Vurugu kubwa zimetokea mkoani Mbeya baina ya Jeshi la Polisi na waendesha bodaboda(pikipiki) baada ya jeshi la polisi kutaka kuzima jaribio la kutaka kuvunja nyumba.
Boda boda hao walifunga barabara na kuzua taflani baina yao na jeshi la Polisi baada ya Jeshi hilo kuingilia kati kumuokoa Mke wa dereva wa pikipiki baada ya madereva hao kuvamia nyumba yake maeneo ya Forest wakitaka kubomoa wakimtuhumu kuhusika na kifo cha mumewe.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa nne asubuhi baada ya waendesha bodaboda kutaka kumdhuru mwanamke huyo wakimtuhumu kumuua dereva mwenzao ndipo jeshi la polisi lilipoingilia kati hivyo kusababisha vurugu kubwa baina ya madereva hao na jeshi la polisi.
Hata hivyo madereva wa pikipiki zaidi ya 20 walilivamia gari la Polisi na kuvunja kioo cha mbele hali iliyopelekea dereva wa gari hilo kulikimbiza hadi kituo cha Polisi cha Kati ili kuomba msaada kwa askari wenzie waliojitokeza wakiwa na silaha za moto na kuwatawanya kabla ya kufunga barabara na kuanzisha vurugu.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha bodaboda Jiji la Mbeya, Vicent Mwashoma, amelaani kitendo hicho na kuongeza kuwa jeshi la polisi limetumia nguvu kubwa kupambana na madereva wa bodaboda ili hali kuna uongozi unaotambuliwa na kusimamiwa na baadhi ya Askari.
Akizungumzia chanzo cha vurugu hizo, mwenyekiti huyo amesema juzi aliuawa dereva mwenzao aliyemtaja kwa jina la Siza Mwambenja ambapo baada ya kuzika madereva hao walianza kufanya upelelezi na kupewa taarifa kuwa aliyehusika ni mkewe aliyeachana naye kwa kusuka njama na wauaji.
Amesema baada ya kupata taarifa hiyo walienda nyumbani kwake kwa lengo la kumkamata hali iliyosababisha jeshi la polisi kufika na kuwatawanya lakini jazba ziliwapanda madereva hao baada ya baadhi ya maaskari kuanza kuvunja pikipiki na kuwapiga.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi baada ya marehemu kuachana na mke wake huyo anayetuhumiwa kusuka njama za mauaji na kuoa mke mwingine hali iliyosababisha mwanamke huyo kupata wivu na kulazimika kufanya mipango ya mauaji hayo.
Wakati vurugu hizo zikiendelea Shule ya sekondari ya Forest ya Jiji la Mbeya ililazimika kuahirisha mitihani ya kufungia mhula kutokana na wanafunzi kuathirika na mabomu yaliyokuwa yakirushwa na jeshi la polisi.
Hata hivyo kufuatia vurugu hizo waendesha boda boda kadhaa wanashikiliwa na jeshi la polisi akiwemo Katibu wa chama hicho kwa kuhusika na uvunjaji wa Sheria na uharibifu wa miundombinu ya barabara na gari la Polisi.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment