
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
CHAMA cha soka mkoani Mbeya, MREFA kimewashukuru
mashabiki wa soka ndani na nje ya mkoa huo kwa kujitokeza kuishangilia timu ya
Taifa ya Tanzania, Taifa stars dhidi ya Malawi.
Mechi hiyo iliyomalizika kwa suluhu pacha ya bila
kufungana, Stars ikiingozwa kwa mara ya kwanza na kocha mpya, Mart Nooij
ilichezwa kwenye uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza na mtandao huu jioni hii, katibu mkuu
wa MREFA, Seleman Haroub amesema mechi ilimalizika salama na kwa asilimia kubwa
walipata mafanikio.
“Tunashukuru mechi imefanyika salama na kila kitu
kimekwenda sawa. Mashabiki walijitahidi kujitokeza na nadhani inatupa taswira
kuwa siku za usoni TFF watatufikiria zaidi”.
“TFF wameonesha kutujali sana na kutuletea mechi
ya timu ya taifa kwa mara ya kwanza, hakika tunayafanyia kazi mapungufu
yaliyopo katika uwanja wetu ili tupewe mechi nyingi zaidi”. Alisema Haroub.
Aidha, alisema ukarabati wa uwanja bado unaendelea
hasa kujenga vyoo vya kisasa kwa lengo la kuufanya uwe na hadhi kubwa ya kimataifa.

Katika mechi ya jana, Kocha Nooij aliamua
kuwatumia wachezaji wenye uzoefu na michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara
badala ya wale waliopatikana katika mpango wa maboresho ya timu hiyo.
Kitendo cha kocha Nooij kuwaacha wachezaji
waliochagulia kutoka katika mpango wa maboresho kimezua hisia tofauti kwa wadau
wa soka.
Wengi wamekuwa wakisikika kuwa wachezaji hao
hawana kiwango cha kuichezea Taifa stars na kuifikisha fainali ya kombe la
mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Lakini baadhi ya wadau wanasisitiza wachezaji hao
wapewe muda na kuaminiwa ili kuiletea mafanikio Taifa stars.
Mechi ya jana ilikuwa ya pili kwa Taifa stars ya
maboresho ambapo aprili 26 mwaka huu siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilicheza dhidi ya Burundi na kulala mabao
3-0.
Mechi dhidi ya Burundi, kaimu kocha kwa wakati
ule, Salum Madadi aliwatumia zaidi wachezaji wa kikosi cha maboresho, lakini
jana bosi wake, Nooij akawatoa kabisa katika mpango wake.
0 comments:
Post a Comment