Na Baraka Mpenja, Dar Es
Salaam
AZAM FC baada ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza msimu huu wa mwaka
2013/2014 wamekumbwa na tuhuma nzito za kufanya mchezo mchafu wa kununua mechi.
Maneno haya yalianza kusikika zaidi kuelekea katika mechi yake
dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Mabatini Mkoani Pwani na mechi ya Mbeya
City mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Azam fc walituhumiwa kuwahonga Mbeya City basi, kocha Juma
Mwambusi kujengewa nyumba ya kisasa Chamazi na wachezaji kupewa hela ili wacheze chini ya kiwango.
Baada ya kusikika kwa tuhuma hizi, viongozi wa Mbeya City
kupitia kwa katibu mkuu Emmanuel Kimbe walikanusha vikali tuhuma hizo.
Siku ya mechi, Mbeya City walicheza kwa nguvu na kuonesha kuwa
hawajahongwa, lakini mwisho wa siku walipoteza mchezo huo kwa mabao 2-1 na
kuwapatia Azam ubingwa.
Hata hivyo mchezo huo uliingia dosari baada ya wachezaji wa
Mbeya City kumzonga mwamuzi kwa madai ya kuwapa Azam bao kinyume na sheria,
japokuwa haikuwanusuru na kipigo.
Kimsingi hizi ni tuhuma tu za mtaani kwasababu hakuna
alijitokeza hadharani kutoa ushahidi wa Azam fc kufanya uchafu huo.
Azam ni timu pekee iliyocheza mechi 25 bila kufungwa msimu huu,
huku wakijiandaa kucheza na JKTR Ruvu katika uwanja wa Azam Complex mwishoni mwa
wiki.
|
Kocha msaidizi wa Azam fc, Kalimangonga Ongala (wa kwanza kushoto) na kocha mkuu , Mcameroon Joseph Marius Omog (wa pili kulia)
Hii itakuwa mechi ya kuandika historia nzuri kwa Azam kwasababu
wakishinda watakuwa wametwaa ubingwa wao wa kwanza bila kufungwa mechi yoyote.
Ikitokea hivyo itakuwa faraja kubwa kwa kocha mkuu, Mcameroon,
Joseph Marius Omog pamoja na wachezaji kwa ujumla.
Toka mwanzo wa ligi ya msimu huu, Azam fc walionesha nia ya
kuhitaji kutwaa taji wakati huo wakiwa chini ya kocha mkuu, Mwingereza Sterwart
John Hall.
Baada ya Hall kuachana na timu mwishoni mwa mzunguko wa kwanza,
Omog alikabidhiwa mikoba na kuendeleza rekodi ya kutofungwa kwa Azam fc mpaka
sasa.
Katika mechi 25 walizocheza, Azam fc wamejitahidi kulinda rekodi
ya kutofungwa, lakini mechi za mwishoni zimezua maneno mengi.
Ushindani mkubwa uliokuwepo baina ya Azam fc dhidi ya Yanga
katika kinyang`anyiro cha ubingwa kumesababisha yazuke mengi.
Yanga walihitaji kutetea ubingwa wao, wakati Azam fc walikuwa
wanahitaji ubingwa wao wa kwanza.
Nao Mbeya City walikuwepo katika mbio hizo, japokuwa
waliharibikiwa mechi za mwisho.
Kabla ya kuanza msimu huu, Azam fc waliwekeza katika kikosi chao
kwa nguvu zote ingawa hawakufanya usajili mkubwa kama ilivyokuwa kwa Yanga.
Klabu hii imejijenga kwa kila kitu na kwa misimu miwili imeshika
nafasi ya pili, hivyo msimu huu ilikuwa inahitaji ubingwa tu.
Baada ya kuzuka kwa tuhuma za kununua mechi, viongozi wa Azam fc
wameshindwa kuvumilia kabisa.
Katibu mkuu wa klabu hiyo, Nassoro Idrisa `Father` kupitia tovuti ya klabu
amesema kuwa maneno yanayozungumzwa kuwa wananunua mechi ni porojo tupu.
“Baada ya Azam Fc kupata mafanikio ya kuwa bingwa wa ligi kuu ya
Tanzania Bara inazunguzwa vibaya. Azam
Fc ilipata nafasi ya pili mara Mbili katika Ligi Kuu,lakini haikuwahi kusemwa
imenunua mechi, leo iweje imekuwa Bingwa isemwe imenunua”. Alisema Idrisa.
Idrisa aliongeza kuwa John Bocco aliweka Historia baada
ya Kufunga Goli la Ushindi katika Mechi ya mwisho ya Ligi Daraja la kwanza na
Kuipandisha Azam Fc kucheza Ligi kuu, na sasa wameshuhudia Bocco akiweka
Historia ya Kufunga Goli la Ushindi na Kuipa Timu
yake Ubingwa kwa Mara ya kwanza tangu ilipopanda Daraja msimu wa 2008/2009”.
“Hatutopuuzia mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu. Tutacheza kama
mechi nyingine tulivyocheza .Tunahitaji kuweka Historia ya Kutopoteza hata
Mechi Moja kwa Msimu huu, hivyo JKT Ruvu wajiandae kwa Kichapo wakati tukiwa tunakabidhiwa
Kombe letu la Msimu Huu”.
“Baadhi ya Maneno ambayo Makocha wanazungumza Sio
Mazuri . Wao kama wataalam hawatakiwi kujihusisha katika Propaganda ambazo
baadhi ya watu wanaziendeleza”. Alisema Idrisa.
|
0 comments:
Post a Comment