
Cristiano
Ronaldo ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Real Madrid tangu ajiunge
na miamba hiyo ya soka la Hispania mwaka 2009 akitokea kwa mabingwa
watetezi wa ligi kuu soka nchini England, Manchester United.
Wakati akijiunga na Madrid tayari nyota huyo raia wa Ureno alikuwa ni mchezaji bora wa dunia mwaka 2008.
Tangu
akiwa Man United, Ronaldo akiwepo uwanjani ilikuwa faida kubwa kwa Sir
Alex Ferguson ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa mlezi wa mchezaji huyu.
Na alipotua Real Madrid, amekuwa mchezaji muhimu kwa wakati wote na kila anapokosekana basi imani ya Madrid inashuka.
Wachezaji wenzake na benchi la ufundi wanamheshimu sana Mreno huyo na wanamuona kama mfalme wao.
Ni kweli kila kocha anatamani kuwa na mchezaji kama Ronaldo.
Lakini
wapo wachezaji wengine Real Madrid wanaoweza kuamua matokeo wakiwemo
Gareth Bale, Angel Dimaria, Karim Benzema na wengineo.
Kwa
muda mrefu nyota huyo amekuwa mwamuzi wa matokeo ya Real Madrid, lakini
hapo jana mambo yamekwenda taofauti kabisa katika fainali ya kombe la
mfalme.
Baada
ya kutwaa kombe la Mfalme jana usiku bila Cristiano Ronaldo, kocha wa
Real Madrid ameibuka na kusema kukosekana kwa mchezaji huyo
kuliwaongezea morali zaidi.
Real
iliwatumia Angel Di Maria na Gareth Bale kufunga mabao yake ni kubeba
mwari mbele ya FC Barcelona kwenye uwanja wa Mestalla.
Mreno, Ronaldo alikosa mechi ya jana ya `El Clasico`kwa sababu ya kuwa majeruhi.
“Tulistahili
ubingwa. Tulicheza kwa umakini na kuwashambulia kwa kushitukiza.
Tulicheza vizuri na wachezaji walijituma mno, kwahiyo nawapongeza kwa
hilo”.
“Kutokuwepo
kwa Ronaldo kuliwapa morali wachezaji. Hali hii iliwafanya wacheze kwa
bidii zaidi. Wote walicheza vizuri. Unahitaji kucheza kitimu ili umfunge
Barca na tumefanya hivyo”. Amesema Ancelloti.
Madrid
wiki ijayo wanatarajia kukutana na Bayern Munich katika nusu fainali ya
kwanza ya UEFA, lakini bado wapo katika vita ya kutafuta ubingwa wa La
Liga japokuwa Atletico Madrid wanaongoza kwa pointi tatu zaidi na
wakibakiwa na mechi tano.
Kwa
upande wa Barca, msimu huu wapo hatarini kubaki mikono mitupu baada ya
kutolewa UEFA, na jana wamekosa kombe la Mfalme. Pia wiki iliyopita
walifungwa na Granada katika mchezo wa La Liga.
Kuhusu Barcelona, Ancelotti amesema;
“Sidhani
kama unaweza kuwaondoa kwenye mbio. Wanacheza mpira mzuri japokuwa
mambo hayaendi vizuri kwao msimu huu, lakini watapambana mpaka dakika ya
mwisho kwenye ubingwa na bado ni wapinzani hatari sana”.
Zaidi Ancelloti ameisifu timu yake kucheza kitimu, lakini anaamini mshindi wa jana ni Gareth Bale.
“Alicheza mpira mzuri mno na kufunga bao muhimu. Lakini wachezaji wote walicheza vizuri”.
0 comments:
Post a Comment