Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
BEKI wa kushoto wa zamani wa Yanga SC, timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa stars na sasa maafande wa Ruvu Shooting, Stephano
Mwasyika amewashauri vijana wanaochipukia katika soka kuiga mambo waliyofanya
kaka zao na kubuni mbinu mpya ili walisaidie taifa siku za usoni.
Katika mahojiano maalum na mtandao huu, Mwasyika
amesema akiwa Stars 2010 walichukua ubingwa wa CECAFA Senior Challenge Cup, lakini vijana wanatakiwa
kujituma zaidi ili kufika mbali kwasababu taifa lina uchu wa kupata mafanikio.
“Ukiangalia uongozi wa sasa wa TFF, nadhani kuna
kitu wamekiona mbeleni ndio maana wanawekeza nguvu kwa vijana”
“ Timu itaweza kufanya vizuri miaka ya 2017-18,
lakini kwasasa si rahisi kwasababu vijana wanatakiwa kuaminiwa na kupewa muda
wa kutosha”. Alisema Mwasyika.
Mwasyika amewataka watu kuwapa moyo wachezaji
wanaochipukia ili kuwajenga zaidi.
“Wachezaji wanaochipukia hawajawa sawa
kisaikolojia. Anaweza kucheza vizuri mechi hii nyingine akachemsha”.
“ Kinachotakiwa kufanyika ni kmshauri na kuwatia
moyo, lakini anapotokea mtu anawapa kashifa inawaharibu na kuwaondoa mchezoni”.
Aliongeza Mwasyika.
Hata hivyo akaenda mbali zaidi na kuwashauri
wadogo zake kuwa katika mpira kuna changamoto kubwa, hivyo wasiwe wepesi wa
kukata tamaa kwa sababu ya maneno ya watu.
Beki huyo aliongeza kuwa kila mchezaji anataka
kucheza timu ya taifa ili baadaye aende kimataifa.
“Angalia mfano akina Samata, Ulimwengu ambao sasa
wamefika mbali kiasi”.
“Kwasasa wamekuwa wazoefu kwasababu wamecheza
mechi nyingi za kimataifa. Vijana waige mfano wao. Kikubwa wafanye kazi yao kwa
bidii na kutosikilza maneno ya watu. Alisema Mwasyika.
Aidha, Mwasyika amewashauri viongozi kutambua kuwa
mpira wa miguu huwa unabadilika, kuna wakati mchezaji anaweza kucheza vizuri na
kuna wakati ukamkataa.
“Watu wameshakariri kuwa Tanzania kuna kuuza mechi. Vitu kama hivyo vipo, mimi
sikatai. Lakini kuna wakati mwingine viongozi wanawapa lawama wachezaji bila kujua kitu”.
“Unaposikia mtu kauza mechi na unaanza kuzungumza
lazima uwe na uhakika”.
“Siku hizi kuna mitandao, kama mtu ametumiwa hela
unaweza kujua tu ukifuatilia. Utajua kuna hela ilitumwa kutoka kwa mtu fulani
kwenda kwa mtu fulani”.
“Viongozi wa siku hizi wanatengeneza kama majungu fulani
kwenye timu. Utasikia fulani kauza mechi, lakini hawana uthibitisho. Timu ikifungwa
utasikia mechi imeuzwa, mara marefaa wamenunuliwa, lazima tuwe tunafuatilia
zaidi”. Alisema Mwasyika.
0 comments:
Post a Comment