Sunday, April 20, 2014

kavumbagu3
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
HISTORIA ya soka inaonesha kuwa nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) zamani Zaire, ilikuwa ya kwanza kutoka kusini mwa jangwa la sahara kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 1974.
Congo wakiwa katika kiwango cha juu barani Africa na kutwaa ubingwa wa kombe la Mataifa ya Africa mwaka huo wa 1974 walipata nafasi ya kushiriki kombe la dunia, lakini waliishia kuacha rekodi ambayo haijavunjwa mpaka leo.
Nchi hii iliyokuwa inatesa kwa soka kali iliambulia kipigo cha mabao 9-0 dhidi ya Yugoslavia kwenye moja ya mechi zake na kubaki kuwa rekodi ya dunia.
Stori iliyopo hapa ni jinsi Congo walivyofanya maandalizi ya kwenda kushiriki mashindano haya makubwa yanayoandaliwa na FIFA.
Congo walikuwa katika ubora wa juu na walifanya mazoezi ya kujiwinda na fainali hizi, lakini wakakosea njia moja.
Wakati wanacheza fainali za mataifa ya Afrika walikuwa wana imani za kishirikina kwa kiasi kikubwa na walidhani wamefanikiwa kwa kuwatumia waganga waliokuwa nao.
Viongozi, mashabiki na wachezaji wa timu ya Taifa ya Congo walikuwa waumini wazuri wa uchawi, hivyo kila wanapoenda ilikuwa lazima watambike na kubeba wazee wa kamati ya ufundi (wachawi).
Sasa walipopata nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia walifanya maamuzi mazito ya kusafiri na wachache wanaosemeka kuwa 9 ili wakashinde mechi.
Wakiwa katika morali kubwa baada ya kuwasili na wazee wa shughuli, waliingia uwanjani kusakata kabumbu.
Wachawi nao walikuwa wametulia sehemu na matunguli yao wakiendelea kufanya yao.
Ghafla, bao la kwanza likaingia, mara la pili, tatu, nne, tano, sita, saba, nane na msumari wa tisa ukakamilisha idadi ya wachawi waliosafiri na timu.
Kah! Wacongo walishangaa sana na kuchanganyikiwa, huku wachawi wakichukiwa vibaya mno na ikafika wakati watu wakawa wanashinikiza wachawi wale wasipande ndege, warudi kwa sayansi yao.
Uchawi ilikuwa imani ya Wacongo na walijijenga katika mambo hayo.
Walidhani kuzifunga nchi nyingi za kiafrika ni kutokana na waganga wao, na wakasahau kanuni za mpira.
Mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, ili timu moja ifunge goli, lazima wachezaji wa timu nyingine wafanye makosa.
Hakuna bao kama wapinzani wako hawajafanya makosa.
Mambo ya uchawi ni sayansi isiyothibitika kwa macho ya kawaida. Na ndio maana ni ngumu kugungua kuwa mtu huyu ni mchawi.
Lakini mtu unapoenda kwa wataalum hawa na kupatiwa dawa fulani au masharti fulani ya kufanya jambo lolote, halafu akafanikiwa , basi atajenga imani.
Timu inaenda wa Mganga wa jadi na kupewa dawa au wanaambiwa kuwa baadhi ya watu wakalale makaburini, kweli wanaenda na kesho wanashinda mechi, wataachaje kuamini mambo haya.
Wakati nacheza ndondo kwetu, tulikuwa na timu yetu  iliyokuwa moto wa kuotea mbali.
Lakini moja ya kitu nilichokuwa nashangaa ni jinsi wachezaji wenzangu walivyokuwa wanaamini dawa za kienyeji.
Siku ya mechi, wakati tunavaa nahodha wetu alikuwa analeta chumvi ya kawaida ya kuunga kwenye mbogo, halafu anasema kila mtu uchovye kidogo na kuweka kwenye soksi au kujipaka mwilini.
Ukimuuliza kwanini? Anakujibu inazuia dawa za wapinzani wetu. Kweli watu wanafanya na tunashinda mechi.
Lakini kuna siku tulifanya hivyo, na tukala kichapo kitakatifu cha mabao 8-0. Mzee wa chumvi akasema imetokana na baadhi ya wachezaji kugomea zoezi lake nikiwepo mimi.
Hizi ni ndondo tu, lakini mambo haya yanatokoe hata katika michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Zinapokutana Simba na Yanga kama jana basi kunakuwepo na vimbwanga kibao.
Kwa miaka mingi sasa, klabu hizi mbili zimekuwa zikiendekeza imani za kishirikina kila zinapokutana.
Kuna miaka ya nyuma, nilikuwa nasikia njiwa au kunguru wanatua uwanjani na watu wanasema wametumwa na timu fulani kuroga.
Kila wakati habari zao zinasikika na naambiwa kuna viongozi fulani ambao kazi yao ni kurekebisha mambo ya uchawi.
Kamati ya ufundi tunayoijua sie, sio ile ya klabu hizi. Ukisikia kamati hii basi utakutana na wazee wa hatari huko, eti wanasaidia kuroga timu pinzani.
Pazia la ligi kuu soka Tanzania bara limefungwa jana kwa timu zote 14 kushuka uwanjani.
Mechi kubwa jana ilikuwa ni ile ya Simba na Yanga kwenye uwanja wa Taifa.
Hii ilikuwa mechi ya kulinda heshima kwa klabu zote na ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Simba walianza kufunga bao dakika ya 75 kupitia kwa Haruna Chanongo, lakini Yanga wakachomoa dakika ya 86 kupitia kwa Saimon Msuva.
Mambo yote mawili yalitokana na uzembe kwa walinzi wa timu hizi.
Goli linatokana na makosa, kweli mabeki walikosea na wakafungwa.
Mnano dakika ya 55 hivi kipindi cha pili, kulitokea  purukushani uwanjani baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mrundi Didier Kavumbagu kutoa taulo la mlinda mlango wa Simba, Ivo Mapunda alilolitundika golini kwa matumizi yake.
Imekuwa kawaida kwa Ivo kuwa na taulo kubwa golini kwake akilitumia kufuta jasho anapofanya kazi yake.
tauloLakini taulo hili limezua balaa kubwa hapa nchini na hata alipokuwa Gor Mahia ya Kenya.
Mashabiki wengi na viongozi wanaamini Ivo ni mshikirikina na taulo linamsaidia kutofungwa magoli.
Lakini Ivo anafungwa mara nyingi, tena mabao ya kizembe sana, huku akiwa na taulo lake.
Kama kweli taulo ndio kinga ya kutofungwa, mbona anafungwa tu.
Kavumbagu jana aliamini taulo la Ivo linawazuia Yanga kufunga. Sijui alishauriwa akatoe au alifikiria mwenyewe.
Baada ya kutoa taulo hilo alilitupia kwa mashabiki wa Yanga na purukushani zikaanza na  mpira kusimama.
Mwamuzi alimzawadia kadi njano, lakini hebu waza kama angepewa kadi nyekundu ingekuwaje?.
Ingeigharimu timu kwa mambo ya kipuuzi tu na pengine Yanga ingepoteza mechi.
Isitoshe  baada ya tukio hilo, Ivo aliletewa taulo lingine, lakini kuna shabiki mmoja wa Yanga aliingia uwanjani na kuiba na kulirusha kwa wenzake.
Mashabiki wenzake walimshangilia, lakini baadaye alitiwa mbaroni na polisi.
Jamaa aliweza kuingia uwanjani na askari wapo. Kwa wenzetu ni ngumu mno, lakini kibongobongo kawaida sana kwasababu polisi wetu wanajikita kutazama mechi na si kazi yao.
Vituko hivi vyote vilitokana na imani za kishirikina nilizozieleza hapo juu.
Mpira wa miguu ni maandalizi na si kitu kingine. Toka mwanzo Simba walisema watafungwa mechi zote na si mchezo na Yanga.
Kweli msimu umekuwa mbaya kwa Simba, lakini mechi ya watani walijipanga na kwenda kujificha Zanzibar.
Yalikuwa maandalizi makubwa sana ili kuepuka fedheha ya kufungw ana mtani.
Jana wachezaji wa Simba walionesha soka safi na kuwazidi Yanga kwa muda mrefu. Walikuwa na mipango mizuri, lakini kukosa umakini kuliwagharimu.
Watu walioshuhudiwa mechi hii wanasema kama Simba wangekuwa wanacheza mpira kama jana, basi wasingeshika nafasi ya nne.
Walionekana kujipanga kisaikolojia na kwa mazoezi kwani walikuwa fiti sana.
Hii inaonesha kuwa ukijiandaa vizuri unaweza kupata mafanikio.
 Na ndio maana baada ya Kavumbagu kuona golini kwa Simba hakuendeki kirahisi, akahisi taulo la jamaa linafanya mambo.
Kumbe Ivo ameliweka tu kwasababu zake. Mbona sasa walifunga?
Kavumbagu na wenzako, punguzeni imani za kishirikina. Ninyi ni wachezaji wakubwa na vijana wapo nyuma yenu.
Fanyeni mazoezi na jiandaeni vizuri na si kuumiza kichwa kwa mambo yasiyoelewa, halafu kumbukeni mnakula fedha nyingi za klabu.
Tangu Azam fc wanaanza mbio za ubingwa msimu huu, sijabahatika kuona kituko kama cha jana kwao.
Walifanya maandalizi mazuri na kucheza kwa kujituma na ndio maana wamefanikiwa kuwapiga bao kwa kuwapoka ubingwa.
Mambo ya uchawi ni ya zamani sana, siku zote mpira unachezwa hadharani.
Timu yenye mipango uwanjani inashinda na si je ya uwanja.
Mnaupotosha umma wa Watanzania kuwa mpira unategemea  uchawi.
Acheni kuwaaminisha watu kuwa timu yenu inafungwa kwasababu wapinzani wametumia ushirikina.
Fanyeni kazi yenu kwa umakini na juhudi mtafanikiwa. Wacongo wanajua haya vizuri.

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video