Na Baraka Mbolembole
Kuna watu wamezaliwa kuwa viongozi, kila wanachokuwa wanasimamia
huendavizuri. Jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa wanachama wa klabu
ya soka ya Simba kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi za urais,
makamu wa rais wa klabu na wajumbe wa kamati ya utendaji. Siku ya jana
niliandika makala kuhusu mtu anayepaswa kuwa rais wa klabu hiyo
anavyotakiwa kuwa. Leo, nitazungumzia kidogo kuhusu nafasi ya umakamu wa
rais ambayo wanachama watano wamechuku fomu za kugombea nafasi hiyo.
Wanachama wawili kati yao walikuwepo katika utawala unamaliza
muda wake, Geofrey Nyange Kaburu ambaye katika kipindi cha miaka ya
uongozi unamaliza muda wake alikuwa ni makamu mwenyewe, kabla ya
kujiuzulu mapema mwaka 2013, na Joseph Itangare ‘ Mzee Kinesi’ ambaye
alikaimu nafasi iliyokuwa imeachwa na Kaburu kwa muda wa mwaka mmoja na
nusu. Wamefuata nini tena? Wameongeza ujuzi gani katika fikra zao za
utawala? Wanarudi, Simba kufanya nini?
Jana nilimsikia aliyekuwa kocha
wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo akitoa yake ya moyoni ambayo yamemfanya
kuchukua fomu za kugombea nafasi ya umakamu wa rais. Unafikiri, Julio
alikuwa pale kuwachekesha watu na kutengeneza vichwa vya habari katika
media, hapana. Nafikiri ameguswa na orodha ya wagombea waliojitokeza
kuwania nafasi hiyo.
Kwa mtu anayeifahamu, Simba nje-ndani kama, Julio bila shaka
atakuwa tayari kutoka nje ya taaluma yake ya ukocha na kwenda kujaribu
kuokoa jahazi katika nafasi ya uongozi katika timu anayoipenda na
kuishabikia.
Kama atafanikiwa kushinda kama
alivyodai yeye mwenyewe, upande wangu nitakuwa na mashaka na wapiga
kura, ila sitashangaa endapo wanachama watampeleka madarakani. Kuna vitu
vinachosha, na kuna watu hawataki kukubali matokeo ya kushindwa wakati
ni changomoto tu katika harakati za maisha. Samahani, nauliza tu, hivi
watu kama Kaburu na Itang`are wanarudi Simba kufanya nini?. Kama
tunawahitaji kina, Issa Hayotou katika klabu zetu na tuwarudishe
madarakani sasa! Si, tunawapenda! Tunawaheshimu! Tunawanyenyekea! Hatuna
kitu bila wao!
Upande wangu napenda kuwafagilia na kuwaunga mkono viongozi
wenye sera na mitazamo ya kisasa yenye maendeleo hata kama watakuwa
wapenda madaraka kama, Sepp Blatter. Unaweza kuwa na tamaa ya kuongoza
jambo au taasisi Fulani lakini katika njia ya kufikia tamaa hiyo ukawa
unakutana na vikwazo vingi kitu ambacho kinakufanya ujifunze zaidi.
Kwa, mfano, mimi ningewaambia, Itangare na Kaburu wakajifunze
kwanza jinsi ya kuunganisha mahusiano ya kiutawala kati ya kiongozi wa
chini na Yule wa nafasi ya juu. Wote hawa walishindwa kwenda sambamba na
mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mh. Aden Rage. Nakumbuka kuna
wachezaji wengi waliwahi kuniambia kuhusu kutothaminiwa, kunyanyaswa
katika malipo, na kudharauliwa na makamu huyo mwenyekiti wa zamani
aliyejiuzulu katika utawala unaomaliza muda wake.
Upande wa Itangare, yeye ni mtu muhimu na ambaye ameisaidia sana
Simba, kifedha na ki-hali, ila ni mtu dhaifu katika mambo ya utawala.
Anayumba, kama vile bendera inayofuata upepo. Sijui sana kuhusu wao, ila
kiutawala ni watu ambao naweza kuwaongea na kuwashauri.Wangejifunza
kwanza ili kuwa viongozi makini, muda bado upo, Simba itaendelea
kuwepo.Simba inatakiwa kuwa na rais na makamu wake wenye mtazamo sawa.
Sifikirii kama safu ya Michael Wambura na Itangare, Swed Nkwabi au
Kaburu inaweza kutoa mafanikio mazuri. Watakuwa wakipishana tu, kama
ilivyokuwa kwa Aden Rage. Sijui kwanini ila nipo njiani kupata ukweli
wake.
Julio, amekumbusha hadi madeni yake ya wakati wa uongozi wa
Mzee, Hassan Dalali. Amesema viongozi wanaomaliza muda wao katika
utawala wa sasa hawapaswi kupewa nafasi safari hii. Akaongeza, yeye ni
kocha wa Simba hadi leo hii. Hahaha, Julio ukimuona anaongea kama
anaropoka jua kuna ukweli hapo. Ujumbe umefika, nafikiri huyo ni bora
zaidi katika nafasi ya umakamu wa rais katika klabu ya Simba, kama
watashindwa kuwatazama usoni. Katika kazi za kimagereza, mfungwa
unapatiwa kazi, ukiwa nyuma wewe ni mvivu, utapigwa kweli, ukiwahi
utaambiwa unataka kutoroka! Mfungwa anafanya kazi kwa saa, anakula kwa
wakati maalumu, kulala muda uliopangiwa na kuishi katika taratibu za
kimagereza. Nafasi ya makamu wa rais, Simba SC, haina watu sahihi?
Julio, ameshazungumza kuwa anaidai, Simba, sijui atajilipa
kwanza madeni yake akiingia madarakani? Huyu amechoshwa na mengi ndani
ya Simba, anataka viongozi makini, wasio wanyonyaji, wenye uchu na moyo
waki-Simba hasa. Yeye ndiye, kwa waliopo! Kutoka uchezaji, ufundishaji,
hadi umakamu wa rais, Simba SC, Julio ni mtu jasiri, nazisubiri, rufaa
zake! Nakumbusha tu, vita ya kwanza kubwa ya viongozi wajao ni kuvunja
utegemezi kutoka kundi la marafiki wa Simba. Nimewasilisha tu, kesho
tena, Inshallaha!
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment