
Ally Mayay (wa pili kushoto kwa waliochuchumaa) enzi zake akiichezea Yanga SC
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
BEKI
na nahodha wa zamani wa Yanga SC, Ally Mayay Tembele amewaasa viongozi,
wachezaji na mashabiki wa klabu za ligi kuu soka Tanzania bara kutambua
kuwa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa.
Akihojiana na mtandao huu Mayay alisema wachezaji wanapokosea wanabebeshwa lawama na kupata hukumu kubwa ikiwemo kusimamishwa na klabu zao.
“Mpira
wa miguu ni mchezo wa makosa. Ili mchezaji afunge goli, lazima mchezaji
pinzani afanye makosa. Huwezi kufunga goli kama mpinzani wako
hajakosea”.
“Kwa
bahati mbaya Watanzania wengi tunaangalia mpira wa Ulaya kwa jicho
lingine na mpira wa Tanzania kwa jicho lingine. Anapofanya kosa
Ferdinand au David Luiz kwa wenzetu wanachukulia kawaida”.
“Wanatambua
kuwa makosa ni sehemu ya mchezo. Lakini akifanya kosa hilo kwa mfano
Yondani, Mosoti au mchezaji yeyote, kwetu utaambiwa kapewa rushwa. Ifike
muda nasisi tusiwahukumu sana wachezaji”. Alisema Mayay.
Mayay
aliongeza kuwa maneno mengi ya wachezaji kuuza mechi yanaanzia kwa
mashabiki wa soka na kwa habati mbaya viongozi nao wanayabeba kama
yalivyo.
“Kiongozi unaposikia mchezaji wako kahongwa, usibebe kama yalivyo, lazima kwanza ujiridhishe mwenyewe kwa kutafiti.”
“Halafu ukumbuke kuwa makosa huwa yapo katika mchezo. Baada ya hapo amua sasa atakavyo”. Alisema Mayay.
Akizungumzia ligi ya msimu huu, Mayay alisema ilikuwa nzuri na ya ushindani mkubwa hususani kwa nafasi ya ubingwa.
‘Binafsi
nilifurahishwa sana na kasi ya Mbeya City fc, imeifanya ligi iwe bora
na yenye mvuto. Hawa jamaa wameifanya ligi kuwa maarufu na kuzungumzwa
sana”.
‘Sishangazwi
na Azam fc kutwaa ubingwa. Tayari kwa misimu miwili walishika nafasi ya
pili. Walichokuwa wanakitafuta msimu huu ni ubingwa. Wamekuwa bora na
waliwekeza sana. Nadhani wamestahili”.
“Msingi
wa Azam fc ulijengwa na kocha Muingereza Sterwart John Hall na
alipokuwa anaondoka alimuandikia mrithi wake Joseph Omog kila kitu.
Hakika alimpa njia nzuri na Omog alikuja kumalizia kazi ya Sterwart”.
“Omog amekuwa muungwana sana kwasababu amekubali kuwa mafanikio yake yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Sterwart”. Alisema Mayay.
Kuelekea
msimu mpya wa 2014/2015, Mayay alisema anatarajia ligi nzuri zaidi ya
msimu huu kwasababu kumekuwepo na ongezeko la timu za wananchi.
‘Sina
hakika, lakini nadhani Ndanda fc na Stand United zinaweza kufanya
vizuri msimu ujao. Najua wananchi wanaozizunguka klabu hizi wameiga
mfano wa watu wa Mbeya. Nafikiri itakuwa ngumu kwa timu nyingine kutoka
na pointi tatu maeneo ya Shinyanga na Mtwara”.
“Natarajia ligi bora zaidi ya msimu huu. Udhamini nao umekuwa mzuri kwasasa”.
Ligi kuu ya Tanzania bara pazia lake limefungwa jana kwa Azam fc kutwaa ubingwaa baada ya kufikisha pointi 62.
Mbali na kutwaa ubingwa huo, Azam fc haijawahi kufungwa mchezo wowote msimu huu.
Yanga wameambulia nafasi ya pili kwa pointi zao 56, huku Mbeya City wakiwa wa tatu kwa pointi 49.
Wekundu wa Msimbazi Simba wamemaliza na pointi 38 katika nafasi ya nne.
JKT
Oljoro, Rhino Rangers na Ashanti United zimeshuka daraja na kuzipisha
timu za Ndanda fc ya Mtwara, Stand United ya Shinyanga na Polisi
Morogoro ya mkoani Morogoro.
0 comments:
Post a Comment