Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mkuu wa Wagosi wa kaya, Coastal Union,
Mkenya, Yusuf Chipo amesema mpira wa miguu ni mchezo wa ajabu kwasababu mwalimu
anaweza kuwa na wachezaji wazuri, wanaolipwa vizuri na wanaishi mazingira
mazuri, lakini timu ikazidi kufanya vibaya.
Akihojiana na mtandao huu kwa njia ya simu kutoka
kwao nchini Kenya alipo kwa mapumziko, Chipo amesema Coastal ina wachezaji
wazuri, lakini kuna tatizo la kutojituma kwa wachezaji.
“Unajua Kenya wachezaji wanajituma sana na
kuisaidia timu tofauti na Tanzania”
“Pia kwa Kenya waamuzi wana viwango vuzuri zaidi,
unapokuja kwa Tanzania marefa wanaboronga sana hasa kwenye mechi muhimu”
“ Nimekuwepo katika ligi ya Vodacom, lakini huwa
nashangaa kwanini wachezaji wanakuwa wazembe kwa kiasi kikubwa”.
Aidha, Chipo amekiri kuwa Tanzania ina vipaji
vingi vya soka kuliko Kenya, lakini kinachokosekana ni malengo kwa wachezaji na
maandalizi kwa ujumla.
“Kila mchezaji anayempata anajua mpira. Ukienda
Mbeya unawapa wachezaji wazuri, ukienda Kagera kuna wachezaji wazuri”.
“Kinachoonekana kwa wachezaji ni kushindwa
kujitambua kuwa mpira ni ajira. Pia wanakosa mazoezi ya kiufundi na kuwajenga
katika saikolojia ya kuutumikia mpira”. Alisema Chipo.
Akiizungumzia klabu yake ya Coastal Union, Chipo
amesema kufanya vibaya kwa klabu hiyo ni yeye kutohusika katika usajili wa
wachezaji.
Chipo alisema wachezaji waliosajili Coastal
walikuwa katika mipango ya kocha aliyepita kwasababu kila mwalimu ana mfumo
wake na matarajio yake.
“Mimi nilikuja na kupewa wachezaji ambao
nilitakiwa kupambana kulingana na vipawa vyao. Pili ndani ya klabu tuna
matatioz yetu ambayo yanaathiri wachezaji”.
“Tukizungumzia ligi ijayo, mimi nina fursa.
Nitatafuta wachezaji wawili watatu kulingana na falsafa yangu na maono yangu”.
“Mimi napenda sana kupiga mipira mirefu, hivyo
nahitaji washambuliaji warefu. Nitawatafuta na nitafanikiwa msimu ujao”.
Alisema Chipo.
Hata hivyo, Chipo aliwashauri makocha wa Tanzania
kuwa na msimamo mkali na kuzingatia falsafa zao.
“Kila mwalimu ana mfumo wake wa ufundishaji”
“ Linapokuja suala la viongozi wa klabu kuwa na
matakwa yao tofauti na falsafa ya mwalimu, hapo ndipo utajua yupi mwalimu
bora”.
“Kitu cha msingi ni kutambua kuwa ukocha ni
taaluma, kuna miiko ya mpira tunayojifunza sisi kama walimu”.
“ Ni wajibu wetu kuwa na msimamo na kuepuka
kushinikizwa kufanya mambo kinyume na falsafa zetu”. Alisema Chipo.
0 comments:
Post a Comment