Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi amesema kuwa kuwaamini vijana katika klabu kunahitaji kuwapa muda ili kufikia malengo.
Mwambusi amesema kuna mambo mawili yanatakiwa
kuzingatiwa katika falsafa za mpira.
Mosi; falsafa ya mpira huwezi kuwajumuisha makocha
wote kwasababu kila mtu ana falsafa yake.
Pili; kila klabu inakuwa na falsafa yake, hivyo
inahitaji kocha atakayeiweza .
Mwambusi aliendelea kufafanua kuwa klabu inapokuwa
na falsafa yake, mfano kutumia soka la vijana, lazima inakuwa na falsafa
mbadala ili kama itashindikana mpango A basi waende mpango B.
Kocha huyo alisema si jambo la ajabu kuona timu
inabadili mfumo wa soka lake ndani ya msimu mmoja, lakini inategemeana na
malengo ya klabu.
Akizungumzia falsafa kwa Makocha, Mwambusi alisema
kuna changamoto kubwa kwa walimu wa kitanzania kwasababu huwa hawajiamini
katika mifumo yao.
“Kama viongozi wanataka mageuzi na mwalimu
akakubali mageuzi bila kuzingatia mfumo wake, basi mwalimu naye atakuwa amefeli”.
“Mwalimu anatakiwa kushikilia msimamo wake na
kuwaambia viongozi kuwa kama wanataka mfumo wao, basi watafute mwalimu mwingine
atakayeweza kufanya kazi hiyo”.
“Mwalimu lazima uwe na msimamo na usifanye kazi
kwa kushinikizwa na watu fulani”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi alibaanisha kuwa walimu wengi wa
Kitanzania wanashindwa kujiamini kwasababu hawaaminiwi.;
“Viongozi wanafanya kazi kwa mazoea. Kila
unachokifanya kocha wa Kitanzania wanapuuzia. Hii inatokana labda na kutuzoea”.
“Inafika muda viongozi wanaona wachukue makocha wa
kigeni kwa kuamini watapata kitu fulani, lakini inakuwa tofauti”.
“Walimu wote tunasoma mpira kinadharia kama
wenzetu, lakini linapofika suala la falsafa ni msimamo wa mwalimu mwenyewe”.
“ Kikubwa viongozi watuamini na kuona kama
tunaweza kufanikisha malengo ya klabu zetu”. Alisema Mwambusi.
Kocha huyo alifanikiwa kuipa nafasi ya tatu Mbeya
Cit fc msimu huu kwa kufikisha pointi 49 alisema kwa upande wake ana msimamo
mkali na anaamini katika vitu vyake.
“Siku zote nina falsafa yangu na ninaiamini sana.
Siwezi kuibadili bila kujali nitapoteza kazi”. Alisema Mwambusi.
Pia Mwambusi amewaomba makocha wenzake kutumia
muda wao mwingi kulea vipaji vya wachezaji vijana.
“Isiwe kuwafundisha tu jinsi ya kupiga mpora. Pia
tujikite katika masuala ya nidhamu, ndani na nje ya uwanja”.
“Saikolojia nayo lazima ipewe kipau mbele kwa
wachezaji vijana ili kuwajenga katika misingi bora”. Alisema Mwambusi.
Aidha, aliwataka viongozi wa klabu kuwajibika
katika majukumu yao ili kuwaweka wachezaji katika mazingira mazuri hususani
mishahara na posho zao.
“Mpira unahitaji sana saikolojia. Hata aje Messi
au Ronaldo hapa, halafu akafiwa na mama yake na umwambie tutakupa milioni 10
cheza mechi hii tu, sidhani kama atacheza vizuri”.
“Maslahi ni muhimu, lazima wachezaji wapate fedha
zao mwisho wa mwezi. Viongozi wajipange kufanya vitu vya msingi kwa wachezaji”.
Alisisitiza Mwambusi.
0 comments:
Post a Comment