Tuesday, April 1, 2014




Ligi kuu imefikia kwenye kilele cha uhondo wake. Ni nadra kufikia hatua ya mashabiki wa Yanga kuiombea Simba matokeo mazuri. Jumapili, tulijikuta hapo, uadui uliwekwa pembeni kwa minajili ya maslahi. Mashabiki wa Yanga na Simba walidhibitisha kuwa hakuna rafiki wala adui wa kudumu bali kuna maslahi tu.
   
            “Ninaenda uwanja wa Taifa kuishangilia Simba kwa mara ya kwanza” - Amir Mohamed mwanachama wa Yanga toka 1973.

Mwisho wa siku, ilionekana kama vile Yanga ilipokea vipigo viwili, kufungwa na Mgambo na Simba kupoteza mchezo wake dhidi ya Azam. Mashabiki wa Yanga walioenda uwanja wa Taifa kuishangilia Simba walitoka na simanzi na wale waliojitokeza Mkwakwani waliondoka vichwa chini. Walivurugwa kote, Dar na Tanga.

Simba, wao walijitia hamnazo na kuonekana wenye furaha licha ya kuambulia kipigo kutoka kwa ‘ndugu’ zao wa Azam. Ni rahisi kuwaona Simba kama mambumbumbu fulani kuchekelea licha ya kutumiwa kama ngazi ya Ubingwa wa Azam. Kwa mashabiki wa Simba ni heri aibu ya kufungwa na Azam, isiyo na mashabiki, kuliko fedheha ya kelele za ubingwa wa Yanga, yenye mashabiki mpaka chumbani mwa mashabiki wa Simba.

Tukirudi uwanjani, licha ya kupokea vipigo stahili, Simba na Yanga walimiliki mpira zaidi ya Azam na Mgambo. Simba waliangushwa na woga wa kujaribu kupiga mashuti kila walipokaribia eneo la hatari la Azam. Yanga wao waliangushwa na papara langoni na kujikuta wakishambulia bila mpangilio wowote.
Takwimu za vipindi vyote viwili vilionesha Simba walimiliki zaidi mpira kuliko Azam. Walikuwa na mpangilio mzuri wa mashambulizi lakini wakashindwa kufunga mabao. Mashambulizi yao yalienda kwa mpangilio, kutoka kwenye idara ya ulinzi, kupitia katikati na pembeni kwenye kiungo hadi kwenye safu ya ushambuliaji. Walikuwa wanapiga pasi zinazoonekana machoni.

Tatizo lilikuwa kwenye kumalizia mashambulizi yao. Kulikuwa na woga wa kujaribu, wachezaji hasa viungo walikuwa wanaogopa kupiga mashuti licha ya kuwa hatua kadhaa kutoka langoni mwa Azam. Ukimuondoa Jonas Mkude, wachezaji wengine wa Simba walikuwa ni kama wana hofu ya kukosea, woga wa kupaisha mipira.

Mara kadhaa Simba walijikuta wakipigiana pasi nje tu au hata ndani ya sanduku ilhali walikuwa katika sehemu nzuri ya kumjaribu Aishi Manula aliyekuwa amekingwa na walinzi wake. Labda ukali wa Logarusic umewafanya wachezaji wa Simba kucheza kwa hofu ya kukokosea, wanacheza kama robot kwamba pasi lazima iende sehemu fulani.

Wachezaji wa Simba wamekuwa watumwa wa woga wa kupoteza pasi. Dhidi ya Azam, walikuwa wanafika langoni lakini unaweza kuhisi walikuwa wanaona ni heri kutoa pasi kuliko kujaribu na kukosa. Wanacheza kuepuka lawama za kukosea. Ndicho kilichowanyima ushindi Jumapili. Azam walicheza kwa uhuru, walitengeneza nafasi chache na kuzitumia, walistahili kuondoka na ushindi

 Gwiji wa Bulgaria, Hristo Stoichkov aliwahi kunukuliwa kuhusiana na woga, hii ilikuwa ni baada ya wao kuwafunga Ufaransa 2-1 na kuwakosesha fainali za kombe la Dunia 1994.
     " Wafaransa walijawa na woga kiasi cha kucheza wakiwa wamekaza makalio….walicheza kusaka sare     na sio kusaka ushindi. Hawakustahili kufuzu na tuliwanyoosha haswa’

Ndiyo, hata Simba walistahili kunyooshwa na Azam kwa kucheza kwa hofu ya kuogopa kukosea.
Kwa upande wa Yanga, wao papara ziliwaponza. Baada ya ushindi wa mabao 5 dhidi ya Prisons, Yanga hawakujiandaa kukabiliana na mazingira ya kutafuta bao la kusawazisha. Walikuwa wamejiandaa kwa karamu nyingine ya mabao lakini si kujikuta wakiwa nyuma dakika ya kwanza tu ya mchezo.

Bao la Fully Maganga lilikuwa kama fumanizi kwao. Ni kama mwanafunzi anayejiamini kwa kukariri mara ghafla akashtukizwa mtihani wa wiki ijayo umegeuzwa kuwa wa kesho.

Baada ya kufungwa bao, Yanga walicharuka na kuwashambulia sana Mgambo bila mafanikio. Mashambulizi ya Yanga yalikuwa hayana mpangilio. Mgambo walirudi nyuma kuzuia , hasa kwa kuwa walikuwa pungufu,  lakini bado Yanga wakaendeleza papara za kucheza kwa haraka kulifikia lango la Mgambo. Kwa hao, ilikuwa mbele daima, nyuma mwiko bila kujali idadi ya walinzi wa Mgambo.

Kifupi, Yanga hawakubadilisha mbinu, badala ya kujaribu kuwavuta Mgambo ili watoke eneo lao, wao waliendelea kucheza kwa staili ya counter attack. Unachezaje kwa kasi ya counter attack kwa timu iliyojaza wachezaji nyuma?

Mwisho wa siku, licha ya kuwaingiza Hussein Javu na Hamisi Kiiza bado mashambulizi ya Yanga yalionekana kama ‘ngumi za kukopa’ ambazo Mgambo wangeendelea kuzikwepa hata kama mechi ingepigwa kwa masaa mawili zaidi ya muda wa kawaida wa dakika tisini.

Yanga ya Okwi, Ngassa, Kavumbagu, Kiiza, Msuva na Javu si ya kuhitaji tuta la ‘asante’ kupata bao la kufutia machozi. Hakuna ubishi hii ndio safu kali zaidi ya ushambuliaji kwenye ligi kuu ila inawezekana kuna mbio binafsi za kuibuka mfungaji bora au kuonekana bora ndani ya klabu zinazowafanya Yanga kuwa na papara. Kila mchezaji anaamini anaweza kufunga, mipango na mikakati ya mashambulizi inapotea.

Imeandaliwa na : Michael Mwebe.

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video