Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABAO 2-0 waliyopata Nigeria dhidi ya timu ya
taifa ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 20,Ngorongoro Heroes jioni
hii uwanja wa taifa katika Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kwa vijana yamempa kazi ngumu kocha mkuu John Simkoko kusonga mbele.
Ngorongora walipata nafasi kadhaa za kufunga
kipindi cha kwanza, lakini bado ugonjwa wa kutotumia nafasi muhimu unazidi
kuitafuna timu hii.
Mshambuliaji Saady Kipanga alishindwa kuonesha
makeke yake baada ya kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika
milango ya timu zote ilikuwa migumu, huku kipa namba moja wa Heroes, Aishi Manula
akiumia.
Kipindi cha pili, Manula alishindwa kurejea uwanjani
na kumpisha kipa namba mbili, Peter Manyika.
Katika Kipindi hicho cha pili Ngorongoro waliingia
kizembe na kujikuta wakifungwa mabao mawili na kumaliza mechi kwa kipigo cha
nyumbani cha mabao mawili kwa sifuri.
Aishi Manula alicheza kwa dakika 45 tu na kumpisha Peter Manyika Peter |
Wakati Ngorongoro wakihaha kusawazisha bao hilo,
Nigeria walifanya shambulizi la kushitukiza na kufanikiwa kupata bao la pili
kupitia kwa Awoinyi Taiwo baada ya kutumia vizuri makosa ya beki Pato Ngonyani
aliyezembea kuondosha mpira kwenye eneo
la hatari.
Kilichoonekana kwa Ngorongoro Heroes ni kukosa
umakini na kushindwa kujiamini kila wanaposhika mpira.
Nigeria waliwazidi vijana wa Tanzania kwa vitu
vingi, lakini kikubwa zaidi ni kucheza kwa kujiamini na kumiliki mpira kwa
wakati wote.
Kwa dakika zote 90, Nigeria walikuwa wanajitahidi
kumiliki mpira na kuwahangaisha vijana wa Tanzania.
Walilindi vizuri lango lao, walikaa na mpira na
kupiga pasi nzuri, na kushambulia kwa kutumia akili nyingi, hivyo kuonekana
kama wapo nyumbani kwao Lagos.
Hawakuwa na papara wanapofika langoni kama
ilivyokuwa kwa vijana wa Heroes.
Nigeria hawakupata nafasi nyingi katika mchezo wa
leo, lakini kila walipokuwa wanafikia lango la Ngorongoro walikuwa hatari
zaidi.
Mabao ya Nigeria yamefungwa kutokana na mabeki wa
Ngorongoro kufanya uzembe wa kuziba njia za kupita wapinzania wao.
Kuna wakati mabeki wa Ngorongoro walikuwa
wanashindwa kufanya maamuzi ya kuondosha mpira ya hatari, hasa bao la pili
ambapo Ngonyani alishindwa kuondosha mpira
katika eneo la hatari.
Sehemu ya ushambuliaji ya Heroes imekuwa butu na
kuwanyima watanzania ushindi leo hii.
Katika michezo miwili dhidi ya Kenya, kocha mkuu
wa Heroes, John Simkoko alikiri kuwa safu ya ushambulaiji ilikuwa butu, hivyo
kuahidi kufanya marekebishao.
Lakini leo bado safu hiyo imeonekana kukosa
umakini na kushindwa kuandika mabao kwa nafasi muhimu walizopata.
Kelvin Friday alifanya kazi nzuri na kupiga mipira
mingi katika eneo la hatari la Nigeria, lakini washambulaiji wa kati Juma
Luizio na Saady Kipanga walishindwa kutumia vyema nafasi hizo.
Ngorongoro kwa muda mwingi walipooza na
hawakucheza kwa kasi, hivyo kuwapa nafasi wageni kutulia na kucheza watakavyo.
Nigeria wameonekana kuwa bora kwasababu waliwazidi
Heroes kwa kila kitu, japokuwa ukiangalia maumbo ya wachezaji yanafanana na vijana
wa Tanzania.
Kwa matokeo hayo, Simkoko anahitaji kufunga mabao
3-0 nchini Nigeria mei 23 mwaka huu katika mchezo wa marudiano au kushindwa 2-0 ili mshindi apatikane kwa mikwaju ya penati.
Simkoko ana kazi ngumu ya kufanya marekebisho ya
makosa ya kikosi chake kwasababu kiwango cha Nigeria cha leo kinadhihirisha
ugumu wa mechi ijayo.
Hata hivyo kitu kibaya zaidi leo hii ni wapenzi
wachache kujitokeza kuwashangilia Ngorongoro Heroes.
Vijana waliomba kupewa sapoti na mashabiki, lakini
watanzania wamewaangusha kwa kushindwa kufika kwa wingi.
Mechi yenyewe imepigwa siku ya wikiendi, lakini
watu wamesita kufika uwanjani. Uzalendo bado ni tatizo kwa soka la Tanzania
hasa timu za taifa.
0 comments:
Post a Comment