Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WALIOKUWA wawakilishib pekee wa Tanzani michuano ya Kimataifa, Young Africans SC wametolewa
kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika na mabingwa watetezi Al Ahly
kwa mikwaju ya penati 4-3 usiku wa jana katika Uwanja wa El Max jijini Alexandria
Mshindi wa mchezo huo alilazimika
kupatikana kwa mikwaju ya penati kufuatia kumalizika kwa dakika 90 za mchezo
huo huku Al Ahly wakiwa mbele kwa bao 1-0 sawa na matokeo ya
Dar es salaam , hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1.
Licha ya kupoteza mchezo huo, Yanga
walipigana kiume kutoka mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Yanga walionekana kucheza kwa kujituma
zaidi kwani walitambua wazi kuwa Watanzania wengi hasa mashabiki wao wapo nyuma
yao.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata ushindi
katika mchezo wa jana kutokana na ukweli kuwa waarabu wanacheza mpira mkubwa sana wakiwa nyumbani kwao.
Al Ahly katika mechi ya kwanza Uwanja wa
Taifa , jijini Dar es salaam walicheza mpira wa taratibu zaidi, huku nusu yao
wakiwa nyuma kulinda lango lao.
Yanga walishambulia sana lango wa Al
Ahly, lakini waarabu walikuwa makini.
Kwa upande mwingine washambuliaji wa
Yanga walishindwa kutumia nafasi walizopata.
Katika mchezo wa jana, Al Ahly si wale
waliocheza Dar es salaam. Kwa haraka mtu anaweza kugoma kabisa. Walikuwa na
kasi kubwa na mashambulizi mengi zaidi.
Walifahamu kabisa kuwa wanahitaji
ushindi katika mchezo huo, hivyo waliingia kwa kazi ya kutafuta mabao.
Wakati waarabu wakihaha kutafuta mabao
katika mchezo huo uliochezwa bila mashabiki kuwepo uwanjani, Yanga walionesha
utulivu mkubwa katika safu ya ulinzi ikiongozwa na nahodha, Nadir Haroub
`Canavaro`.
Kipindi kizima cha kwanza, Al Ahly
walishindwa kufurukuta na kutikisa nyavu za Yanga.
Kwa upande wa Yanga wao waliingia
uwanjani wakiwa makini na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa lango la Al
Ahly.
Kikwazo kilikuwa kwa wachezaji wa Yanga,
Didier Kavumbagu , Simon Msuva na Frank Domayo ambao walikosa umakini katika
nafasi za wazi walizopata.
Bao la dakika ya 70 walilopata Al Ahly kupitia
kwa beki wao wa kushoto Al Ahly Saed Mowaeb liliwaamsha zaidi na kuwashambulia
Yanga kwa nguvu.
Mchezo ukawa mgumu zaidi kwa
wanajangwani, lakini walinzi wake Kelvin Yondani, Nadir Haroub walikua makini
kuokoa michomo hiyo huku mlinda mlango Deogratius Munishi `Dida` akifanya kazi
ya ziada kuokoa hatari langongi mwake.
Kipindi hicho cha pili hakikuwa kizuri
sana kwa Yanga, japokuwa walifanya
mashambulizi kadhaa langoni mwa wapinzani wao, lakini mwamuzi wa mchezo huo
kutoka nchini Senegal aliwaonesha kadi za njano wachezaji wa Yanga na kupuliza
filimbi kila wachezaji wa Al Ahly walipoguswa kawaida tu.
Sitaki kuamini kuwa alikuwa
akiwapendelea wenyeji, lakini kuna wakati alikuwa akizidisha mno. Wachezaji wa
Al Ahly walikuwa wakiguswa kawaida .
Hizo ni mbinu katika mpira wa miguu, cha
msingi unapogundua wapinzani wako wanasaidiwa na mwamuzi kila wanapoguswa na
kujiangusha, unatakiwa kuongeza umakini.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa Yanga.
Walionesha ukomavu na uvumilivu mkubwa hapo jana.
Mikwaju ya penati kuna wakati inafungwa
kwa ufundi, lakini kuna muda unaweza kuamini katika bahati.
Tumeshuhudia wanasoka maarufu kama
Ronaldo na Messi na wengine wengi wakikosa penati katika michezo mbalimbali.
Kukosa penati sio kesi. Kuna wakati
inakuwa ni bahati tu.
Yanga walipata penati 3 huku wenyeji wao
wakipata 4.
Waliofunga penati za Yanga ni Nadir
Haroub , Didier Kavumbagu, na Emmanuel Okwi
Wakati huo penati ya Oscar Joshua
iligonga mwamba , Said Bahanuzi ilitoka nje, na ya Mbuyu Twite iliokolewa na golikipa Ekramy.
Al Ahly penati zao zilifungwa na Abdalllah
Said, Gedo, Trezeguet na Mohamed Nagieb, huku mlinda mlango Deo Munshi akipangua penati
mbili za Saed Mowaeb na Hossan Ashour
Nawapongeza Yanga kwa kucheza kwa kujituma
ingawa malengo yao hayakutimia.
Kinachotakiwa si kukata tamaa, wajiandae
kwa wakati mwingine kwani wanacho kikosi bora cha kushindana.
Najua watabezwa sana na mashabiki wa
upande wa pili pamoja na viongozi, lakini wanatakiwa kutambua kuwa utani katika
mpira una nafasi yake.
Warudi nyumbani na kuelekeza nguvu zao
ligi kuu soka Tanzania bara ili kutetea ubingwa wao.
Wapo nafasi ya tatu katika msimamo,
lakini wanayo michezo mkononi, cha msingi ni kusahau matokeo ya jana na kuanza
upya kazi ya kuutafuta ubingwa wa ligi kuu.
Kama watatwaa ubingwa msimu huu watapata
nafasi nyingine ya kushiriki katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa
ngazi ya klabu.
Kwa kiwango cha Yanga katika mchezo wa jana
ambao ulikuwa mgumu namna kwao, unaweza
kugundua kirahisi kuwa Yanga wamejiamini na wana kikosi bora msimu huu.
Bila shaka waarabu wamelala na viatu
huku mashabiki wao wakishangilia usiku kucha mitaani jijini Cairo, kwani
ushindi wao ulipatikana kwa nguvu sana.
Yanga walikuwa wanawashinda Al Ahly katika
maarifa ya kufumania nyavu, na endapo vijana wa Hans Van Der Pluijm wangekuwa
makini wangefunga mabao.
Poleni wana Yanga wote, huo ndio mpira.
Njooni nyumbani mcheze ligi kuu.
0 comments:
Post a Comment