Maofisa wa Azam fc wakikagua uwanja wa Sokoine asubuhi hii
Na Baraka Mpenja
DIMBA la
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya lipo katika hali nzuri asubuhi hii kuelekea
mtanange wa kukata na shoka leo jioni baina ya vinara wa ligi kuu soka Tanzania
bara, Azam fc dhidi ya Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc.
Maofisa wa Azam fc wamekagua uwanja huo asubuhi ya
leo na kukubali ubora wake.
Mbeya City wenye rekodi ya kutofungwa nyumbani
kwao wanawakabili Azam fc wanaohitaji pointi tatu tu kujitangazia ubingwa wao
wa kwanza tangu waanze kushiriki ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kuelekea katika mechi hiyo, haya ndio maneno ya
kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi;
"Tunatambua Azam hawajapoteza mechi, lakini
lazima wajue tunahitaji kulinda heshima pia ya kutofungwa kwenye uwanja wetu wa
nyumbani msimu huu. Tutambana hadi dakika ya mwisho ili tushinde mechi
hiyo," .
Azam fc wapo kileleni kwa pointi 56 na kama
watashinda mchezo wa leo watafikisha pointi 59 ambazo hazitaweza kufikiwa na
Yanga hata wakishinda mechi zao mbili walizosaliwa nazo.
Wakimalizana na kipute cha leo, Azam fc watakuwa
wanasubiri mechi ya kufungia msimu dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, jijini Dar es salaam.
Nao Yanga wanashuka dimbani huko Shk. Abeid Jijini
Arusha dhidi ya JKT Oljoro.
Ushindi ni muhimu kwa Yanga kwasababu ili kujipa
matumaini ya kutetea ubingwa wao wanahitaji kushinda mechi zao mbili
zilizosalia.
Kama Yanga watashinda leo watafikisha pointi 55,
wakati wakisubiria nini kitatokea Mbeya.
Endapo Azam
fc watapoteza mechi ya Mbeya na Yanga wakishinda, basi matumaini ya kutetea
ubingwa wao yatakuwepo kutegemeana na matokeo ya mechi ya mwisho ya Azam fc.
Mpaka sasa Yanga wamejikusanyia pointi 52 katika
nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 24.
Mechi nyingine itapigwa katika dimba la Taifa
ambapo Wekundu wa Msimbazi Simba watawakaribisha wauza mitumba wa Ilala,
Ashanti United.
Nayo
Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), huku
Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga .
0 comments:
Post a Comment