HAMUELEWEKI tatizo. Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic haelewi
lolote kuhusu mkataba wake mpya utakaomuwezesha kuendelea kuifundisha
klabu hiyo, ameamua kuondoka zake kwenda Kenya kisha Ghana alikoitwa na
rafiki zake.
Wiki chache zilizopita Logarusic raia wa Croatia,
alizungumza na Mwanaspoti akilalamikia kitendo cha Simba kumpiga
danadana kuhusu mkataba mpya hadi wiki iliyopita kupewa sharti la
kuifunga Yanga katika mchezo wa juzi Jumamosi ili apewe mkataba
mwingine.
Mkataba wa sasa wa kocha huyo unaisha mwezi ujao,
lakini ni kama umeisha kwani Simba haina michuano yoyote itakayoshiriki
ndani ya siku zilizobaki hadi kocha huyo atakapomaliza siku zake za
kuitumikia timu hiyo.
Jana Jumapili, Logarusic alisema hajui lolote juu
ya hatma yake ndani ya timu hiyo na akaenda mbali kwa kusema amebakiza
siku tano za kubaki nchini na kujua kama ataendelea kuinoa timu yake au
vinginevyo.
Logarusic ambaye katika mechi ya juzi almanusura
mbinu zake ziwalaze mapema mashabiki wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu
Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1, alisema hakuna kiongozi
yeyote wa Simba aliyemfuata kuzungumza naye kuhusu mkataba mpya.
Alisema ndani ya siku chache zijazo ataondoka
kuelekea Kenya na Ghana kuwatembelea rafiki zake, lakini zikitimia siku
tano yaani Ijumaa ya wiki hii atakuwa amejua Simba haina mpango naye na
atajiunga na timu nyingine itakayomuhitaji ndani na nje ya Tanzania.
“Nitakuwepo Tanzania hadi Jumatano au Alhamisi
mapema, baada ya hapo nitaenda Kenya halafu Ghana ambako rafiki zangu
wameniita, ikifika siku ya tano ambayo ni Ijumaa bila ya Simba kuniambia
lolote nitajua mimi na wao hatuna kitu cha kuendelea kutufanya tuwe
pamoja.
“Silazimishi Simba wanipe mkataba lakini sitaki
kuonekana nina tamaa ya fedha kwa kwenda timu nyingine bila ya wao
kuniambia kitu, mimi sasa ni kama kocha huru ninayeweza kujiunga na timu
yoyote.
“Kuhusu kitakachotokea nikiwa Kenya au Ghana
siwezi kukuthibitishia lakini mimi kama kocha ajira yangu ni soka,
nikipata timu siwezi kukataa maana ndiyo maisha yangu,” alisema
Logarusic.
Ukweli wa mambo
Mwanaspoti lina uhakika kuwa, Logarusic anaenda
Kenya kufanya mazungumzo na klabu za Gor Mahia na AFC Leopards ambazo
zilionyesha nia ya kumsajili ili aweze kuifundisha mojawapo ya timu hizo
zinazoshiriki Ligi Kuu Kenya.
Kama mambo hayataenda vizuri na moja kati ya klabu
hizo za Kenya, Logarusic ataenda Ghana kufanya mazungumzo na klabu ya
Accra Hearts of Oak inayotafuta kocha kwa nguvu zote.
Ashindwa kufanya usajili
Kutokana na kutofahamu hatma yake, Logarusic
amesema anashindwa kufanya jambo lolote kuhusu usajili japokuwa
anamalizia ripoti ya kazi zake ndani ya mzunguko wa pili wa ligi.
“Hapa namalizia ripoti yangu ili niwakabidhi kabla
ya kuondoka, siwezi kujishughulisha na usajili wakati sijui hatma
yangu. Wanaweza kuniuliza nafanya mambo ya usajili mimi kama nani?
Sishughulikii usajili hata kidogo,” alisema Logarusic.
Kauli ya Simba
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema
uongozi unafahamu kama Logarusic anapaswa kuongezewa mkataba wake lakini
kuna mambo wanayoshughulikia ili waweze kumpa mkataba kocha huyo.
“Nakuhakikishia bado tunamuhitaji Logarusic kuliko
anavyotuhitaji, isipokuwa kuna mambo tunayashughulikia na kabla ya
Ijumaa (ya wiki hii) tutakuwa tumefikia sehemu nzuri sisi na yeye,”
alisema Kamwaga.
Logarusic alijiunga na Simba Desemba Mosi mwaka
jana na alisaini mkataba wa miezi sita na kuiwezesha Simba kushika
nafasi ya nne katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha
pointi 38 baada ya kucheza mechi 26. Kocha huyo ameiongoza Simba katika
mechi 13 za Ligi Kuu.
CHANZO: MWANASPOTI
CHANZO: MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment