Na Boniface Wambura, TFF
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka huu ambapo atafungua
semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka
huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema
Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa
wengine wa saba wa FIFA.
Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika
kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya
kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni
marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao
ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan
Kusini, Tanzania na Uganda.
Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye
alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa
kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira
wa miguu katika ukanda huu.
0 comments:
Post a Comment