
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
HONGERENI
Mbeya City fc kwa kumaliza nafasi ya tatu kwa pointi zenu 49 katika
msimu wenu wa kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Haya ni mafanikio makubwa kwenu kwasababu mmewachomoa wakongwe Simba, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar katika nafasi tatu za juu.
Mlianza ligi kwa nguvu na kufanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa.
Mmefanikiwa kushinda mechi 13 kati ya 26, mmetoa sare 10 na kufungwa mechi 3.
Mmefunga mabao 33 na kufungwa mabao 20. Si haba kwenu.
Hata hizo mechi tatu mlizofungwa si kwamba mlicheza vibaya.
Mechi yenu ya kwanza kufungwa ilikuwa dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa ambayo mlilala kwa bao 1-0.
Bao
la mapema la Mrisho Ngassa, lakini mlicheza kwa kujituma zaidi na huku
mkiwa pungufu baada ya fundi wenu wa kati Steven Mazanda kulimwa kadi
nyekundu.
Coastal
Union waliwafunga 2-0 Mkwakwani na mkapoteza mechi yenu ya tatu dhidi
ya Azam fc kwa kufungwa mabao 2-1 na kuwapa ubingwa msimu huu.
Haya ni mafanikio makubwa kweni, cha msingi mjiandae kwa msimu ujao.
Wenzenu
wawili mliopanda nao daraja, Rhino Rangers na Ashanti wameshashuka
daraja, lakini ninyi mmefanikiwa kushika nafasi ya tatu. Pongezi muhimu.
Mbeya
City wakati wanaanza ligi kwa kasi, watu wengi walisema ni nguvu ya
soda. Wakidhani mtapoteana mechi kadri zinavyozidi kwenda.
Baadhi ya mashabiki waliwaponda kuwa wanakamia mechi, lakini mzunguko wa kwanza ulimalizika bila kufungwa.
Wakatabiri
kuwa mzunguko wa pili vijana hawa wa Juma Mwambusi watapoteana zaidi,
lakini walikaza na kufungwa mechi tatu tu kati ya 13.
Mchango wa Mbeya City fc msimu huu ni mkubwa mno katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Licha
ya kuleta ushindani wa uwanjani kwa kuzisumbua klabu za Simba na Yanga,
Wagonga nyundo hawa wa Mbeya wameifanya ligi kuwa maarufu zaidi msimu
huu.
Huu ni mchango wao mkubwa kwasababu mashabiki wote walikuwa wanaijadili timu hii kila inapotarajia kucheza amechi.
Simba, Yanga ni klabu kongwe. Azam fc si wakongwe, lakini wamewazidi umri Mbeya City.
Timu hizi tatu zilishasemwa sana, lakini ujio wa Mbeya City fc ulileta uhondo mwingine.
Unakumbuka
jinsi mechi ya Mbeya City dhidi ya Yanga, Simba na Azam fc zilivyosemwa
kwenye vyombo vya habari na kwa mashabiki wa kawaida.
Nini kilichangia haya, bila shaka ni ubora na ushindani mkubwa wa Mbeya City fc.
Kwahiyo licha ya kuleta changamoto uwanjani, pia wameifanya ligi izungumzwe mno msimu huu.
Hata nje ya nchi, ligi ilikuwa inasemwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wanaume hawa kutoka jiji la kijani.
Watanzania wengi wanaoishi nje ya nchi walijikuta wakivutika kuifuatili timu ya Mbeya City na kuifanya ligi kuwa maarufu kwao.
Kwa hili Mbeya City wanastahili pongezi kwa roho safi, ukinuna sio mzalendo wa soka na sio shabiki bora.
Mtu anapochangia kitu fulani hasa kutangaza ligi ya nchi, lazima apewe haki yake ya kupongezwa.
Tazama ubingwa wa Azam fc ulivyoleta uhondo mpya. Mitandao mikubwa ya kimichezo duniai inauangazia ubingwa huu.
Kama Simba au Yanga ingwetwaa taji, ingekuwa kawaida kwasababu wamezoeleka, lakini kwa Azam fc imekuwa mpya kabisa.
Sasa watu wanajadili mafanikio ya Azam. Kwa lugha nyepesi Azam wameitangaza ligi zaidi msimu huu.
Kwa mpira wa uwanjani, Mbeya City fc walionekana kuwa imara na kujipanga vizuri.
Ni timu ambayo haitengenezi matokeo kwa kumtegemea mtu mmoja.
Wana wachezaji wanaofanana viwango na Mwambusi anaweza kuwatumia wote kadri atakavyo.
Walionekana kuimarika kimazoezi na kuwa na pumzi kubwa uwanjani.
Haya ni mafanikio kwao na Mwambusi anastahili kupongezwa kwa hili.
Makocha wengi wanapenda kuwa na timu na si wachezaji au mchezaji.
Unapomtegemea mchezaji mmoja kufunga basi akikabwa sana hauna matokeo.
Mbeya City ni tofauti kabisa, Paul Nonga, Jeremiah Peter, Saady Kipanga, Mwegane Yeya, Peter Mapunda, Richard Peter wote wakianzishwa wanaweza kufunga.
Hili ni jambo zuri sana kwa Mbeya City fc na pengine klabu zote zinatakiwa kuwa hivyo.
Nidhamu kubwa ya uwanjani na nje ya uwanja kwa wachezaji wa Mbeya City fc pia ni mafanikio mengine.
Wamekuwa waadilifu kwa kazi yao na si wazungumzaji wa mambo ya ndani ya klabu.
Si rahisi kujua hawajalipwa posho au mshahara. Hapa wameweza kujitambua kwelikweli na wanazingatia kazi kuliko maslahi binafsi.
Mashabiki wa Mbeya pia wametisha sana msimu huu. Wamesafiri mikoa mbalimbali kuwashangilia vijana wao.
Huu
ni mfano mzuri wa kuigwa na kama timu mpya zilizopanda zitapewa sapoti
kubwa kiasi hiki, basi tutegemee ligi kuu nzuri mwakani.
Watu wa Shinyanga nasikia wameweka pembeni mambo ya Simba na Yanga, sasa kwa nguvu moja ni Stand United.
Nako Mtwara kuna wazee wa Ndanda fc kwa roho safi. Simba, Yanga sidhani kama watapata urahisi huko.
Kwa Polisi Moro hakuna mishemishe kabisa na hii nadhani inatokana na timu hiyo kutokuwa ya wananchi.
Yapo mengi ya kusema juu ya Mbeya City, lakini kwa leo yanatosha na tutaendelea kukupasha kadri siku zinavyoenda.
Kila la heri Mbeya City katika harakati zenu za soka.
0 comments:
Post a Comment