maana
nyepesi anawaomba radhi wanachama wa Yanga walioumia na kuondoka kwa nyota
huyo. Njia ya kuwapooza ni kuwaletea wachezaji wengine watakaoziba nafasi ya
kiungo huyo.
Kwa suala la Kavumbagu, Manji amekuwa mkweli kuwa
TFF ndio wamewayeyusha kwa kuchelewa kujibu juu ya sheria ya wachezaji wa
kigeni. Hapa huwezi kuwalaamu sana, japokuwa kuna swali moja la kujiuliza, Azam
walipokuwa wanamsajili Kabumbagu walijua kuwa sheria itabakia kuwa wachezaji
watano?
Kama ndiyo, nani aliwaambia ? kwasababu
walifikisha wachezaji 6 wa kigeni baada ya kumsajili Kavumbagu, lakini
wakavunja mkataba na Ismail Kone na kubakia na watano.
Manji ameonesha ukomavu mkubwa wa uongozi, si
mwepesi wa kuja juu, anapokosea anakiri na kuahidi kufanya vizuri zaidi. Kwa
hili na ufafanuzi huu mzuri, Yufus Manji umepata kura yangu.
Pia Manji alisema pamoja na kuondoka kwa wachezaji
hao bado kwa kushirikiana na kocha Hans der Pluijm watahakikisha Yanga
inaendelea kutisha msimu ujao na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Pluijm wakati anaondoka wiki iliyopita aliahidi
kuleta wachezaji wazuri watakaoisaidia Yanga .
Ni utaratibu wa makocha dunia kote kuwasilisha
ripoti kila msimu unapomalizika.Yanga walishapokea ripoti ya Pluijm inayoeleza
kila kitu.
Kwa kuzingatia mapendekezo ya mwalimu wao, Manji
alisema wataleta `majembe` mapya ya kuisaidia Yanga katika mashindano ya msimu
ujao wa ligi kuu na kombe la shirikisho.
Hapa lazima Yanga wasajili kwa kuzingatia
mapendekez ya benchi la ufundi na si kusajili kwa sifa na kuwakomoa watu fulani.
Kombe la shirikisho ni mashindano makubwa, lazima
wasajili vizuri kwa kuangalia nafasi na si kulundika wachezaji wasiokuwa na
maana katika klabu kwa wakati huu.
Manji iambiea kamati yako ya usajili na uwasimamie kuleta
wachezaji hao unaoahidi kuwa watakuja kuziba nafasi za Domayo na Kavumbagu.
Suala la ujenzi wa Uwanja wa Kisasa eneo la
Jangwani , Manji alisema bado lipo pale pale, kikubwa kinachosubirwa ni majibu
ya serikali juu ya maombi ya eneo la ziada, kwani Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
alisema suala hilo lipo ukingoni na mda si mrefu.
Simba na Yanga zinatia aibu kwa hili la kukosa viwanja.
Kuna wakati timu hizi zinahangaika kutafuta wapi kwa kufanyia mazoezi.
Wakati fulani Mahafali ya kidado cha nne au saba
inavunja program ya mazoezi ya klabu hizi kwasaabu viwanja wanavyoomba hutumika
kwa sherehe. Aibu iliyoje hii.
Hii ni fedheha kubwa sana kwa timu hizi kongwe
katika soka la Tanzania.
Siku za karibuni, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa
Yanga miaka ya nyuma, Bilionea Davis Mosha alikaririwa akisema anashangaa kuona
Azam fc iliyokuja juzi juzi tu ikishindana na Yanga kupora wachezaji.
Mosha alijenga hoja yake kuwa Yanga ni klabu
kongwe ambayo inastahili kuchukua wachezaji Azam fc na si Azam kuchukua Yanga.
Suala la Domayo lilimuuma sana Mosha na kuamua kufichua ya moyoni.
Mosha aliwalaumu viongozi kwa kufanya uzembe wa
kuwaachia wachezaji hawa. Na jana Yusuf Manji alikiri kuzembea juu ya suala
hili.
Pia Mosha alisema klabu ya Azam fc iliyokuja juzi
inamiliki uwanja, TV na sasa wanajiandaa kuanzisha redio yao. Bilionea huyo
alisikitika sana.
Suala la uwanja si Mosha peke yake, wapenzi wengi
wa soka wanazishangaa Yanga na Simba kushindwa kujenga hata viwanja vya
mazoezi.
Tatizo kubwa ni siasa kutawala kwa viongozi wa
klabu hizi. Wamekuwa wakiahidi kujenga viwanja, lakini inapofika utekelezaji
wanakula kona.
Aden Rage wakati anaingia madarakani katika klabu
ya Simba miaka miwili iliyopita, aliahidi kupambana na kujenga uwanja wa
kisasa. Lakini baadaye alikuja kuruka kamba na kusema kama serikali ya CCM
imejenga uwanja wa Taifa kwa miaka 50, yeyee na kamati yake wanawezaje kujenga
uwanja kwa miaka miwili?
Swali, wakati anaingia madarakani hakujua kama
kujenga uwanja ni gharama kubwa?, na kwanini aliahidi wakati anajua hawezi. Hizi
ndio siasa za mpira wa Simba na Yanga.
Miaka miwili sasa imepita, Yusuf Manji aliahidi kujenga uwanja wa kisasa
katika klabu ya Yanga. Muda wake umeisha na hatagombea tena, huku dalili za
kujenga uwanja zikiwa hazionekani.
Viongozi wa Yanga mara zote wamekuwa wakishindwa
kunyosha maelezo juu ya ujenzi wa uwanja mpaka sasa wanaondoka madarakani.
Maneno ya Manji hapo jana kuwa ahadi ya uwanja ipo
palepale ni kutoka mdomoni tu, utekelezaji unasubiriwa kwa hamu. Si mara ya
kwanza kwake kutamka juu ya hili, na watu tunakumbuka alishawahi kusema.
Kwasasa hatuna haja ya kusikia akisisitiza ahadi
yake bali tunataka kuona vitendo. Kusema ahadi ipo palepale ni maneno ya siasa
tu, kisayansi hatujaona kitu chochote katika ahadi hiyo.
Kama kweli Bilionea huyo anataka kujenga uwanja ,
basi kuna haja ya kuungana na wenzake kuhakikisha wanatekeleza ahadi hii tamu
kwa wanayanga.
Yanga ina rasilimali nyingi na mtaji mkubwa wa wanachama
nchi nzima. Kuna kila uwezekano wa kufanikisha ujenzi wa uwanja, lakini tu kama
watapatikana viongozi wenye mtazamo wa maendeleo.
Kuelekea uchaguzi ujao, wanachama wa Yanga
chagueni watu watakaoshirikiana na mwenyekiti wenu atakayekuwa mstaafu kwa
wakati huo, Yusuf Manji ili mjenge uwanja wenu.
Igeni mfano wa Azam fc ambao hutumia zaidi vitendo
na si siasa za kupeana moyo kila wakati. Tutajenga uwanja tutajenga uwanja sasa
imekuwa kama wimbo wa taifa.
Kwa Manji kulifuta rasmi tawi la Tandale kutokana
na kuwa na chanzo cha vurugu na migogoro ndani ya klabu, pia amewafuta
uanachama wanachama sita ambao walikiuka katiba ya Yanga kwa kwenda kuongea na
waandishi na HABARI bila ya Idhini ya uongozi huku pia wakishindwa kulipia ada
zao za uanachama kwa zaidi ya miezi sita, sina tatizo nalo.
Kama waliunda wenyewe sheria hiyo na kuambizana,
basi watajijua wao wenyewe. Kuvunja sheria mliyojiwekea wenyewe kwa matakwa
yenu ni makosa na halina maswali.
Kuongea na vyombo vya habari sio kosa kwasababu ni
haki ya kikatiba, lakini kama kuna sheria ambayo Yanga wamejiwekea kwa
kukubalina, basi sisi tuliopo nje ya Yanga hatuna maswali. Waliofutwa uanachama
ni:
1. Ally Kamtande, 2. Isiaka Dude, 3. Hamisi
Matandula, 4.Waziri Jitu Ramadhani, 5.Mohamed Kigali Ndimba , 6. Selaman Hassan
Migali
Mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba utafanyika
terehe mosi Juni, 2014 katika Ukumbi wa Oysterbay Police Mess na wanachama wote
wanaombwa kulipia ada zao ili waweze kuhuhudhira mkutano huo wakiwa hai.
0 comments:
Post a Comment