Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
HATIMA ya Ashanti United kubakika ligi
kuu au kushuka daraja itajulikana katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro
aprili 19 mwaka huu wakati itakapokabiliana na Tanzania `Prisons `wajejela`.
Maafande wa Rhino Rangers na JKT Oljoro
tayari wameshakata tiketi ya kushuka daraja na wanasubiri mwenzao wa kuungana nao
katika safari hiyo kati ya Ashanti au Prisons.
Kocha mkuu wa Ashanti, Abdallah
Kibadeni “King Mputa” ameuambia mtandao huu kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu
kutokana na mazingira ya timu zote, lakini amefanya maandalizi makubwa ya
kuibuka na ushindi.
“Nilikabidhiwa timu kwa malengo ya
kuinusuru isishuke daraja. Uongozi umekuwa ukiniunga mkono kwa jitihada zangu.
Tunakaa kambi nzuri lengo likiwa ni kuwatuliza wachezaji wetu katika mechi hizi
za mwisho”.
“Tunajiandaa kuhakikisha tunaibuka na
ushindi dhidi ya Prisons na kubakia ligi kuu. Najua itakuwa mechi ya ushindani,
lakini nawapanga wachezaji wangu kukabiliana na wenzetu”. Alisema Kibadeni.
Kocha huyo aliongeza kuwa mechi hiyo
inamnyima usingizi kwasababu muda wote anatafakari mbinu za kuwafunga Prisons.
Aidha, alikiri kuwa Prisons imekuwa
bora zaidi mzunguko wa pili na wamekuwa wakicheza soka zuri, hivyo lazima
ajipange kumaliza biashara mapema siku hiyo.
“Hatuna haja ya kulinda, tutashambulia
mda wote ili kupata mabao ya mapema. Lakini mabeki wangu na sehemu ya kiungo
watatakiwa kucheza kwa uangalifu mkubwa ili kutofungwa siku hiyo”. Alisema
Kibadeni.
Wakati Kibadeni akikesha kufikiria dawa
ya Prisons, naye kocha wa Wajelajela, David Mwamwaja usingizi unampaa kila siku
akiwaza mechi hiyo.
Mwamwaja ataingia katika mchezo huo
akiwa na malengo sawa na Kibadeni kwasababau naye alipewa timu ili ainusuru na
janga la kushuka daraja.
Mwamwaja anasema wapo katika maandalizi
makubwa ya kuzima ndoto ya Ashanti msimu huu.
“Tutacheza mpira kwa makini zaidi.
Tunajua kufungwa itakuwa mwiba kwetu”.
“ Tutalinda lango letu na kushambulia
kwa muda wote wa mchezo, Nawaandaa wachezaji wangu kucheza kitimu zaidi ili
kusaidiana katika mchezo huo”. Alisema Mwamwaja.
Mpaka sasa timu zote zimecheza mechi 25
na kujikusanyia pointi 25. Kinachozitofautisha ni mabao ya kufunga na kufungwa.
Prisons wamecheza mechi 25 ambapo
wameshinda mechi 5, sare 10 na kupoteza mechi 10.
Wajelajela hao wamefumania nyavu mara
25 na kufungwa mabao 33. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa unapata hasi (-8).
Ashanti United wameshinda mechi 6, sare
7 na kufungwa mechi 12.
Wamefunga mabao 20 na kufungwa mabao
38. Ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa anapata hasi kumi na nane (-18).
Kwa wastani huo wa mabao ya kufunga na
kufungwa, Prisons wanakuwa juu ya Ashanti United.
Katika msimamo, Prisons wapo nafasi ya
11, huku nafasi ya 12 ikikaliwa na Ashanti United, lakini zimefungana pointi.
Kuelekea katika mechi hiyo, klabu zote
zinahitaji ushindi, lakini Ashanti ndio wahitaji wakubwa zaidi kwasababu
wamezidiwa mabao mengi ya kufunga na Prisons.
Endapo Ashanti United watashinda mechi
hiyo watafikisha pointi 28 na kuvuka mkasi wa kushuka daraja, wakati Prisons
watakuwa wameshashuka daraja.
Matokeo ya sare ya aina yoyote ile
yatawashusha daraja Ashanti kwasababu ya wastani wa mabao ya kufunga na
kufungwa.
Kama Prisons watapata sare siku hiyo,
watakuwa wamenusurika kushika daraja kwa faida ya mabao ya kufunga na kufungwa.
0 comments:
Post a Comment