
MAJOGOO
wa Jiji, Liverpool wanazidi kujipa matumaini ya kubeba kombe kwa mara
ya kwanza baada ya miaka 24 kupita kufuatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi
ya Nowrich katika mchezo wa ligi kuu soka nchini England alasiri hii.
Kwa ushindi huo Liverpool wanafikisha pointi 80 kileleni kwa kucheza mechi 35 na sasa mnuso wa ubingwa kuanza kunukia Anfield.
Wapinzani
wao Chelsea wamebakia nafasi ya pili kwa pointi 75 baada ya kucheza
mechi 35 na jana walipigwa vidude viwili kwa Moja na paka weusi, klabu
ya Sunderland.
Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa na mwamuzi Andre
Marriner , mashabiki wa Liverpool waliosafiri na timu yao wameshangilia
sana kutokana na matokeo hayo kuwa na msaada mkubwa kwao katika
harakati za kutwaa ubingwa.
Liverpool walianza mchezo kwa kasi nzuri na dakika ya nne tu, Raheem Sterling aliandika bao la kwanza.
Dakika ya 11, Luis Suarez alifunga bao la pili, lakini Nowrich walisawazisha bao la kwanza dakika ya 54 kupitia kwa Gary Hooper.
Liverpool
wakiwa katika morali ya kusaka ushindi, Raheem Sterling katika dakika
ya 62 aliwainua vitini mashabiki baada ya kufunga bao la tatu.
Nowrich waliokuwa nyumbani leo walijitahidi kutafuta mabao ya kusawazisha na katika dakika ya 77 , Robert Snodgrass aliisawazishia bao la pili.
Hadi dakika 90 zinamalizika Liverpool walikuwa mbele kwa mabao 3-2.
Matokoe ya leo ni faraja kubwa kwa kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers pamoja na nahodha wake Steven Gerrard.
Rodgers ana hamu ya kuandika historia ya kuwapa ubingwa majogoo wa jiji baada ya ukame wa maika 24.
Mpinzani mkubwa wa Rodgers katika
mbio za ubingwa ni Jose Mourinho, lakini kufungwa kwa Chelsea jana na
Liverpool kushinda mechi ya leo kumetengeneza pengo la pointi kuwa 5,
huku timu zote zikicheza mechi 35.
Chelsea na Liverpool zote zimebakiza mechi tatu ili kufunga msimu huu.
Chelsea ikishinda mechi zote itafikisha pointi 84, wakati Liverpool watafikisha pointi 92 kama watashinda mechi zote.
Endapo Liverpool watashinda mechi moja na sare 2 basi watafikisha pointi 85 ambazo haziweza kufikiwa na Chelsea.
Lakini
tahadhari kwa Rodgers ni Manchester City kwasababu wamebakiwa na mechi 5
mpaka sasa, huku wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi 71.
Kama
watashinda mechi zote tano wataweza kufikisha pointi 86 na kwa maana
hiyo watavuka pointi za Liverpool kama watashinda mechi moja na sare
mbili.
Matokeo
ya kushinda mechi moja na sare mbili yatamfanya Rodgers amshinde
Mourinho tu, lakini Manuel Pellegrini na Man City yake wanaweza
kuwaletea shida endapo watashinda mechi zote.
Ili
kujihakikishia ubingwa , Liverpool wanatakiwa kushinda mechi mbili na
kutoa sare moja ili wasiweze kufikiwa na timu yoyote kwa pointi zao 87.
Man City kesho wanaingia uwanjani kukabiliana na West Brom katika uwanja wao wa nyumbani wa Etihad.
Hii ni mechi muhimu kwa Pellegrini kwani kufungwa au kutoa sare kutazidi kumshusha katika mbio za kuwania ubingwa.
0 comments:
Post a Comment