Ronaldo alifunga bao la kwanza dakika ya sita kwa pasi ya Angel di Maria kabla ya kuongeza la pili dakika ya 52 kwa pasi ya Isco na Sergio Ramos akafunga la tatu dakika ya 60 kwa pasi ya di Maria kabla ya Daniel Carvajal kufunga la nne dakika ya 83 pasi ya Isco.
Ushindi huo, unaifanya Real itimize pointi 82 baada ya kucheza mechi 34 na inaendelea kukamata nafasi ya pili nyuma ya vinara Atletico Madrid wenye pointi 85 kwa kucheza mechi 34, huku FC Barcelona yenye pointi 81 za mechi 34 ikiwa ya tatu.
Kwa kiwango cha jana cha Ronaldo kinawapa tahadhari Bayern Munich kuelekea katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya keshokutwa jumanne katika uwanja wa Allianz Arena jijini Munich.
Mechi ya kwanza katika uwanja wa Santiago Bernabeu,bao pekee la Karim Benzema lilitosha kuwapa ushindi wa bao 1-0 Real Madrid.
Hata hivyo, harakati bado zinaendelea na malengo yao makubwa ni kufika fainali na kutwaa ubingwa wa UEFA.
Aidha, Real wanataka kutwaa taji la La Liga ambapo msimu huu mahasimu wao wa jadi, Atletico Madrid wameendelea kukaza mwanzo mwisho.
Baada ya mechi ya jana, Sergio Ramos alisema malengo yao ni kushinda mechi zote nne zilizosalia ili kuwapa presha mahasimu wao wa jiji la Madrid, vinara Atletico Madrid.
“Tumefurahi sana”. Beki huyo aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi.
“sasa tunatakiwa kuendelea hivi hivi mpaka mwisho wa msimu. Tuna mechi nne za fainali katika ligi, tutajitahidi kushinda zote na nadhani tutaweza”.
“Naamini matokeo ya leo (jana) tulistahili kupata kwasababu tulicheza kwa kujituma sana”.
Beki huyo mwenye miaka 28 ghafla alibadilisha maongezi yake na kuyaelekeza katika mechi ijayo ya UEFA dhidi ya Bayern Munich.
“Sasa tumefurahia ushindi na tunaanza kuwaza mechi ya UEFA. Tutajitahidi kushinda mechi hiyo ili tucheze fainali”.
Real Madrid Tayari wameshabeba kombe la Copa del Rey na wamebakiwa na mechi nne za La Liga dhidi ya Valencia, Valladolid, Celta na Espanyol.
0 comments:
Post a Comment