Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mkongwe na mchezaji machachari wa zamani wa
Simba na timu ya taifa ya Tanzania na sasa Ashanti United, Abdallah King
Kibadeni `King Mputa` amesema kwa uzoefu wake anafahamu kuwa vijana wengi
wanashindwa kujitambua na kujitathimini.
Akihojiana na mtandao huu, Kibadeni amefafanua
kuwa wapo vijana katika Nyanja mbalimbali za michezo na burudani mfano bongo
fleva, filamu, mpira na vinginevyo, lakini kwa wachezaji wa soka kujitambua
imekuwa shida sana.
“Ukiangalia
vijana wanaofanya Bongo fleva , siasa, wengi wao wanatambua kuwa muziki na
siasa ni kazi yao na wanaweza kupata maisha mazuri kwa kazi hizo”.
“Ukija kwa vijana wetu wa mpira, huwa wanaridhika
mapema na wanacheza kwa sifa”.
“Akicheza kwa mafanikio na wakamsifia basi inakua
shida kwa walimu”.
“Unapomchukua na kumuweka kambini ili umtulize,
bado anashindwa kujitambua. Kambini kuna uwanja, walimu na kila kitu, lakini
hata kuamka inakuwa shida”.
“Wanataka mwalimu awasimamie, awasukume, sasa
unaanzaje kusema wachezaji hawa wanajitambua”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliwaomba walimu wenzake kuwaelemisha vijana
kwasababu wanachukua nafasi ya wazazi.
“Tanzania tuko milioni ngapi? Kijana anapochaguliwa
miongoni mwa watanzania wengi wanaocheza soka lazima aheshimu jambo hilo”.
“Leo hii timu ya taifa inakuwa na wachezaji 30,
hivi kuna watu wangapi wanaocheza mpira Tanzania?, hawa vijana lazima waelimishwe
ili wajitambue na kutathimini malengo yao”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliongeza kuwa vijana lazima watambue
kuwa makocha wao ni wazazi hivyo ni haki yao kuuliza wanakula nini, wanalala
wapi na wanatumiaje pesa zao.
“Kijana ukimfuatilia na fedha zake anaona kama
unamuonea. Kocha ni mzazi na lazima ajue unachokipata anafanyia nini kwa maisha
ya baadaye”.
“Hatuna malengo ya kuwabana na hela zao, lakini ni
muhimu kuwaeleza ukweli kuwa wanachokipa leo kinaweza kisipatikane kesho”.
“Mpira una muda wake, leo utaonekana mzuri kesho
utaoekana hufai. Lazima ujitambue na
kujua utaishi vipi baadaye. Sasa kwa kuzingatie hili, kwanini makocha
tusikufuatilie?” Alihoji Kibadeni.
“Lazima
wajipangia malengo yao. Lazima wajue wanataka kucheza kwa muda gani na baada ya
hapo wawe nani?, wanataka kuwa mameneja, makocha au viongozi”.
“Vijana wasipokuwa na malengo watajikuta wanacheza
kwa mwaka mmoja halafu wanapotea kabisa”.
“Wawe na nidhamu na wajijue wanacheza kwa ajili ya
nani, kwa ajili ya nchi au klabu”.
“Lazima tuwe na wivu, kwani tumekatazwa kuwa wachezaji
bora wa dunia au Afrika?”.
“kwanini watu bora waonekana wanatoka magharibi?,
lazima vijana wetu wawe wapambanaji na kuwa na malengo ya mbali”. Alihitimisha
Kibadeni.
0 comments:
Post a Comment