Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA msaidizi wa Yanga Sc, Charles Boniface
Mkwasa `Master` amewashauri mashabiki wa
soka nchini kuzipenda timu zao kwa wakati wote na kuepuka tabia ya kuwabebesha
lawama wachezaji, mabenchi ya ufundi na viongozi yanapotokea makosa.
Mkwasa ameuambia mtandao huu kuwa tatizo la
wapenzi wengi wa soka Tanzania hawana uvumilivu hususani timu inapofanya vibaya
tofauti matarajio yao.
“kwa mfano unakuta timu imefungwa, wachezaji wanaenda
kwa mashabiki wao ili wawasalimia, halafu ukashangaa wanarushiwa chupa za maji
tofauti na wenzetu Ulaya”.
“Najua hatuwezi kufananisha kwetu na ulaya, lakini
kuna makosa ya kawaida yanatokea uwanjani mfano kukosa penati”.
“Hivi ni vitu vya kawaida tu, lakini ikitokea
hivyo wachezaji wanapata lawama nyingi”. Alisema Mkwasa.
Mkwasa aliongeza kuwa mazingira kama haya
yanamfanya mchezaji ashindwe kujiamini anapocheza mpira.
“Baadhi ya wachezaji wakizomewa wanashindwa
kujiamini kabisa, sasa hii inamfanya ashindwe kufanikisha malengo yake”.
“Tatioz ni watu kutokuwa na mapenzi ya kimpira
kama wenzetu Ulaya”.
“Kwa nchi nyingi za kiafrika tatizo la mashabiki
kukosa mapenzi ya dhati na timu zao lipo kwa kiasi kikubwa”.
“Wachezaji wanashangiliwa wanapofanya vizuri tu,
lakini wakifanya makosa ni dhambi kubwa”. Alisema Mkwasa.
Kocha huyo aliwashauri vijana kuzidisha umakini
katika kazi yao ili kuendana na mazingira ya kitanzania kwasababu kubadilika
kunahitaji muda.
Mkwasa alifafanua kuwa kama vijana wanataka
kushangiliwa, basi wafanye vizuri na kujituma zaidi uwanjani.
“Tatizo kubwa la wachezaji ni kukosa msingi ya
mwanzo ya mpira na malengo.”.
“Unakuta mchezaji fulani ni mzuri lakini ameibukia
wapi huelewi”.
“Nadhani ipo haja ya kuwaelemisha vijana kama
hawa. Kama hawana misingi ya mpira toka utotoni, lazima wakubali kushaurika na
kuzingatia mafunzo ya walimu wao”.
“Wakiwa watulivu katika mafunzo ya makocha wao
wataepuka kuzomewa na mashabiki wao”. Alisema Mkwasa.
Aidha kocha huyo aliwataka wachezaji kutumia muda
wao katika mazoezi wakati huu wa likizo ndefu kwasababu mpira uchawi wake ni
bidii ya mazoezi.
“Najua wapo likizo kwasasa. Hatuwezi kuwazuia
kufanya starehe kwasababu walijinyima walipokuwa kazini”
“Cha msingi kwao ni kutambua kuwa starehe ni adui
mkubwa wa mpira. Lazima mchezaji ajipe muda wa mazoezi ili kulinda kiwango
chake”.
“Wajitambue na wawe makini wakati huu ili wakirudi
uwanjani wasianze upya na kuwapa shida makocha wao”. Alishauri Mkwasa.
0 comments:
Post a Comment