Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
HUWEZI amini!. Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka
Tanzania bara wameweka rehani nafasi yao ya kutetea taji lao msimu huu baada ya
kufumuliwa bila haruma mabao 2-1 na wapambanaji wa kukwepa kushuka daraja,
Mgambo JKT katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa CCM Mkwakwani, Jijini
Tanga.
Yanga wakiwa na kikosi kamili gado waliingia
uwanjani wakiwa na imani kubwa ya kuibuka na ushindi ili kuwasogelea Azam fc
wanaozidi kutesa kileleni.
Maafande wa Mgambo walianza kushusha kirungu cha
kwanza katika dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao hatari,
Fully Maganga.
Bao hilo lilidumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza
zinamaliza.
Mbaya zaidi, Mgambo walilazimika kubaki pungufu kwa
dakika 60 baada ya mchezaji wao Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 30 kipindi cha
kwanza.
Baada ya kipindi cha pili kuanza, Yanga waliingia
kwa kasi wakihitaji kupata bao la kasawazisha.
Dakika ya 50, Yanga walifanikiwa kupata penati na
nahodha wake, Nadir Haroub `Canavaro` aliukwamisha mpira kimiani kwa shuti
kali.
Dakika ya 69, Mgambo JKT walipata penati iliyokwamishwa kimiani na Malima Busungu na
kuandika bao la pili kwa maafande hao wa Jeshi la kujenga Taifa.
Mpaka dakika 90 zinamalizika, Mgambo
walikuwa mbele kwa mabao mawili, huku kikosi cha Hans Van Der Pluijm
kikiambulia bao moja la kufutia machozi.
Mechi nyingine iliyokuwa
ikiangaliwa kwa jicho la tatu ni baina ya vinara wa ligi kuu, Azam fc dhidi ya
Simba SC kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Azam fc wamefanikiwa kuvuna pointi
tatu muhimu baada ya kuikung`uta Simba sc mabao 2-1.
Mabao ya Azam fc yalifungwa na
Hamis Mcha `Vialli` mnamo dakika ya 16 kipindi cha kwanza, lakini Simba sc
walisawazisha dakika ya 45 ya kipindi hicho kupitia kwa Joseph Owino.
Azam fc waliandika bao la pili na
la ushindi kupitia kwa nahodha wake, John Raphael Bocco `Adebayor` katika
dakika ya 56.
Baada ya mchezo huo, afisa habari Azam fc, Jafar Idd Maganga amesema bado
wanaendelea kupambana mpaka dakika ya mwisho ili kujua kama watabeba ubingwa.
“Tunamshukuru Mungu tumeweza
kucheza kadri ya uwezo wetu na kuwafunga Simba mabao 2-1. Vijana wetu
wameendelea kukomaa na kuonesha kuwa wao ni bora. Ligi bado sana, tuna mechi
nyingine, tutahakikisha tunashinda zote
na kujihakikishia ubinwa”. Alisema Jafar.
Kwa upande wa Simba Sc wameendelea
kuwa wapole na kukubali matokeo ya uwanjani.
Afisa habari wa Simba, Asha Muhaji
alisema mechi ilikuwa ngumu kwao kutokana na ubora wa Azam fc, hata hivyo timu
imecheza vizuri na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.
“Mpira ndivyo ulivyo. Matokeo ya
uwanjani lazima uyakubali. Wenzetu walitumia nafasi vizuri na kushinda.
Tunasahau ya leo tunajiandaa na mechi ijayo”. Alisema Asha.
Mechi nyingine imepigwa katika
dimba la Sokoine jijini Mbeya ambapo wagonga nyundo, Mbeya City FC walikuwa na
kibarua kizito dhidi ya Tanzania Prisons.
Ulikuwa mchezo muhimu kwa timu
zote, lakini ulikuwa muhimu zaidi kwa Prisons kwasababu wapo katika hatari ya
kushuka daraja.
Dakika 90 zimemalizika kwa Mbeya City
Kuvuna Pointi tatu muhimu kufuatia ushindi wa bao 1-0.
Bao hilo limefungwa dakika ya pili ya kipindi cha
kwanza kupitia kwa mshambuliaji hatari, Paul Nonga.
Afisa habari wa Mbeya City, Freddy Jackson alisema
Prisons walijipanga vizuri kwa lengo la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0
mzunguko wa kwanza.
“Mbeya City nafasi bado tunayo. Sisi tunafukuzia
nafasi mbili za juu. Kufungwa kwa Yanga leo kwetu ni heri. Tunajipanga kushinda
mechi zote. Lolote linaweza kutokeo, Kupoteza kupo”.
“Hata hao wa juu wanaweza kupoteza na ndio maana
umeona Yanga wamefungwa. Mungu atapanga mwisho wa siku nani ashike nafasi hizo”.
Alisema Freddy.
Tanzania Prisons kupitia kwa katibu mkuu wake,
Sadick Jumbe wamekiri kuzidiwa maarifa na Mbeya City, hivyo hawana cha kulaumu
zaidi ya kujipanga mechi zijazo.
“Timu ilicheza vizuri, lakini tulifungwa mapema na
kuharibikiwa na mchezo. Bado tunasema, nafasi yetu ipo hata kama Mgambo
wameshinda leo dhidi ya Yanga”.
“Ona maajabu ya Mpira, Yanga wametoka kutufunga
mabao 5-0, leo wamefungwa 2-1 na wanyonge wenzetu. Lolote linaweza kutokea
katika soka.” Alisema Jumbe.
Mechi ya Azam fc dhidi ya Simba, Mgambo na Yanga, Mbeya
City dhidi ya Prisons zilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kwa mashabiki na makocha
wa timu hizo zinazowania nafasi tatu za juu.
Baada ya Azam fc kushinda, wametia mguu mmoja ndani
mwingine nje katika mbio za kutwaa ubingwa mwaka huu.
Sasa wameshatimiza michezo 23 kwa kujikusanyia
pointi 53 kileleni, huku Yanga wakicheza mechi 22 na kuvuna pointi 46 kibindoni
katika nafasi ya pili.
Matokeo ya Azam yamekuwa faraja kubwa kwa kocha
Joseph Marius Omog wa Azam fc kwasababu sasa ameweka pengo la pointi 7 dhidi ya
mabingwa watetezi Yanga.
Kwa maana hiyo, Yanga wameweka ubingwa wao reheni na
nguvu kubwa inahitajika kuwazuia Azam fc ambao hawajafungwa mpaka sasa.
Yanga wamebakika kiporo kimoja dhidi ya Kagera Sugar
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, April 9 mwaka huu.
Hata hivyo bado watahitaji kujipanga zaidi kwasababu
matokeo yanayopatikana uwanjani kwa sasa yamekuwa ya ajabu kidogo.
Wakati wanaelekea Tanga, bila shaka walidhani
wanaenda kuvuna pointi tatu muhimu mbele ya Mgambo na kila mtu alikuwa
anafikiria hivyo kutokana na ubora wao na kiwango walichoonesha kwenye mchezo
uliopita dhidi ya Prisons.
Mtandao huu jana uliwapa tahadhari Yanga kuwa
wasiende kirahisi na hii ilitokana na maneno ya kocha msaidizi wa klabu hiyo,
Charles Boniface Mkwasa aliyesema kuwa Mgambo
ni timu ndogo, hivyo watahangaika sana, lakini mwisho wa siku wajue Yanga ni
timu kubwa na kongwe.
Hakuna aliyetarajia matokeo ya leo, na hii imezidi
kuwapa hofu zaidi Yanga katika michezo yao iliyobaki dhidi ya Kagera Sugar, JKT
Ruvu, JKT Oljoro na Simba sc.
Yanga lazima watulize akili zaidi kuhakikisha
wanashinda mechi zote kama kweli wanahitaji kutetea ubingwa wao.
Nao Azam fc wamebakiwa na mechi tatu dhidi ya Ruvu
Shooting, Mbeya City na JKT Ruvu.
Katika mechi hizo tatu, Mbili atasafiri kwenda
mkoani Pwani na nyingine atakwenda Mbeya, baada ya hapo atamalizia nyumbani
kwake Azam Complex, Chamazi.
Mbeya City baada ya ushindi wa leo, wamefikisha
pointi 45, pointi moja nyuma ya Yanga.
Hii imezidi kuwapa njia Mbeya City kuwania nafasi
mbili za juu.
Kama matokeo yanayopatikana ndio haya, huwezi
kutabiri kirahisi nani anaweza kutwaa ubingwa.
Nafasi ya kubeba taji ipo wazi kwa timu tatu za juu na
klabu yoyote inaweza kupoteza mchezo na kujiweka mazingira magumu zaidi.
Katika mechi nyingine leo hii, Kagera Sugar wameshindwa
kutamba katika dimba lake la nyumbani, Kaitaba, baada ya kulazimisha suluhu ya
bila kufungana na Ruvu Shooting ya Pwani.
Pale Manungu Complex, Mtibwa Sugar wamewafumua
wababe wengine wa Simba sc, Coastal Union mabao 3-1.
Nao maafande wa JKT Ruvu wameimaliza kabisa Rhino
Rangers baada ya kuifunga mabao 3-1 katika dimba la Azam Complex, hivyo
kuwafanya maafande hao wa Tabora kuendelea na safari yao ya kuiaga ligi kuu.
0 comments:
Post a Comment