Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA
wapya wa ligi kuu soka Tanzania bara, wana Lambalamba, Azam fc wameamua
kuwapumzisha wachezaji wao kwa muda mrefu baada ya kufanya kazi kubwa
ya kubeba taji lao la kwanza tangu wapande ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tovuti ya klabu, wanandinga wa Azam fc
wamepewa likizo hadi juni 15 mwaka huu na baada ya hapo watarudi
kambini kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu na michuano ya
ligi ya mabingwa barani Afrika.
Kwa
misimu miwili mfululizo, Azam fc wameshiriki michuano ya kombe la
shirikisho inayoshirikisha washindi wa pili wa ligi za nchi mwanachama
wa CAF.
Lakini msimu ujao wanapanda na kushirikia CAF Champions League, moja ya michuano mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Jana
kilifanyika kikao cha pamoja baina ya wachezaji, viongozi na bodi ya
klabu kwa lengo la kupongezana na kuagana kwa likizo hiyo ndefu.
Katibu
mkuu wa klabu, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’ alisema benchi la Ufundi
kwa pamoja na wachezaji wanakwenda likizo vizuri baada ya mafanikio ya
msimu huu.
Wakati
huo huo, Uongozi wa Azam fc umesema nia yao ilikuwa ni kutwaa ubingwa
wa ligi kuu, na sasa wamefanikiwa, hivyo malengo yao yamebadilika ambapo
wanaanza kufikiria kufanya vizuri michuano ya kimataifa na kutwaa
ubingwa, huku wakizingatia kuwa wana wajibu wa kutetea ubingwa wao msimu
ujao.
Azam fc msimu huu imekuwa na mafanikio makubwa kwasababu licha ya kubeba taji, imefanikiwa kucheza mechi zote 26 bila kufungwa.
Wanalambalamba wamemaliza Ligi Kuu kwa kujikusanyia pointi 62 dhidi ya 56 za waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC.
Kwa
ubingwa huo , Azam inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa
ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 ambapo Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.
Azam
inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya
Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu
Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili
mfululizo 1999 na 2000.
Wakati
huo huo, Wachezaji wa akademi ya Azam nao pia wamepewa likizo hadi Mei
8, mwaka huu watakaporejea kuendelea na mafunzo ya soka ya kisasa.
Malengo ya Azam fc ni kuwekeza katika soka la vijana ili kuwa miongoni mwa klabu bora zaidi duniani.
Azam fc kwasasa ina karibu kila kitu kinachohitaji kwa klabu yoyote kwasababu imejenga uwanja mzuri wenye hadhi ya kimataifa.
Pia ina hosteli nzuri za wachezaji na mazingira kwa ujumla yanastahili kuwa klabu ya kisasa.
Kwa
uwekezaji mkubwa wanaofanya Azam fc wanastahili kuwa mfano wa kuigwa
kwa klabu nyingine zikiwemo Simba na Yanga ambazo zimekaa muda mrefu
katika soka la Tanzania, lakini hazina mipango makini na zinaendeshwa na
siasa zaidi.
0 comments:
Post a Comment