Na Baraka Mpenja,
Dar es salaam
0712461976/0764302956
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara na
wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa, Dar Young Africans
tayari wamewasili jijini Cairo kujiandaa na mchezo wa marudiano wa ligi ya
mabingwa barani Africa utakaopigwa jumapili machi 9 mwaka huu dhidi ya mabingwa
watetezi wa kombe hilo, klabu ya
National Al Ahly.
Taarifa kutoka Misri zinaeleza kuwa baada ya
wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa klabu ya Yanga SC kufika uwanja wa
ndege mjini humo, waandishi wa habari walitaka kuzungumza na wachezaji, lakini
hakuna mchezaji yeyote aliyezungumza nao kwa sababu maalumu.
Waandishi hao baada ya kuchuniwa na wanajangwani,
waliishia kuwapiga picha wachezaji, viongozi pamoja na basi walilopanda kuelekea
Katika Hotel waliyokusudia kuweka kambi.
Waarabu wamekuwa na utamaduni wa kufanya fitina kwa
timu za kigeni kila zinapokwenda kucheza kwao, lengo likiwa ni kuwaondoa
mchezoni wapinzani ili wawafunge kirahisi.
Mwaka 2003, Mnyama Simba aliwatoa Zamalek na kuwavua
ubingwa wakiwa kwao Cairo kwa njia ya mikwaju ya penati, lakini kabla ya mchezo
huo, zilifanywa fitina nyingi sana ili kuwafunga Simba.
Simba wakiwa katika ubora wa hali ya juu ndani ya
uwanja na nje ya uwanja, walikabiliana na changamoto zote, huku viongozi
wakiongozwa na `Friends of Simba` walikuwa makini kusimamia kila kitu ili fitina
za Zamalek zisiathiri mchezo.
Hatimaye walishinda na kuwatoa wenyeji wao, hivyo
kuleta heshima kubwa kwa Tanzania.
Leo baada ya Yanga kuwasili, nao Al Ahly wanaonekana
wamekusudia kufanya fitina kwani wamekuwa wakichelewesha baadhi ya mambo ya msingi
kisheria ikiwemo kutowafahamisha Yanga uwanja utakao tumika jumapili.
Yanga wamejiandaa kwa lolote lile, ndio maana
inawezekana wamewakataza wachezaji wao kuongea na waandishi wa habari wa Misri
wanaoiunga mkono timu yao.
Wanajangwani wataingia katika mchezo huo wakiwa na
faida ya ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam Machi mosi mwaka huu.
Bao hilo pekee lilifungwa na beki wakati na nahodha
wa klabu hiyo, Nadir Haroub `Canavaro` katika dakika ya 82 ya mchezo.
Yanga wanahitaji sare yoyote ile au suluhu, au
matokeo ya kufungwa kwa tofauti ya bao moja, mfano 2-1 ili wafaidike na bao la
ugenini.
Kikosi cha Mholanza Hans Van Der Pluiljm kimekuwa
kikijaanda kwa takribani wiki nzima katika hoteli ya Bahari Beach kunduchi
jijini Dar es salaam, hivyo kina nafasi ya kushinda endapo wachezaji watakuwa
makini.
Wachezaji wa Yanga wanahitaji kuwa watulivu na
kutambua kuwa kuna mashabiki wengi wapo nyuma yao, hivyo fadhila kwao ni
kuucheza mpira kwa nguvu zote.
Taarifa kutoka Misri zinaeleza kuwa hali ya wachezaji
ni nzuri, kiafya, fikra na morali ya kuelekea mchezo wenyewe bado ni kubwa
kwani bench la ufundi na wachezaji wanaamini maandalizi wanayoyafanya
yatasaidia kupelekea kupata ushindi katika mchezo huo na kuweza kusonga mbele
katika hatua ya 16 bora.
Mchezo wa jumapili
unatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Arab Contractors uliopo jijini Cairo
huku mechi hiyo ikichezwa bila ya mashabiki kufuatia Serikali ya Misri kuzuia
mashabiki wa soka kutokana na mashabiki hao kufanya vurugu katika mchezo wa
Fainal ya Super Cup dhidi ya CS Sfaxien na kupelekea askari kadhaa kujeruhiwa.
0 comments:
Post a Comment