Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
DIDIER Kavumbagu kwaheri Yanga. Hii ni baada ya
mchana wa leo kusaini mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa wapya wa ligi kuu soka
Tanzania bara, klabu ya Azam fc, lakini kuna kipengele kinachosema ataongezewa
mwaka mwingine kama atafanya kazi nzuri.
Taarifa hii imethibitishwa na meneja wa Azam fc,
wana Lambalamba, Jemedari Said.
“Kavumbagu is a done deal! Tumemalizana nae na
amesaini rasmi mkataba wa mwaka mmoja, so tutakuwa nae msimu ujao kwenye
kampeni ya kutetea ubingwa wetu pamoja na michuano ya klabu bingwa ya Afrika,”
alifunguka Jemedari
Mshambuliaji huyo hatari na nahodha wa timu ya
Taifa ya Burundi ameamua kumwaga wino Azam baada ya Uongozi wa Yanga kusuasua
kumpa mkataba mwingine baada ya ule wa miaka miwili kumalizika.
Kavumbagu mara kadhaa alikaririwa na vyombo vya
habari kuhitaji mkataba mpya katika klabu ya Yanga, lakini viongozi wa kalbu
hiyo hawakuonesha nia na leo hii imeamua kuanza maisha mapya Chamazi.
Katika maelezo yake, Kavumbagu alieleza kuwa mpira
ni sehemu ya maisha yake na kazi yake, hivyo yuko tayari kuichezea klabu yoyote
yenye nia ya kumsajili kwa masharti ya kukidhi mahitaji yake ya msingi.
Azam fc wenye nia ya kufanya vizuri katika
michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani, wamekusudia kuongeza nguvu
katika kikosi chao.
Kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog ameenda
likizo kwao Cameroon , lakini uongozi wa Azam ulithibitisha kupokea taarifa ya
mapendekezo yake na tathimini ya msimu uliomalizika aprili 19 mwaka huu.
Usajili huu unathibitisha kuwa Kavumbagu alikuwa
katika rada za Omog na aliwaachia viongozi mpango mzima.
Kuzugazuga kwa Uongozi wa Yanga kumemfanya nyota
huyo kuangukia mikononi mwa matajiri wa Azam fc japokuwa alikuwa tayari kumwaga
wino tena katika klabu ya Yanga.
Mkataba aliosaini Azam fc unasemekana kuwa na
masilahi bora zaidi ya ule wa Yanga.
Nyota huyo mwenye uchu wa mabao alijiunga na Yanga
mwaka 2013 akitokea klabu ya Atletico ya nchini Burundi.
Kavumbagu amesaini mbele ya Katibu Mkuu wa klabu
ya Azam, Nassor Idrisa makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es
Salaam.
Nassor amekaiririwa na Tovuti ya klabu akisema;
“Tumepata mshambuliaji mzuri, ambaye tayari ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya
Tanzania kwa misimu miwili, mchezaji huyu ni chaguo la kocha wetu Joseph Omog,
ambaye alivutiwa naye baada ya kumuona akichezea klabu yake zamani, Yanga
SC,”alisema.
Kwa upande wake, Kavumbangu ameiambia Tovuti ya
Azam kuwa; “Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga,
lakini viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini,”.
Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu amesema sasa
akili yake anaipeleka kwa mwajiri wake mpya, Azam FC ambako pia amepania kwenda
kushinda mataji na kuiwezesha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa
na familia yake kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.
“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi kujiunga
na klabu hii kubwa. Kawaida yangu huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi
ni mshabiki namba moja wa Azam,”amesema.
Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2013 akitokea
Atletico ya Burundi na katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo,
amefunga mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.
Kila la heri Kavumbagu katika maisha mapya Azam
fc.
0 comments:
Post a Comment