Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati leo (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu
zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam fc wakikabidhiwa kombe lao
Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili
jioni.
Mtandao huu unajaribu kukupatia tathmini ya mechi
zote saba zikazopigwa leo hii.
YANGA SC VS SIMBA SC
Mechi hii haina mchecheto sana kwasababu timu zote
zimeshapoteza nafasi ya ubingwa, japokuwa lengo kubwa leo hii ni kutafuta
heshima kwa klabu zote.
Simba wamefanya vibaya msimu huu na kuelekea
kuishia nafasi ya nne ambayo inategemeana na matokeo watakayopata dhidi ya
Yanga, wakati huo huo matokeo ya Kagera Sugar waliopo nyuma yao yakisubiriwa
huko Mkwakwani.
Simba wamecheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 37
katika nafasi ya nne, wakati Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 55 kwa
kucheza mechi 25.
Endapo Yanga watashinda leo, basi watafikisha
pointi 58, lakini hazitawasaidia kitu zaidi ya kulinda heshima, kwasababu Azam fc walishazivuka na kuchukua
taji msimu huu.
Kwa mazingira haya matokeo ya ushindi kwa timu
yoyote hayatakuwa na maana hususani kwa Yanga, lakini angalau Simba yanaweza
kuwahakikishia kushika nafasi ya nne.
Makocha wa timu hizi, Dravko Logarusic ( Simba) na Hans Van der Pluijm (
Yanga) wanakutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya watani wa jadi.
Lakini Loga aliwashawahi kuonja raha ya ushindi
desemba 21 mwaka jana baada ya kuwafunga Yanga mabao 3-1 kwenye mechi ya `Nani Mtani
Jembe`.
Pluijm leo ndio mara yake ya kwanza kukutana na
presha ya mechi ya watani wa jadi.
Yanga na Simba zinakutana zikiwa na malengo
yanayofanana, ingawa Simba wanakuwa kwenye presha kubwa zaidi.
Kama kweli wamedhamiria kupata nafasi ya nne, basi
ni muhimu kushinda kwasababu wakifungwa wataipoteza endapo Kagera Sugar
watashinda.
Kwa ujumla heshima ni muhimu sana na ndio maana
timu hizi zilijificha kambini ambapo Simba walijichimbia Zanzibar na Yanga walikuwa
Kunduchi jijini Dar es salaam.
Kwahiyo mechi hii itakuwa na ushindani mkubwa na
timu yoyote inaweza kushinda.
JKT RUVU V AZAM FC
Mechi hii itapigwa katika uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itatumika kuwakabidhi Azam fc ubingwa
wao wa kwanza waliofanikiwa kuutwaa.
Kwa mechi 25 walizocheza, Azam fc hawajafungwa
hata mechi moja, na leo hii wanahitaji kushinda ili kuandika historia ya kubeba
taji lao la kwanza bila kufungwa.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amewataka
wachezaji wake kucheza kwa kujituma ili kushinda mechi ya leo na kushangilia
ubingwa kwa raha zote.
Baada ya mechi hii, Azam fc wameandaa sherehe za
kushangilia ubingwa wao huko Chamazi, hivyo ushindi utanogesha zaidi.
Kwasababu hii ya Azam kutaka kuandika rekodi,
mechi hii itakuwa ngumu kwa kocha wa JKT Ruvu, Fredy Minziro.
Hata hivyo kama Minziro atapoteza mechi hii
haitakuwa na madhara kwake kwasababu poiniti 31 alizonazo sasa katika nafasi ya
10 zinamfanya awe mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwa ujumla mechi itakuwa na mvuto kwasababu Azam
fc wanahitaji kushinda.
TANZANIA PRISONS VS ASHANTI UNITED
Hii ni mechi ngumu
mno na inahitaji maarifa makubwa kwa kocha wa Ashanti, Mzee Abdallah Kibadeni
na David Mwamwaja wa Tanzania Prisons.
Kati ya timu hizi mbili, moja lazima
iungane kushuka daraja na timu za JKT Oljoro ya Arusha na Rhino Rangers ya
Tabora.
Timu zote zimecheza mechi 25 na
kujikusanyia pointi 25. Kinachozitofautisha ni mabao ya kufunga na kufungwa.
Prisons wamecheza mechi 25 ambapo
wameshinda mechi 5, sare 10 na kupoteza mechi 10.
Wajelajela hao wamefumania nyavu mara
25 na kufungwa mabao 33. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa unapata hasi (-8).
Ashanti United wameshinda mechi 6, sare
7 na kufungwa mechi 12.
Wamefunga mabao 20 na kufungwa mabao
38. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa anapata hasi kumi na nane (-18).
Kwa wastani huo wa mabao ya kufunga na
kufungwa, Prisons wanakuwa juu ya Ashanti United.
Katika msimamo, Prisons wapo nafasi ya
11, huku nafasi ya 12 ikikaliwa na Ashanti United, lakini zimefungana pointi.
Kuelekea
katika mechi hiyo, klabu zote zinahitaji ushindi, lakini Ashanti ndio wahitaji
wakubwa zaidi kwasababu wamezidiwa mabao mengi ya kufunga na Prisons.
Endapo
Ashanti United watashinda mechi hiyo watafikisha pointi 28 na kuvuka mkasi wa
kushuka daraja, wakati Prisons watakuwa wameshashuka daraja.
Matokeo
ya sare ya aina yoyote ile yatawashusha daraja Ashanti kwasababu ya wastani wa
mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama
Prisons watapata sare siku ya leo, watakuwa wamenusurika kushika daraja kwa
faida ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kitendawili
cha timu gani inashuka baina ya Prisons na Ashanti United kitageguliwa kesho
uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
MBEYA
CITY FC VS MGAMBO JKT
Hii
itakuwa mechi muhimu kwa kocha mkuu wa klabu hiyo ya Mbeya City fc, Juma Mwambusi kutokana na matokeo aliyoyapata
wiki iliyopita dhidi ya Azam fc ambapo alifungwa mabao 2-1 nyumbani na kuwapa
ubingwa rasmi.
Endapo
Mwambusi atashinda mechi hii, basi itakuwa faraja kubwa kwake na kwa
mashabiki wa klabu hiyo iliyoleta ushindani mkubwa mno msimu huu.
Mbeya
City FC mpaka sasa wamecheza mechi 25 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi
ya tatu ambayo tayari wamefanikiwa kuichukua.
Kwa
upande wa Mgambo JKT, wanauchukulia mchezi huo kwa uzito wa hali ya juu ili
kuweza kupata pointi tatu muhimu na kufikisha pointi 29.
Japokuwa
maafande hawa wapo nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi 25 na kujikusanyia
pointi 26 na kujiweka mazingira mazuri ya kubaki ligi kuu, lakini bado
wanahitaji ushindi katika mechi ya leo.
Kwa
mazingira haya, mechi hii itakuwa na mvuto mkubwa na soka la ushindani
linatarajiwa.
COASTAL
UNION VS KAGERA SUGAR
Katika
mechi hii itakayopigwa uwanja wa Mkakwani, timu zote zinaingia kwa mitazamo
tofauti.
Coastal
Union hawana cha kupoteza, lakini wakishinda
wanaweza kusogea nafasi moja mbele kutegemeana na matokeo watakayopata Mtibwa
Sugar leo hii.
Wagosi
wa Kaya waliotabiriwa kufanya makubwa msimu huu wamedoda katika nafasi ya 9 kwa
pointi 29 baada ya kucheza mechi 25.
Mtibwa
wapo nafasi ya 8 kwa pointi 30, hivyo wakifungwa leo hii wataporomoka nafasi
moja chini.
Kagera
wao wanahitaji pointi tatu muhimu ili angalau kuambulia nafasi ya nne, lakini
kama Simba watafungwa leo ndio itawasaidia.
Kagera
wapo nafasi ya 5 kwa pointi 35 na kama watashinda watafikisha 38, na kama Simba
wenye pointi 37 watafungwa, basi watachukua nafasi ya nne.
Kwa
mazingira haya, Kagera Sugar watakuwa washindani wazuri leo hii na kuufanya mchezo
uwe na mvuto.
RHINO
RANGERS VS RUVU SHOOTING
Mechi
hii haitegemewi kuwa ya ushindani hata kidogo kwasababu matokeo ya ushindi yatawasaidia
Ruvu Shooting kusogea nafasi ya juu
kutoka ya 6 kwenda ya 5.
Ruvu
Shooting wapo nafasi ya 6 katika msimamo wakiwa na pointi 35 swa na Kagera,
lakini Wakata miwa wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama
Kagera na Simba zitafungwa leo, halafu Ruvu Shooting wakashinda, basi
watafanikiwa kuchukua nafasi ya 4.
Rhino
walishashuka daraja, hivyo hawana wanachokitafuta leo hii zaidi ya kukamilisha
ratiba tu.
Kwa
ujumla mechi hii itakuwa na presha kwa Ruvu Shooting kwasababu watakuwa
wanahitaji matokeo mazuri huku wakiwaombea mabaya Simba na Kagera.
JKT
OLJORO V MTIBWA SUGAR
Mechi
hii haina jipya kwasababu Oljoro wameshashuka daraja msimu huu.
Mtibwa
watahitaji ushindi ili kuendelea kukaa nafasi yao ya nane.
Kwa
ujumla mechi hii haitakuwa na msisimko hata kidogo na mpira wa kawaidia unategemewa,
japokuwa Mtibwa wanaweza kuingia kwa nguvu.
Mtandao
huu utakuletea matokeo ya mechi zote hapo baadaye.
0 comments:
Post a Comment