Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba sc wamesahau vipigo
vyote vya mechi za nyuma na sasa wameelekea visiwani Zanzibar kuweka kambi kujiandaa
na mechi dhidi ya Yanga SC aprili 19 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam.
Katibu mkuu wa Simba sc, Ezekiel Kamwaga ameuambia
mtandao huu dakika chache zilizopita kuwa kikosi cha wachezaji 18 kimeondoka
jioni hii kwenda Zanzibar kutafuta sumu ya kuwaua Yanga.
“Timu ipo katika hali nzuri. Yaliyopita si ndwele,
sasa akili yetu ni mchezo wa jumamosi dhidi ya mtani. Tuna matarajio makubwa ya
kushinda mechi hiyo”. Amesema Kamwaga.
Kamwaga amewatoa hofu mashabiki wa Simba ambapo
amewahakikishia kuwa maandalizi wanayoenda kuyafanya ni ya hali ya juu.
“Tumefanya vibaya msimu huu kinyume na matarajio
ya mashabiki wetu”.
“ Kuwafunga Yanga mechi ya mwisho itakuwa faraja
kubwa kwao. Uongozi umejiandaa vizuri na timu ipo katika hali nzuri kabisa”.
Ameongeza Kamwaga.
Hata hivyo taarifa zilizoenea mchana wa leo ni
kuwa wachezaji wa Simba waligoma kwenda Zanzibar wakishinikiza kulipwa
mishahara yao ya mwezi huu.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo,
Zacharia Hans Poppe alilazimika kuwalipa fedha wachezaji wote na benchi la
ufundi ili kuokoa jahazi, na jioni hii safari ilianza.
Simba sc wataingia uwanjani wakiwa na malengo ya
kushinda na kulinda heshima yao.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Dravko Logarusic
alikaririwa na mtandao huu akisema mechi ya mwisho ameipa uzito wa hali ya juu,
hivyo alihitaji kambi kuwepo maeneo tulivu.
Mechi hiyo haitakuwa na presha kubwa kwani matokeo
kwa timu zote hayatabadili chochote kwa maana ya Simba kupanda nafasi za juu
wala Yanga kuchukua ubingwa.
Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 55 baada ya
kucheza mechi 25, pointi nne nyuma ya Azam fc waliopo kileleni kwa pointi 59,
huku tayari wakiwa wameshajitangazia ubingwa kwasababu hakuna klabu inayoweza
kuzifikia pointi hizo.
Wachezaji waliondoka jioni hii ni walinda mlango
Ivo Philip Mapunda na Yaw Berko.
Walinzi ni William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid
‘Baba Ubaya’ Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassor Masoud ‘Chollo’.
Viungo Henry Joseph,
Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Uhuru Suleiman Jonas Mkude, Said Ndemla, Awadh
Juma, Ramadhani Singano ‘Mesi’, Haroun Chanongo, Amri Kiemba na washambuliaji ni
Amisi Tambwe na Zahor Pazi.
0 comments:
Post a Comment