Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
NAHODHA wa zamani wa Taifa stars na kiungo wa
Simba sc msimu uliopita, Henry Joseph Shindika amesema kwasasa ni mchezaji huru
na anakaribisha klabu yoyote kufanya mazungumzo.
Katika mahojiano maalum na mtandao huu, Joseph
amesema bado anahitaji kucheza soka nchini Tanzania, japokuwa kuna mchakato
anaufanya na kama atafanikiwa anaweza kwenda nje ya nchi.
“Nimemaliza mkataba Simba, naweza kucheza klabu
yoyote ya hapa nyumbani, cha msingi ni kuzungumza juu ya maslahi”.
Joseph alisema Simba sc hawajazungumza na yeye kuhusu
kuongezewa mkataba, hivyo timu yoyote itakayokaa mezani na kuelewana, atafanya kazi bila tatioz lolote.
Kiungo huyo
aliipongeza TFF kuongeza timu mbili msimu wa 2015/2016, lakini aliongeza
kuwa zinatakiwa kufika ishirini kwasababu kwa sasa ligi ni fupi sana.
“Sijui kwanini timu zipo chache, labda ni wadhamini,
lakini nashauri ziongezwe zaidi. Tunamaliza ligi mapema mno, halafu hakuna
mashindano mengine kama kwa wenzetu”.
Aidha, Joseph alisema bado anajiona yupo katika
kiwango kizuri japokuwa hakuwa na namba ya kudumu katika klabu ya Simba sc.
“Nadhani ni mipango ya mwalimu. Mimi nilijiona
kabisa ninaweza kuisaidia timu, lakini sikuwa na nafasi. Sijui kwa nini, nafikiri
mwalimu anajua”. Alisema.
Pia aliongeza kuwa wachezaji wengi wa Tanzania
hawana uelewe wa mikataba yao, hivyo ni muhimu kutafuta mawakala au mameneja
ili wachezaji wapate haki zao za msingi.
“Wachezaji wengi wanasaini tu mikataba bila
kupitia vipendekele vyote. Watafutwe mawakala wazuri ili kuepusha kuvunjiwa
mikataba bila kupewa haki zao”.
Akizungumzia ushindani wa ligi, Joseph alisema
bado haoni kama wachezaji wanashindana katika mechi, hasa timu za chini.
“Nimecheza ulaya, utakuta timu ipo nafasi za
mwisho, lakini wachezaji wanapigana mno kwa lengo la kupata ushindi. Hata kama
watashuka daraja wanajua kuna timu zitawahitaji”.
“Ukija hapa nyumbani unakuta wachezaji wanaonekana
kukata tamaa mapema”.
‘Pia masuala ya maslahi yamekuwa yakiwaathiri sana
wachezaji wa ligi yetu”.
“Sisi ni watanzania na tunayajua maisha yetu.
Utakuta mchezaji ana familia au ndugu, sasa kama halipwi hawezi kufanya kazi
nzuri”.
“Wenzetu wanajituma sana hata kama kuna matatizo
katika timu. Malengo yao yanakuwa mbali sana”.
0 comments:
Post a Comment