Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
PAZIA la ligi kuu soka Tanzania bara
msimu wa 2013/2014 linafungwa kesho aprili 19 kwa timu zote 14 kushuka uwanjani
katika miji tofauti nchini.
Ligi inamalizika kesho wakati timu tatu
zimeshajihakikishia nafasi tatu za juu.
Azam fc wametwaa ubingwa baada ya
kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote.
Yanga wamechukua nafasi ya pili wakiwa na
pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote chini yake.
Mbeya City nao wameshika nafasi ya tatu
kwa pointi 46 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ya chini yake.
Simba sc wao wao wapo mbioni kuisaka
nafasi ya nne kwa pointi zao 37 baada ya kucheza mechi 25.
Nafasi ya tano wapo Kagera Sugar wenye
pointi 35, na endapo Simba watafungwa kesho na wao wakashinda, basi Mnyama
anaweza kumaliza ligi katika nafasi ya tano.
Katika mechi zote 7 hapo kesho, mechi
tatu pekee zina hamasa kubwa kwa mashabiki wa soka nchini.
Mechi ya kwanza iliyovuta hisia za
mashabiki wa soka ni ile ya Yanga dhidi ya Simba sc ndani ya uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Timu hizi zitakutana zikiwa na
mafanikio tofauti msimu huu ambapo Yanga wameambulia nafasi ya pili, huku
Mnyama akijikongoja katika nafasi ya nne.
Simba na Yanga zinakutana jumamosi,
huku Yanga wakiwazidi wenzao kwa mafanikio msimu huu.
Yanga wamecheza mechi 25 sawa na Simba
sc, lakini wameweza kushinda mechi 16, kutoa sare 7 na kufungwa mechi 2 tu,
hivyo kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili.
Pia Yanga ndio klabu iliyofunga mabao
mengi zaidi mpaka sasa ambapo imetikisa nyavu za timu pinzani mara 60, lakini
wamefungwa mabao 18 na kuwa timu ya pili kufungwa mabao machache.
Mabingwa watetezi Azam fc wamefunga
mabao 50 na kufungwa mabao 15 tu, hivyo kuwa timu yenye rekodi ya kufungwa
mabao machache zaidi msimu huu.
Ukirejea kwa upande wa Simba sc, msimu
huu upepo mbaya umevuma kwa upande wao kwasababu mpaka sasa wamecheza mechi 25
na kushinda mechi 9, sare 10 na kufungwa mechi 6.
Pia Mnyama Simba amefanikiwa kufunga
mabao 40 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 26, huku wakiiwinda nafasi
ya nne.
Mechi ya kesho haina jipya zaidi ya
klabu hizo kulinda heshima tu.
Hata Yanga wakishinda hawana uwezo wa
kusogea juu, labda Simba wanaweza kujihakikishia nafasi ya nne msimu huu endapo
wataibuka na ushindi.
Mechi ya watani huwa inavuta hisia za mashabiki
wengi wa soka, hivyo tusubiri kuona nani ataibuka kidedea.
Mechi ya pili yenye mvuto ni ile ya
Ashanti United dhidi ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani
Morogoro.
Timu hizi zitapambana ili kupata timu
moja itakayoshuka daraja msimu huu.
Timu zote zina pointi 25 baada ya
kucheza mechi 25, lakini Prisons wanawazidi wenzao kwa wastani mzuri wa mabao
ya kufunga na kufungwa.
Matokeo mazuri kwa Ashanti ni ushindi
tu, kwasababu wakifungwa au kutoa sare watakuwa wameungana na JKT Oljoro na
Rhino kushuka daraja.
Sare kwa Prisons au ushindi itakuwa
faida kwao na wataendelea kudunda ligi kuu msimu ujao.
Hii ni mechi tamu mno kwasababu makocha
wa klabu hizi, Abdallal Kibadeni ( Ashanti) na David Mwamwaja (Prisons) wataingia
uwanjani wakiwa na malengo sawa.
Wote walipewa timu mzunguko huu wa pili
ili kuzinusuru zisishuke daraja, lakini siku ya mwisho wanakutana pamoja.
Kibadeni ndiye mwenye shughuli pevu
kwasababu yeye anahitaji ushindi tu, wakati mwenzake anahitaji hata sare.
Mechi ya tatu kwa mvuto ni baina ya
mabingwa Azam fc dhidi ya JKT Ruvu ndani ya uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Hii haina presha yoyote, lakini uzuri
wake unatokana na uhitaji wa matokeo kwa Azam fc ili wabebe `ndoo` ya ligi kuu
bila kufungwa timu yoyote.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog
alisema anahitaji kuchukua ubingwa kwa kushinda mechi zote, hivyo aliwataka
wachezaji wake kucheza kwa makini dhidi ya JKT Ruvu hapo kesho.
Mechi nyingine za kesho ni baina ya
Wagonga Nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc dhidi ya Mgambo JKT kwenye uwanja wa
Kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya.
Vibonde wa ligi hiyo walioshuka daraja,
Maafande wa Rhino Rangers watawakaribisha Ruvu Shooting katika uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Timu nyingine iliyoshuka daraja, JKT
Oljoro itakuwa mwenyeji wa mabingwa wa zamani wa Tanzania , mwaka 1999 na 2000,
Mtibwa Sugar katika uwanja wa Shk. Amri Abeid Kaluta, jijini Arusha.
Wagosi wa kaya, Coastal Union watakuwa
wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
0 comments:
Post a Comment