Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MAKAMU mwenyekiti wa zamani wa Yanga sc, Bilionea,
Davis Mosha ameushutumu uongozi wa sasa wa klabu hiyo kushindwa kuwabakiza
wachezaji muhimu kikosini kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara na
michuano ya kimataifa.
Mosha ambaye ni mwanachama na shabiki mkubwa wa
Yanga, ameshangazwa na uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti Yusuf Manji kumwachia
kiungo wake mkabaji, Frank Domayo na mshambuliaji Didier Kavumbagu kwenda Azam fc.
“Tunajua Kavumbagu kaenda kule, labda ndiye
walikuwa wanamhitaji”.
“Haya, tumekuja kusikia Domayo naye kaenda Azam,
mara tunasikia fununu kuwa Mbuyu Twite naye anakwenda Azam”.
“Sasa ni nini kinaendelea hapa katikati, ni kwamba
viongozi wanataka kuondoka na kuacha timu haina wachezaji kwasababu wamesema
hawagombei tena au wanataka kuleta wachezaji wazuri zaidi kuliko hao”. Alisema
Mosha kwa masikitiko makubwa.
“Yanga iliyoanzishwa mwaka 1934 haina uwanja. Timu
ya Azam iliyoanzishwa juzi ina uwanja, timu ya Azam ina TV, timu ya Azam
imekuja juzi sasa inachukua wachezaji Yanga. Hii ni aibu, sisi ndio tunatakiwa
kuchukua wachezaji Azam”.
“Itafika mahali tutabaki tuna historia ya wanachama
nchi nzima, lakini hatuna maendeleo yoyote. Kama Azam wanachukua wachezaji wetu
manake itafika wakati na wanachama watahamia Azam”.
Akizungumzia kuhusu kuwa kiongozi wa Yanga kwa
mara nyingine, Mosha alisema hana kinyongo kuwa kiongozi wa klabu hiyo kwasababu
yeye sio kiongozi, lakini bado wanamfuata na hilo ndilo jambo la msingi zaidi.
“Sio unaonekana kiongozi halafu hauisaidii Yanga.
Mimi nina mapenzi na Yanga, sijawa na mapenzi na yanga jana au leo, nimekuwa na
mapenzi na Yanga miaka mingi”.
“Na ndio maana wana Yanga wengi wananikubali,
mambo ya Yanga mimi nabishana mpaka mwisho, nabishana mpaka kufa kuhusu Yanga.
Siwezi kusema labda kwasababu nyie waandishi mnaniuliza”.
“Devis Moshi ni Yanga na nitaendelea kuisaidia
Yanga. Si kwasababu ya kipato nilichonacho, hata kabla ya kipato”.
“ Kama unakumbuka historia ya nyuma, mimi nimekuwa
nikiisapoti Yanga tangu nikiwa timu ya Ushirika ya Moshi”.
Aidha, Mosha amewataka wanachama kuwa makini
kuelekea uchaguzi ujao utakaofanyika mwezi juni mwaka huu ili wasichague bora
kiongozi kwasababu wamejifunza.
Alisema wasimchague mtu kwasababu labda sura yake
ni nzuri na amejipaka mafuta wakaona anafaa, bali waangalie watu wenye historia
na mapenzi ya Yanga.
“Tumechukua watu wasiojulikana, hatimaye Yanga
yetu inakufa”.
“Mimi nilitoka kwenye uongozi baada ya kuona nina
watu wasioipenda Yanga, nikaona nisije kuchafua jina langu”.
“Ushauri wangu ni kwamba kiongozi anayekuja Yanga
awe ni Yanga na awe anaipenda Yanga na awe anatoa muda wake mwingi kuisaidia
Yanga”.
“Usitake kuwa kiongozi kwa kutaka jina, awe kiongozi
kwa kuonesha mapenzi yake na nia yake ya kuisaidia timu. Asije akachukua
uongozi halafu kesho akaona unamkera na kuamua kufanya mambo yake”. Aliongeza
Mosha.
0 comments:
Post a Comment