Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
MBEYA CITY fc ni klabu ya kwanza kuipatia Azam fc ubingwa
wake wa kwanza tangu ianze kushiriki
michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2008/2009.
Ardhi ya Mbeya imekuwa ya kwanza kwa Azam fc kutwaa ubingwa ndani
yake.
Azam fc imekuwa klabu ya kwanza kuwafunga Mbeya City msimu huu
katika uwanja wao wa nyumbani wa kumbukumbu ya Sokoine.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amekuwa kocha wa kwanza
kuwapatia mafanikio ya ubingwa wa ligi kuu Azam fc.
Rekodi nyingi sana zimewekwa kwa Azam fc msimu huu, lakini yote
hii inatokana na ubingwa huo kuwa wa kwanza kwao.
Msimu wa mwaka huu umekuwa na ushindani mkubwa mno hasa katika nafasi
ya ubingwa.
Klabu mbili kongwe za Simba na Yanga zimekumbana na changamoto
kubwa kutoka kwa Azam fc na Mbeya City katika nafasi nne za juu.
Mpaka sasa kimeeleweka ambapo Yanga pekee wameweza kushika nafasi
ya pili, wakati Simba wakitupwa nafasi ya nne.
Imekuwa kazi ngumu kwa wafalme hawa wa soka la Tanzania kutoka
mwaka 2000 kuachia ubingwa zaidi ya kupokezana kama mbio za vijiti.
Wana TamTam Mtibwa Sugar walibeba `ndoo` mwaka 1999 na 2000, baada
ya hapo Simba na Yanga walikuwa wanatawala, lakini mwaka huu 2014 wamepinduliwa
rasmi kwa Azam fc kutwaa taji.
Cheche zinawaka zaidi kwa Simba kwasababu kwa misimu miwili
mfululizo wanakosa michuano ya kimataifa.
Angalau Yanga mwaka huu walishiriki ligi ya mabingwa na kuonesha
upinzani mkubwa, na mwakani wataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la
shirikisho.
Kwa upande wa Simba imekuwa pigo kwao kwasababu mashabiki wake
walizoea kuona timu yao inawakilisha bendara ya Tanzania kimataifa.
Azam fc wamestahili kutwaa ubingwa kwasababu ya uwekezaji mkubwa
waliouweka katika kikosi chao kuanzia vifaa vya mazoezi na mazingira ya kambi
kwa wachezaji.
Ingekuwa fedhea kwao kukosa ubingwa, kwasababu hawakustahili kushika
nafasi ya pili ambayo wameshaishika sana misimu ya nyuma.
Matokeo mazuri kwao ilikuwa ni ubingwa tu na ndio
maana waliweka mikakati mikubwa ya kufanya vizuri na katika mechi 25
walizocheza hawajapoteza mechi yoyote
Ukirejea kwa Mbeya City fc, hii ni klabu pekee iliyopanda ligi kuu
msimu huu na kuonesha ushindani mkubwa kutoka mwanzo wa ligi mpaka sasa ligi
inaelekea ukiongoni.
Wenzao Ashanti hatima yao imebakia mikononi kwa kocha wa Prisons,
David Mwamwaja mnamo aprili 19 mwaka huu.
Kama watatoa sare mechi hiyo watashuka daraja, na matokoe pekee
yatakayowasaidia ni kushinda tu.
Rhino Rnagers wao wameshashuka daraja mpaka sasa.
Kwa mazingira hayo, Mbeya City imekuwa timu bora zaidi msimu huu
ukiangalia kigezo cha ugeni wa ligi kuu.
Huwezi kuwafananisha Mbeya City na Azam fc, Yanga, Simba, Mtibwa,
Kagera Sugar, Coastal Union kwa kigezo cha ukongwe.
Wao ni wageni sana kwani ndio kwanza msimu wao wa kwanza.
Wachezaji wengi wa Mbeya City ni wageni na hawana majina kabisa
katika soka la Tanzania.
Mpaka sasa wagonga nyundo hawa wa Mbeya wamecheza mechi 25 na
kushinda mechi 12, sare mechi 10 na kufungwa mechi 3. Kwa matokeo hayo
wamefikisha pointi 46 katika nafasi ya nne.
Hata hivyo safu yao ya ushambuliani imeweza kufunga mabao 32, huku
safu ya ulinzi ikiruhusu kufungwa mabao 20.
Yanga waliwafunga Mbeya city bao 1-0 katika uwanja wa Taifa na
kule Mbeya mzunguko wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1 katika dimba la Sokoine.
Coastal Union katika mechi ya mzunguko wa kwanza walitoka sare ya
bao 1-1 dhidi ya Mbeya City uwanja wa sokoine, lakini mechi ya mzunguko wa pili
Mkwakwani, wagosi wakashinda mabao 2-o.
Simba waliambulia pointi moja moja kwa mechi zote mbili ambapo
Mbeya walitoka sare ya 1-1 na Dar es salaam walitoka sare ya 2-2.
Azam fc katika mechi ya kwanza chamazi, walilazimisha sare ya
mabao 3-3 na Mbeya wakashinda 2-1 na kutwaa kombe huko huko.
Kwa mazingira hayo, Yanga, Coastal na Azam fc ni timu pekee
zilizoweza kuifunga Mbeya City.
Nini kimekuwa nyuma ya Mbeya City mpaka wanakuw ana upinzani
mkubwa kiasi hicho?
Baadhi ya sababu ambazo zinawapa nguvu wagonga nyundo hawa wa
Mbeya zaweza kuwa ni;
Mosi; falsafa ya kocha mkuu, Juma Mwambusi na msaidizi wake, Maka
Mwalwisyi.
Makocha hawa wanaamini katika soka la vijana na kuwapa nafasi ya
kucheza kwa mechi yoyote ile.
Mara nyingi Mwambusi anaeleza kuwa mchezaji yoyote unayemuona bora
duniani alipewa nafasi ya kucheza na akafanikiwa kupata uzoefu mkubwa na
kung`ara.
Kwa mantiki hiyo, huwa anawapa vijana wake nafasi na kukwepa
kuonesha kuwa anawategemea wachezaji fulani.
Mwambusi amekuwa akichagua timu yake kwa kuangalia ufiti wa
mchezaji kwa mechi fulani na anaweza kuwabadilisha anavyotaka.
Katika kikosi chake hakuna mchezaji tegemeo, na ndio maana leo hii
unaweza kumuona Mwegane Yeya yuko benchi, lakini Jeremiah Peter yupo
uwanjani na anafanya kazi kubwa.
Ukiona Paul Nonga unaweza kuogoapa kuwa hawatafunga, lakini
unashangaa kumuona Peter Mapunda amevaa jezi ya zambarau na kuonesha soka zuri
mno.
Kwa mzingira haya, wachezaji wanajiamini na kuamini kuwa
watapangwa wakati wowote, cha msingi wajitume katika mazoezi.
Kwa hili Mwambusi ameweza kuwaweka pamoja wachezaji wake na
kuooneana wivu kwenye mechi.
Pili; kujielewa kwa wachezaji wa Mbeya City fc. Ni ngumu sana
kugundua kuwa wachezaji wa klabu hii wapo katika dhiki fulani.
Lakini taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hii ni kuwa kuna
wakati wachezaji wanacheleweshewa mishahara yao na posho.
Wakati wote wamekuwa wavumilivu sana na hii inatokana na makocha
wao kuwajenga katika mazingira ya kuamini kuwa Mbeya City wanapita na safari
yao ni kwenda kimataifa.
Wanapenda kufanya kazi yao na ni wazalendo wakubwa mno, huku
wakiamini kuwa ipi siku watauzika.
Ukiwa na wachezaji wenye malengo ya kufanya kazi kwanza na
kusubiri mafanikio baadaye basi watakusaidia kama ilivyo kwa Juma Mwambusi.
Tatu; nidhamu kubwa kwa wachezaji. Vijana wa Mbeya City fc wana
nidhamu nzuri uwanjani na nje ya uwanja.
Wamejengwa katika misingi ya kuheshimu miiko ya mpira, hivyo ni
ngumu kuwaona wakifanya makosa ya kujirudia rudia au kufanya fujo uwanjani.
Kwa mara ya kwanza walionekana kuwa na hasira katika mechi
iliyopita dhidi ya Azam fc na sababu kubwa ilikuwa ni presha ya mchezo wenyewe.
Lakini kwa takribani msimu mzima wamekuw a na nidhamu nzuri
ikiwepo nidhamu ya uwanjani.
Nne; kufanikiwa kucheza kitimu; Mwambusi amefanikiwa kwa hili kama
makocha wengi duniani wapendavyo.
Kuwa na timu inayocheza kitimu bila kutegemea matokoe kwa
wachezaji fulani ni faida kubwa mno.
Hata timu kubwa duniani kuna wakati zinajenga matokeo yake kupitia
mchezaji mmoja.
Mfano kwa muda mrefu Lionel Messi amekuwa mwamuzi wa matokoe kwa
FC Barcelona pamoja na Cristiano Ronaldo kwa Real Madrid.
Wachezaji hawa wanapokabwa ile `ngado kwa ngado` basi timu nzima
inapwaya.
Lakini kwa kocha Mwambusi imekuwa ni tofauti. Timu yake imekuwa
ikicheza kitimu na kila anapokosekana mchezaji mmoja basi hakuna shida.
Tano; Wachezaji kuwa na nguvu za kucheza kwa dakika zote.
Wanandinga wa Mbeya City wana uwezo wa kucheza kwa dakika zote na kuhimili
presha ya mchezo.
Hawaishiwi na pumzi ndani ya dakika 90. Haya ni matunda ya
maandalizi yao ya muda mrefu.
Wamekuwa hawatabiriki wanapokuwa uwanjani. Kwa muda wote wanacheza
kwa kasi nzuri na kuilinda mpaka mwisho wa mchezo.
Pia hili limewabeba sana tofauti na timu nyingine zinazokata pumzi
katika dakika fulani.
Sita; Mashabiki wengi kuwepo nyuma yao. Kwa msimu mzima mashabiki
wa soka mkoani Mbeya wamekuwa nyuma ya klabu yao na wanaweza kusafiri kwenda
mikoani kuishangilia timu yao.
Wameleta utamaduni mpya kwa timu za Tanzania kwani ni kawaida
kuikuta Simba akicheza na Oljoro lakini mashabiki wa Arusha wanaishangilia Simba
badala ya timu yao.
Kwa Mbeya imekuwa ni tafouti kabisa hata Simba na Yanga zimepoteza
mashabiki wengi.
Wachezaji wanafurahi kuona mashabiki wengi wapo nyuma yao, hivyo
kucheza kwa kujituma ili kuwalipa fadhila.
Mashabiki ni wachezaji wa kumi na mbili, hivyo Mbeya wamefanikiwa
kwa hili na ndio sababu ya timu yao kufanya vizuri msimu huu.
Hizi si sababu pekee zilizowafanya Mbeya City fc kufika hapo
walipo, bali zipo nyingine nyingi ambazo nitazieleza baadaye.
0 comments:
Post a Comment