Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Timu ya
Watoto wa Mitaani kwa kutwaa Kombe la Dunia huko Rio de Janeiro nchini Brazil.
Taarifa iliyotolewa na ikulu imesema Rais Kikwete amefurahishwa
jinsi watoto hao walivyonyakua kombe hilo la dunia.
"Mmetuwakilisha vyema, ninawapongeza sana, pia mmewapa moyo
watoto wengine wote wenye vipaji maalum lakini hawakubahatika kuwa na makazi
rasmi, hongereni sana" Rais amesema.
Timu hiyo ya watoto wenye umri chini ya miaka 16 ilipangwa kundi
la 2 ambapo pia zilikuwapo timu kutoka Nchi za Argentina, Nicaragua,Philippines
na Burundi.
Makundi yaliyopangwa yalikuwa matatu.
Tanzania iliingia nusu fainali kwa kuwa mshindi wa pili na pia
kumenyana na Marekani na kuichapa mabao 6-1 na baadae kuitoa Burundi kwenye
fainali kwa mabao 3-1.
"
Hongereni kwa kujituma na kucheza kwa ustadi". Rais amesema na kuwaasa
watoto "ongezeni bidii, nidhamu na mazoezi ya kutosha na hakika
mtafanikiwa zaidi na kulibeba jina la Tanzania mbali zaidi ya hapa katika
ulimwengu wa soka duniani, kwani hakuna kisichowezekana kama mtazingatia
maelekezo, mafunzo, bidii na nidhamu ya yote mnayofanya" Ameongeza Rais
Kikwete .
0 comments:
Post a Comment