Na Baraka Mbolembole
Majuzi nilizungumza na mchezaji mmoja wa timu ya Yanga SC. Ni rafiki yangu wa miaka mingi sana toka tukiwa mkoani tukicheza soka pamoja.
Tulikuwa tunazungumzia kuhusu kiwango chake cha sasa, na nilimwambia amekuwa bora na si rahisi kwake kurudi katika benchi.
Kama ilivyo wachezaji wengine wengi, naye alishukuru ila akaniambia ' Nimeshika kwa muda nafasi ya Mtu'.Nilipingana naye kuhusu hilo nikamwambia 'Huu ni wakati wako, utakuwa mchezaji wa kutegemewa wa timu ya Taifa si muda kuanzia sasa'.
Namfahamu vizuri! Ni mchezaji mwenye nidhamu ndani na nje ya uwanja. Anaupenda mpira. Mpambanaji. Mtu jasiri, na mchezaji mwenye maarifa mengi ndani ya uwanja.
Nilimkumbusha kila kitu, tangu akianza kucheza ligi kuu na kufunga mabao nane katika msimu wake wa kwanza akicheza kama mlinzi wa kulia katika timu iliyo daraja la chini kwa sasa. Nikwambia, ' Wewe jiamini tu, nafikiri umeandaliwa kuwa mrithi wake.
Sasa timu zinafungwa katika kusaini wachezaji wengi kutoka nje ya nchi, hivyo watahitaji kuona wachezaji wazawa kama wewe ambao tayari mmekomaa mnabaki kuwa msingi wa timu.
Ndiyo wakati fulani wachezaji wazawa wanaona hawana nafasi ya
kupambana na kushinda vita ya kuwania namba dhidi ya wachezaji kutoka nje ambao usajiliwa na kulipwa pesa nyingi kuliko wao. Lakini bado tumeweza kuona kocha wa Yanga, Hans alipanga wachezaji wazawa nane kati ya 11 katika kikosi kilichoanza mechezo dhidi ya Azam, Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu, na Hamis Kizza walikuwa wachezaji pekee kutoka nje na wote walianza katika safu ya mashambulizi.
Je, kukosekana kwa Mbuyu Twite kulikuwa tatizo kwa Yanga?. Mbuyu ana uwezo wake!, ni mchezaji mzuri kutoka nje ya nchi ambaye timu yake inajivunia kuwa naye. Lakini bado tunaona mbadala wake akimudu jukumu la beki namba mbili. Ni hivyo hivyo kwa Haruna Niyonzima.
Ni kiungo wa aina yake ambaye anaweza kuleta tofauti ya mchezo muda wowote kutokana na uwezo wake wa kupiga mashuti ' on target', pasi za mwisho, mmiliki wa eneo la katikati ya uwanja. Yanga walimmiss sana Niyonzima katika mchezo dhidi ya Azam, na Mnyarwanda huyo ndiye aliyeleta tofauti katika mechi baina ya timu hizo msimu uliopita kwa kufunga bao kali la umbali akiwa katika 'pembe ya uwanja'.
Lakini kuanzia mchezo wa marejeano dhidi ya Al Ahly, Yanga wameona wanaweza kusonga mbele bila Haruna. Wachezaji mbada wamekuwa wakicheza kwa kujituma, ila wamekosa matokeo katika siku za karibuni.
Mazungumzo yangu na mchezaji huyo ndiyo yaliyonifanya niandike makala hii. Kwani wakati nikimweleza umuhimu wake na nafasi anayocheza kwa sasa ni lazima atatesa. Akanishtua kwa kuniambia jambo ambalo linabeba kichwa cha habari cha hoja yangu ya leo.
MISHAHARA NA UWAJIBIKAJI NI TATIZO KWA YANGA?, Imekaa katika muundo wa swali kwa kuwa ni hoja inayofungua milango kwa mtu mwingine kutoa mawazo yake. Pamoja na umuhimu wote ambao amekuwa akionesha katika kikosi, bado mchezaji huyo aliniambia.
Hawa jamaa ( Yanga) hawaeleweki' ni kamuuliza kwa nini anasema hivyo. ' Unajua sisi wanatuona watoto. Tunafanya kazi kubwa uwanjani lakini wenzetu ndiyo wamekuwa wakilipwa pesa nyingi'
Nikamwambia, hapana! Hiyo siyo sababu ya kumfanya alalamike. Yeye aendelee kufanya kazi yake vizuri uwanjani kama anavyofanya sasa, mwisho kiwango chake ndicho kinapandisha thamani ya malipo yake.
Nikamwambia kila mchezaji nyota duniani alianza kulipwa '
kidogokidogo' na viwango vyao ndiyo vilipandisha thamani yao.
Akaniambia, ' Sawa, lakini huu ni wakati ambao na mimi natakiwa kuvuna kinachonikidhi. Nina familia, na watu wanaonitazama. Mimi siyo mtoto tena'
Nilipojaribu kumdadisi kama kuna tatizo lolote kati yake na timu,
akaniambia hakuna.nafikiri mchezaji huyu anatakiwa kusikilizwa kwa umakini mkubwa na viongozi wa Yanga. Kwa nafasi yake itawachukua muda kumpata mchezaji kama yeye, bado ni kijana na tayari yupo hapo kwa msimu wa tatu sasa.
Kama walianzisha kikosi cha wachezaji nane katika mchezo muhimu dhidi ya Azam, huku kundi kubwa la wazawa hao wakiwa ni vijana, kumsaini tena Omega Seme kwa dau la millioni 20, hiyo ni ishara kuwa ' Yanga yenye sura ya Kitanzania zaidi itaonekana msimu ujao' lakini inakuwaje kushindwa kumsaini mchezaji wa nafasi muhimu kama mlinzi wa pembeni kwa sababu za mshahara?
'Mkataba wangu unamalizika mara baada ya msimu huu kufika mwisho. Nimewambia wanipandishie malipo lakini wamekuwa wazito, ni kama hawapo tayari kwa jambo hilo.' Hapana pia pana pointi zake pia. Mkataba unapokwisha inatakiwa kutazamwa mchango na uwajibikaji wa muhusika.
Kama alikidhi viwango, anatakiwa kupewa mkataba ulio bora zaidi, kama anahitajika katika malengo yajayo ya klabu ni muhimu kumuhifadhi mchezaji huyo. Yanga wamesaini wachezaji wengi kutoka ng'ambo na wanalipwa vizuri lakini kilio cha mchezaji huyu kinamaanisha kuwa kuna kundi la wachezaji wengi wanaocheza mara kwa mara linalipwa kiwango
cha chini cha mishahara. Kuna tofauti kubwa katika mishahara ya
wachezaji kama Okwi, Mbuyu, Haruna, Kiiza na Kavumbagu na wachezaji wazawa.
Lakini unapofika wakati wazawa hao wanapoomba walau ongezeko kidogo ya mishahara hufungiwa vioo, wale ambao bila kucheza Yanga hawawezi kuwa wachezaji wazuri, wamekuwa wakisaini mikataba mipya kwa mishahara 'kiduchu'.
Ndiyo kuna wakati bora kuchukua kilichopo kuliko kukosa
kabisa. Ila, mbeleni inaweza kuwa tatizo kwa klabu endapo wazawa hao
watajikuta wapo wengi. Je, ni kiasi gani mchezaji huyo anahitaji ili
kubaki Yanga na kusaini mkataba mpya?
Sikumuuliza kiwango halisi anachotaka ila nilimuomba aniambie kwa makadirio ni kiasi gani anataka walau Yanga wafikie kama mshahara wake, Mil. 1.5, itatosha. Huu si wakati wa kucheza soka kwa mapenzi.
Mimi nimesimamia hilo la nyongeza yangu ya mshahara, nitasaini
wakifikia lakini ni kama hawataki. Nitaondoka msimu ukimalizika endapo watashindwa kufikia mshahara huo, Tunajituma sana, ila wapo wachezaji wengine wanalipwa zaidi japo hawana mchango mkubwa.
Yanga imeporomoko kutoka nafasi ya kwanza hadi ya pili katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara.
Wapo nyuma kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya Azam Fc, na watacheza na JKT Ruvu siku ya jumapili hii katika uwanja wa Taifa. Wakati, Azam watakuwa ugenini kucheza na Ruvu Shooting, mjini Mlandizi.
Je tofauti kubwa ya mishahara ni tatizo kwa Yanga wakati huu hasa wachezaji wakitoa malalamiko kuwa kuna upendeleo fulani unaofanywa na viongozi kwa baadhi ya wachezaji?., Wachezaji nafikiri wanapopandisha viwango vyao wanatakiwa kulipwa vizuri. Ndivyo inavyotokea hata katika dunia ya kina Wayne Rooney, Cristiano Ronaldo, Leonel Messi, mikataba mpya inakwenda na thamamini ya mchango wa mchezaji katika mkataba uliopita.
Mchezaji huyu asikilizwe Yanga.
0 comments:
Post a Comment