Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
COASTAL UNION maarufu kwa jila `Wagosi wa Kaya`
hawajajitendea haki kumaliza katika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa ligi kuu soka
Tanzania bara msimu huu.
Wakicha chini ya kocha Mkenya, Yusuf Chipo, Costal
wamefanikiwa kukusanya pointi 29 tu katika michezo 26 waliyocheza msimu huu.
Wamefanikiwa kushinda mechi 6 tu, sare 11 na
kufungwa mechi 9.
Jana katika mechi ya mwisho walipokea kichapo cha bao
1-0 kutoka kwa Kagera Sugar katika uwanja wao wa Mkwakwani.
Coastal ni mjoa ya timu iliyofanya maandalizi
makubwa msimu huu na kusajili wachezaji wazuri.
Waliwekeza fedha nyingi katika kikosi chao na
kuweka kambi nzuri kwa wachezaji wao.
Kumbuka wakijiwinda na mzunguko wa pili, walienda
kuweka kambi nchini Oman ambako walicheza mechi za kirafiki.
Wakati wakiwa Oman, Yanga walikuwa zao Uturuki
kujiandaa na mzunguko wa pili.
Haya ni maandalizi makubwa sana kwa klabu, hivyo
walistahili kushika nafasi tatu za juu.
Yanga ya Uturuki imeshika nafasi ya pili kwa
pointi 56, huku Azam fc walioenda Afrika kusini kujiandaa kabla ya ligi kuu
msimu huu kuanza wakimaliza na pointi 62 kileleni na kuwa mabingwa wapya.
Mbeya City waliomaliza nafasi ya tatu kwa pointi
49, wao walikaa zao mwakareli Tukuyu kwa muda mrefu.
Simba nao walifanyia maandalizi hapahapa nchini,
kama ilivyo kwa klabu nyingi za ligi kuu.
Yanga, Azam fc na Coastal ni klabu zilizotumia
fedha nyingi katika maandalizi ya msimu huu, japokuwa Azam walifanya hivyo
kabla ya ligi kuanza.
Malengo ya Coastal na Yanga kwenda nje ya nchi
kabla ya kuanza mzunguko wa pili yalikuwa ni kusaka ubingwa au nafasi tatu za
juu.
Hata katika usajili, Coastal walinasa nyota kibao
wakiwemo akina Haruna Moshi `Boban`, Juma Nyoso, Kato Yayo kutoka Uganda,
Mkenya Crispian Odula, Jerry Santo, Shaban Hassan Kado na wengine wengi.
Mbali na kusajili nyota hao, pia kuna wachezaji
wengine wenye viwango vizuri.
Akina Fikirini Suleiman, Hamadi Juma, Abdi Banda,
Yusuf Chuma, Mbwana Kibacha, Razak Khalfan, Ally
Nassor ‘Ufudu’, Behewa Sembwana, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Kenneth Masumbuko,
Danny Lyanga ni wachezaji wazuri sana.
Pia wapo akina
Mansour Alawi, Ayoub Masoud, Marcus Ndeheli, Ayoub Semtawa, Mohammed Miraji,
Crispian Odula, na Mohammed Kipanga.
Coastal Union ina
wachezaji wa aina zote. Wapo wenye uzoefu na vijana wadogo.
Mechi za mwisho,
kocha Chipo aliamua kutumia vijana wengi ambao walionekana kukiongezea kasi
kikosi chake.
Binafsi nafasi ya
tisa kwa Coastal naiona kama hukumu kubwa kwao.
Kwa jinsi
walivyotumia mkwanja mrefu hawakustahili kukaa katika nafasi hiyo.
Lakini ukirudi
uwanjani, jinsi wachezaji hawa wanavyocheza, utagundua kuna kitu hakiko sawa
klabuni hapo.
Wachezaji wanafanya
uzembe mwingi bila sababu na wanakuwa chini ya morali katika mechi nyingi.
Nadhani mivutano ya
muda mrefu ya viongozi wa Coastal Union imekuwa chanzo kikubwa kwa klabu hiyo
kufanya vibaya.
Hakuna uelewano wa
viongozi kwenye baadhi ya mambo ya msingi.
Tulisikia juzi juzi
wanachama wa Coastal wakilalamika kubaniwa kadi za uanachama kwa muda mrefu
bila sababu ya msingi.
Coastal ni timu ya
watu, lakini viongozi wamekuwa na mambo yao kinyume na matakwa ya mashabiki
wao.
Hata maamuzi ya
kumfukuza kocha Hemed Morroco yalichukuliwa kwa matakwa ya watu wachache na si
kwa mafanikio ya klabu.
Mara nyingi Morroco
alikuwa anakaririwa akisema haelewi kwanini wachezaji wake wanashindwa kufanya
vizuri.
Nadhani ilifika
wakati hakuwa na uhusiano mzuri na mabosi wake mpaka anaamua kuondoka.
Lakini ishu kubwa sio
kwa viongozi kuvutana, hata wachezaji wana wajibu wa kuivusha klabu kufika pale
inapohitaji.
Timu ina Boban,
Nyoso, Kato, Odula, Santo inashindwaje kukaa hata timu nne za juu au hata sita
basi.
Hakika wachezaji wa
Coastal wanatakiwa kukaa chini na kufanya tathmini ya kuboronga kwao msimu huu.
Wamekaa kambi nzuri,
wamepewa pesa na kupelekwa mpaka Oman, lakini wanaifanya klabu kuwa ya tisa.
Hakika kila mtu ndani
ya Coastal Union anatakiwa kuwajibika kwa nafasi yake.
Kama kuna matatizo ya
uongozi, basi wakae chini na kumaliza mivutano yao ili waifanikishe timu.
Kufanya vibaya ni
kuwakatisha tamaa wadhamini wao. Nani wakuweka pesa sehemu isiyokuwa na faida?.
Mtu anapoamua
kuwekeza ndani ya timu, anategemea kufanya biashara na kufikia malengo yake.
Kiukweli hakuna mtu
anayeweza kuwekeza sehemu ambayo hailipi.
Coastal wanatakiwa
kujipanga vizuri ili kupata mafanikio sawa na pesa wanazowekeza.
Wachezaji nao
wajipange upya. Kwa wale watakaokuwepo
msimu ujao waje na mtazamo mpya wa kuisaidia timu.
Moja kati ya amri kuu
ya mpira miguu katika amri zake 10, ni mchezaji kucheza kwa faida ya timu.
Kama timu inashindwa
kupata matokeo, nawewe mchezaji kwa jitihada zako binafsi unaona unaweza kuiokoa,
basi fanya kazi hiyo kwa maslahi ya timu.
Lakini wachezaji wa
Coastal Union kuna wakati wanaonekana
kuwa chini ya kiwango na ukiwaangalia unagundua kuna tatizo vichwani mwao.
Poleni Coastal Union,
huo ndio mpira, lakini jipangeni sawasawa kwa msimu ujao.
Mkienda tena Oman mje
na nguvu kubwa zaidi, na sio kuwa wachovu kama ilivyotokea msimu huu.
Viongozi wa klabu kaeni chini kujua wapi
mmekosea ili kuisaidia timu yenu msimu ujao.
0 comments:
Post a Comment