
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
MOJA ya kununi ya kusaka mafanikio ni kuendeleza pale unapofikia ili kutimiza ndoto zako.
Mfano
kama ulipanga kupata shilingi milioni moja kwa mwaka, lakini ukaishia
laki 3, mwakani unatakiwa kuanzia laki 3 kuendelea kuisaka milioni moja.
Ukianza upya basi utashindwa kutimiza malengo yako uliyojiwekea.
Hata kwenye mpira wa miguu kanuni hii inatumika kwa klabu zenye malengo ya kufika mbali.
Kama msimu huu klabu imefanikiwa kushika nafasi ya pili, basi msimu unaofuata inatakiwa kutafuta ubingwa.
Klabu ikishika nafasi ya tatu basi itakuwa imeshindwa kuendeleza mafanikio yake ya msimu uliopita.
Azam fc wamefanikiwa kwa hili katika michuano ya ligi kuu kwasababu wameendeleza pale walipokuwa wanafikia.
Walishashika nafasi ya pili mara mbili mfufulizo, wakajipanga na kuendeleza mafanikio hayo na hatimaye kutwaa ubingwa mwaka huu.
Rekodi nzuri kwao ni kutwaa ubingwa huo bila kufungwa mechi yoyote.
Ukija
kwa apande wa michuano ya kombe la shirikisho ambayo wameshiriki mara
mbili mfululizo, hapa Azam fc wameshindwa kuendeleza pale walipofikia.
Mwaka
jana walifika hatua ya tatu na almanusura wafuzu hatua inayofuata kama
John Bocco angefunga penati ya dakika za lala salama dhidi ya AS FAR
Rabat mchezo wa marudiano nchini Morocco.
Lakini mwaka huu walitolewa hatua ya awali kabisa na Feroviario de Beira ya Msumbiji. Kwa maana hiyo walishindwa kuendeleza walipofikia.
Kama unashindwa kuendeleza mafanikio uliyoyafikia, basi ujue kuna mambo huyaende sawa katika mipango yako.
Mwaka huu waliokuwa mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans wamevuliwa ubingwa wao na Azam fc.
Watu wengi walikuwa na matarajio makubwa kuwa Yanga wangetetea ubingwa wao kutokana na usajili waliofanya na maandalizi kwa ujumla.
Ni kweli Yanga walionekana kuwa na kikosi cha nguvu kwa kutazama majina ya wachezaji nje ya uwanja.
Lakini inapofika ndani ya uwanja, mambo huwa ni tofauti, timu bora inaweza kupoteza mchezo kwa timu inayoonekana ya kawaida.
Wataalam wa mpira wanasema mpira wa miguu ni mchezo wa makosa. Ili ufunge lazima mpinzani wako afanye makosa.
Hivyo unaweza kuwa na wachezaji wazuri, lakini wakafanya kosa moja na kupoteza mechi.
Kitakachobaki
kusemwa ni timu ilicheza vizuri na kuwazidi wapinzani wetu kwa kila
kitu, lakini hatukuwa na bahati au chenga twawala magoli watufunga.
Ndiyo,
bahati pia ipo katika maisha. Kuna timu huwa hazima makali, lakini zina
bahati ya kupata matokeo muhimu kwa wakati sahihi.
Mfano
jinsi Mgambo walivyopata matokeo muhimu kutoka kwa Yanga ndani ya
uwanja wa Mkwakwani kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Ushindi huu umekuwa msaada mkubwa kwao kuendelea kubaki ligi kuu msimu ujao.
Achana na hayo, ngoja nirudi kwenye pointi yangu ya msingi katika makala hii.
Yanga kukosa ubingwa msimu huu si dhambi hata kidogo. Katika mpira wa miguu kushinda ni haki ya kila klabu.
Azam fc kutwaa ubingwa ni haki yao wala hakuna tatizo, hata Mgambo, Mbeya City, Kagera wana haki ya kufanya hivyo.
Kinachozinyima nafasi baadhi ya timu kufanikiwa kutwaa ubingwa au kupata nafasi tatu za juu ni kukosekana kwa maandalizi na uwekezaji katika klabu.
Kwa Simba na Yanga imekuwa faraja kwao kwasababu wana uwezo wa kifedha na wana mtaji mkubwa wa wanachama.
Mbali na hilo, wapo vigogo wenye pesa zao ambao ni msaada kubwa kwa klabu hizi.
Ndio maana zinaweza kusajili wachezaji wazuri na kuweka kambi hata Ulaya.
Kwa uwezo wao, Simba na Yanga wamekuwa wafalme wa soka nchini na imekuwa utamaduni kuwaona wakipokezana ubingwa.
Hii ikakaa akilini mwa watu wengi kuwa lazima Yanga au Simba ichukue ubingwa.
Mambo yanapoenda tofauti kama msimu huu ambapo Bingwa mpya amepatikana, basi yanasemwa mengi.
Ukipita mitaani mashabiki wanasikika wakisema bora Simba na Yanga zote zimekosa ubingwa.
Kwa wale wa Simba wanaonekana kufurahi zaidi kwasababu wao wameshindwa kabisa kuonesha makali msimu huu.
Kukosa ubingwa kwa Yanga imekuwa faraja kubwa kwa wana Simba.
Ndio maana baadhi ya viongozi wao wanashindwa kujizuia na kueleza wazi kuwa wamefurahi Yanga kukosa ubingwa.
Yanga wanahukumiwa mno kwa kukosa ubingwa, lakini swali la msingi ni kuwa lazima wao wachukue ubingwa?
Kama Azam fc walifanya maandalizi mazuri zaidi yao, kwanini wasichukue ubingwa?
Matarajio ya wengi ilikuwa kuona Yanga wanatete ubingwa wao.
Hata mimi niliamini hivyo, lakini mwendo wa Azam fc ulinipa mashaka kwa muda mrefu.
Kila nikienda kuwatazama kwenye mechi zao na mazoezi, niligundua kuna kitu wanahitaji na mwisho wa siku mawazo yangu yakatimia.
Yanga wamekuwa na wachezaji wazuri , na walifanya kazi kubwa katika ligi ya mabingwa barani Afrika.
Miaka mingi Yanga wamekuwa wateja wa timu za Misri, lakini mwaka huu mambo yalikuwa magumu kwa mafarao.
Al Ahly walifungwa bao 1-0 uwanja wa Taifa, walipoenda kwao Misri waliwafunga Yanga bao 1-0 na wastani kubaki 1-1.
Mshindi aliamuriwa kwa mikuwaju ya penati ambapo Al AAhly walifunga penati 4-3.
Mbali na kutolewa kwa penati, kiukweli Yanga walicheza mpira mzuri na kuwapa watanzania wengi matumaini ya kuwatoa Al Ahly.
Hata
mimi niliamini kwasababu kiwango cha Yanga uwanja wa Taifa na kule
Misri nilitegemea kuona rekodi ya Simba 2003 dhidi ya Zamalek.
Penati
nazo zina bahati yake, licha ya mlinda Mlango wa Yanga, Deo Munish
`Dida` kufanya kazi nzuri ya kuokoa penati mbili, lakini bado bahati
haikuwa kwa Yanga hasa baada ya Said Bahanuzi kukosa penati muhimu mno.
Baada ya kutoka, Yanga walisema wanarudisha nguvu zao ligi kuu ili kutetea ubingwa.
Hatua waliyofikia ligi ya mabingwa na kiwango chao kilivyokuwa juu, walihitaji kupata nafasi nyingine mwakani.
Walijiandaa vizuri na walisajili wachezaji wazuri, hivyo ingekuwa bahati nzuri kwao kama wangerudi tena msimu ujao.
Bahati mbaya timu zetu huwa haziendelezi pale zinapofikia.
Hivi unadhani ile Simba iliyokuwa na makali 2010/2011 iko wapi?
Wachezaji wangapi wa timu ile wapo sasa hivi kama si Amri Kiemba na Masud Nassor Cholo pekee?
Simba walionesha soka safi, lakini wakashindwa kuyaendeleza mafanikio yale.
Timu zetu zina tabia ya kuanza upya na kujikuta zikipiga mwendo wa nenda rudi.
Yanga
wameshindwa kutetea ubingwa wao na kukosa bahati ya kuendeleza
walipofikia, lakini kupata nafasi ya pili na kushiriki kombe la
shirikisho si haba kwao.
Kama wamekosa nafasi ya ligi ya mabingwa, basi sasa waanze maandalizi ya kombe la shirikisho.
Kama
kikosi chao kitabaki kama kilivyo au watapunguza baadhi ya wachezaji na
kuongeza nguvu, naamini wataweza kufanya vizuri kombe la shirikisho.
Uongozi uwaamini makocha na wachezaji wao ili waweke mipango ya pamoja kuelekea michuano hii mikubwa barani Afrika.
Kocha mkuu, Hans Van der Pluijm anafahamu wapi kuna madhaifu katika kikosi chake.
Ni muhimu kuzingatia mapendekezo yake kama mtaalamu wa benchi la ufundi.
Najua juni 15 mwaka huu ni mkutano mkuu wa uchaguzi wa Yanga ambapo tunaweza kushuhudiwa safu mpya ya Uongozi.
Mwenyekiti
wa sasa Yusuf Manji ambaye ni msaada mkubwa kwa klabu ya Yanga
alishatangaza kutogombea, japokuwa mpaka sasa haijulikani kama kweli nia
yake ipo palepale.
Uongozi
utakaopatikana, lazima utambue kuwa Yanga inahitaji kuhamisha nguvu
zake walizowekeza ligi ya mabingwa kwenda kombe la shirikisho.
Wataalum wa soka wanasema mwisho wa mechi moja mwanzo wa mechi nyingine.
Mwisho wa msimu mmoja mwanzo wa msimu mwingie. Lazima usahau ya nyuma na ugange ya mbele.
Kuna umuhimu wa kutumia makosa ya nyuma ili kuboresha ya mbele.
Yanga waangalie walipojikwaa na kuweka mikakati mizuri ya baadaye.
Waepukane na maneno ya mtaani ili waendelee kufanya yao.
Kikosi chao ni kizuri na kinahitaji marekebisho machache tu ili kuwa tayari kwa michuano ya kombe la shirikisho.
Cha msingi waanze maandalizi ya mapema, wasajili vizuri na kuweka timu pamoja kwa muda mrefu.
Kumbuka
kupanda daladala si dhambi. Kila mtu anaweza kupanda daladala, lakini
kwa Rais wa nchi inaonekana haiwezekani na ni ajabu.
Kinachofanya Rais aogope kupanda daladala ni hadhi yake aliyonayo.
Huo ni mfano mkubwa sana, rudi kwa watu maarufu kama wasanii, wanamichezo na wanasiasa.
Inafika wakati hawawezi kutumia usafiri wa Umma kutokana na majina yao.
Umaarufu unakufanya usemwe sana na wakati fulani kukunyima uhuru.
Yanga wakumbuke hili, kusemwa kwao, kupondwa kwao kwasababu ya kukosa ubingwa ni kwasababu ya ukongwe wao, na hadhi yao kama ilivyo kwa Simba.
Timu hizi mbili zitaendelea kuwepo kwasababu zimeingia damuni mwa watu.
Hivyo wajifunze kupuuza maneno ya mitaani na kujikita kufanya mambo ya msingi.
Yanga jipangeni upya, acheni maneno yanayoweza kuwagawa ili mfanye vizuri kombe la shirikisho.
0 comments:
Post a Comment