Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
TANGU mwaka 2000 ambapo wana TamTam Mtibwa Sugar walitwaa taji, ubingwa
wa ligi kuu soka Tanzania ulikuwa kama mbio za kupokezana vijiti baina ya Simba
na Yanga, lakini msimu huu klabu hizo zimeshindwa kutamba mbele ya Azam fc.
Wanalamba wametawazwa mabingwa jana katika dimba la Sokoine baada ya
kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Mbeya City.
Ushindi huo umewafanya Azam fc kufikisha pointi 59 kileleni ambazo
haziwezi kufikiwa na waliokuwa washindani wao wakubwa, Yanga sc.
Timu zote zimebakiwa na mechi moja ambapo mwishoni mwa wiki hii, Azam fc
watakalimisha ratiba dhidi ya JKT Ruvu katika dimba la Azam Complex Chamazi, huku
tayari wakiwa mabingwa wapya na wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya ligi
ya mabingwa barani Afrika mwakani.
Watakaokuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la
shirikisho mwakani, Dar Young Africans watafunga pazia la ligi kuu dhidi ya
watani wao wa jadi, wekundu wa msimbazi Simba sc.
Mechi hizi mbili hazitakuwa na presha kubwa kama za jana kwasababu
tayari mambo yameharibika kwa Yanga na kuwa poa kwa Azam fc.
Kwa muda mrefu Azam na Yanga zimefukuziana kusaka ubingwa msimu huu,
lakini mwisho wa safari Wanalambalamba wamefanikisha ndoto zao.
Haya ni mafanikio makubwa kwa Azam fc kwasababu ndio ubingwa wao wa
kwanza tangu waanze kushiriki ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kabla ya ubingwa huu, Azam fc walifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la
Mapinduzi mara mbili mfululizo na kushika nafasi ya pili zaidi ya msimu mmoja.
Mcameroon, Joseph Marius Omog ameingia katika kitabu cha historia ya
Azam baada ya kuwa kocha wa kwanza kuipa ubingwa klabu hiyo.
Haya ni mafanikio mazuri kwa Omog, japokuwa amejenga kazi yake mabegani
mwa kocha aliyekaa zaidi Azam fc, Mwingereza
Sterwart John Hall.
Hall aliondoka Azam mwishoni mwa mzunguko wa kwanza akiiacha klabu bila
kufungwa mechi yoye, naye Omoga ameendelea kuilinda rekodi hiyo mpaka sasa.
Azam wameshuka dimbani mara 25 na hakuna timu yoyote iliyoondoka na
pointi tatu zaidi ya moja tu, huku wakibakiwa na mechi moja.
Rekodi nyingine kwa kocha Omog ni kuwa kocha wa kwanza kuifunga Mbeya
City katika uwanja wake wa nyumbani.
Kutokana na Mbeya City fc walivyo na nguvu katika uwanja wa Sokoine Omog
amefanya kazi kubwa na kuandika rekodi nzuri.
Naye John Raphael Bocco
`Adebayor` anakuwa mchezaji wa kwanza
katika historia ya Azam fc kufunga bao lililowapa ubingwa wao wa kwanza.
Hii ni historia nzuri kwa Bocco ambaye ni nahodha wa klabu hiyo.
Rekodi
nyingini ni Azam kuwa timu ya sita nje ya Simba
SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Tukuyu
Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999
na 2000.
Kocha Omog baada ya kuanza kazi yake kwa
mafanikio katika klabu ya Azam amefurahishwa sana na ubingwa walioutwaa mwaka
huu katika ligi yenye ushindani mkubwa mno.
“Ni furaha sana, tumepambana sana, haikuwa kazi nyepesi, tumepitia mengi magumu tangu naanza kazi hapa, lakinitulibaki kwenye dhamira yetu na tukaendelea kupambana hatimaye tumetimiza malengo. Sote tuna furaha sasa, kilamtu ana sababu ya kufurahia kazi yake kati yetu,”alisema Omog.
Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo ya jana, na badala yake waelekeze nguvu zao katika mchezo wa Aprili 19, ili washinde na kukabidhiwa Kombe kwa furaha.
“Nasikia Yanga walikata rufaa, hata kama haina maana, lakini lazima tushinde mechi ya mwisho, wachezaji wangu wanajua hilo, nimewaambia,”alisema.
Kikosi cha Azam kimeondoka leo Saa 10:00 asubuhi jijini
Mbeya kwa ndege kurejea Dar es Salaam na wachezaji watapewa mapumziko ya siku
moja kabla ya kukutana kwa maandalizi ya mchezo wa kufungia pazia la msimu.
0 comments:
Post a Comment