YANGA SC imeamua kukirudisha kikosi chake kambini Bagamoyo kwa ajili ya mechi zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara- kuanzia Jumapili dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji wa Yanga SC wanatarajiwa kukutana makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwa safari ya Bagamoyo ambako wataweka kwa ajili ya mechi na JKT Ruvu.
Hatua hiyo inakuja baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili hivyo kupunguzwa kasi katika mbio za ubingwa ambako inafukuzana na Azam FC.
Wazee wa Bagamoyo; Yanga inaingia kambini katika hoteli ya Kiromo leo |
Matokeo hayo yanaifanya Azam iendelee kubaki kileleni kwa pointi zake 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC inabaki na pointi zake 46 baada ya mechi 22 katika nafasi ya pili mbele ya Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23.
Tangu Januari mwaka huu iliporejea kutoka kambi ya mafunzo ya siku 10 na zaidi nchini Uturuki, Yanga imekuwa kambini katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani na ilihama huko kwa wiki moja kujiandaa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misiri.
Yanga iliyoweka katika katika hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ilitolewa katika Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Tangu iliporejea Dar es Salaam kutokea Misri, Yanga SC haikurudi Bagamoyo na katika mechi nne ilizocheza ilishinda moja tu dhidi ya Prisons ya Mbeya 5-0, mbili ikitoa sare na Azam FC 1-1 na Mtibwa Sugar 0-0, wapinzani wake wote wakiwa pungufu baada ya kupoteza wachezaji kwa kadi nyekundu.
Hata mechi yake iliyopita ikilala 2-1 Tanga, pia wapinzani wake Mgambo walipoteza mchezaji kwa kadi nyekundu.
CHANZO: BIN ZUBEIRY
0 comments:
Post a Comment