BAYERN Munich wamevuliwa ubingwa wa UEFA kwa kipigo
cha mbwa mwizi baada ya kufungwa mabao 5-0 na Real Madrid katika mechi mbili za
nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mechi ya kwanza katika dimba la Santiago Bernabeu,
Real Madrid walishinda bao 1-0 na leo hii katika nusu fainali ya pili kwenye
uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, kikosi cha Carlo Ancelotti kimeibuka na
ushindi wa mabao 4-0.
Real Madrid walitumia dakika 16 tu
kufunga goli ambapo Luca Modric alichonga kona kutoka winga ya kulia na Sergio
Ramos kujitwishwa mpira huo na kuuzamisha kimiani.
Dakika nne baadaye, beki huyo wa kati
aliwamaliza Bayern baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo
uliochongwa na Gareth Bale.
Baadaye Real Madrid walifanya
shambulizi la kushitukiza ambapo Cristiano Ronaldo alifunga bao safi baada ya
Bale kumpatia pasi murua.
Bao hilo liliwafanya Real wahitimishe
dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa mabao 3-0.
Bao la dakika ya 90 la Cristiano
Ronaldo kwa njia ya adhabu ndogo lilitia chumvi katika kidonda cha Bayern na
kuvuliwa ubingwa kwa wastani wa mabao 5-0.
Kabla ya mechi hii, nyota
wa zamani wa soka la Ujerumani, Stefan Effenberg alionesha wasiwasi wake kama
falsafa ya Pep Guardiola itaisaidia Bayern Munich kutwaa ubingwa wa UEFA, wakati huu ambapo mchezaji muhimu Frank Ribery
yupo katika kiwango cha chini.
Effenberg anaamini falsafa ya sasa ya Bayern ya
kupiga pasi nyingi haikuweza kuwasaidia Bernabeu na alikuwa na wasiwasi katika
mechi ya leo.
Kipigo cha mabao 4-0 kimethibitisha mawazo ya
gwiji huyo wa soka la Ujerumani.
Tangu enzi za Zinedine Zidane, Luis Figo, Roberto
Carlos na Raul, Real Madrid hawajacheza fainali na sasa wamefanikiwa kuelekea La
Decima mjini Lisbon mwezi ujao.
Kabla ya mechi, watu walikuwa wanasema
Real Madrid wanahitaji bao 1 zaidi au suluhu ili kuwashinda Bayern, lakini
wameweza kushusha mvua kubwa ugenini.
Baada ya mechi hiyo, Gareth Bale amesema kipigo
walichotoa leo hii ni sababu mojawapo ya yeye kujiunga na klabu kubwa duniani
majira ya kiangazi mwaka jana.
“Ni matokoe mazuri mno kwetu. Nadhani tumejituma,
tulitumia vizuri mbinu zetu na kucheza vizuri usiku huu, hivyo tulistahili
ushindi”. Bale amezungumza na ITV.
“Walicheza mpira sana, waliacha nafasi za
kushambuliwa kwa kushitukiza, nasisi tunapenda hivyo”.
“Tuna wachezaji wenye kasi na tunatumia nafasi
kama hizo. Tulikuwa katika kiwango bora na tumefurahi kufika fainali”.
“Lakini kuna hatua nyingine mbele”.
“Kiukweli hii ndio sababu ya kwanini nilijiunga na
Madrid. Ndio maana niliamua kuja kujiunga na klabu kubwa zaidi duniani”
“Lengo ni kushinda makombe na mechi kubwa. Tunatakiwa
kushinda taji, tutakuwa na fainali ngumu kwa timu yoyote itakayopita kesho”.
Ronaldo baada ya kufunga mabao mawili usiku huu
amevunja rekodi ya Lionel Messi kwa kufikisha mabao 16 katika msimu mmoja wa
UEFA.
Real Madrid wamefuzu kwa mara ya kwanza fainali
tangu walipofanya hivyo mwaka 2002 na kutwaa kombe na sasa wanatarajia kukutana
na Chelsea au Atletico Madrid ambazo zitapambana kesho katika uwanja wa
Stamford Bridge.
Mechi ya kwanza katika dimba la Vicente Calderon
mjini Madrid, Chelsea walilazimisha suluhu ya bila kufungana, hivyo wanahitaji
bao 1-0 ili kufuzu fainali.
0 comments:
Post a Comment