Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976/0764302956
ZIMEBAKI saa chache kuwashuhudia wawakilishi pekee wa
Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, Young Africans Sports Club wakioneshana
shughuli pevu dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, National Al Ahly katika
dimba la El Max Haras El Hodod jijini Alexandria.
Mchezo wa leo unatarajiwa kuanza majira ya saa 1:00
usiku kwa saa za Misri ambapo kwa sasa za Afrika mashariki itakuwa saa 2:00
usiku.
Yanga wana matumaini makubwa ya kuwafunga Al Ahly
kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza iliyopigwa uwanja wa Taifa machi mosi mwaka
huu ambapo Wanajangwani walishinda bao 1-0.
Bao hilo pekee lilifungwa na nahodha wa Yanga na beki
wa kati, Nadir Haroub `Canavaro` katika dakika ya 82.
Taarifa kutoka Misri kwa viongozi wa Yanga zinaeleza
kuwa mpaka sasa hali ni shwari kabisa, wachezaji wapo salama na wana morali
kubwa ya kupambana na Al Ahly usiku wa leo.
Kikosi cha Young Africans kiliwasili jana jijini
Alexandria kikitokea jijini Cairo na usiku kilifanya mazoezi katika uwanja utakaotumika
kwenye kipute cha leo.
Wachezaji 20 waliopo Alexandria walifanya mazoezi
chini ya makocha Hans Van der Pluijm, Charles Mkwasa pamoja na kocha wa makipa
Juma Pondamali anayewanoa magolikipa.
Maandalizi ya mchezo huo ambao utaoneshwa na
televison zaidi ya 8 za nchini Misri, yamekamilika na katika kikao cha
maandalizi ya mechi kamisaa ameendelea kusisitiza kuwa mchezo hautakua na
mashabiki wa aina yoyote.
Wakati hayo yakiriji huko Misri, waliokuwa
wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika na
washindani wa Yanga kuwania ubingwa msimu huu, klabu ya Azam fc imeitakia kila
la heri Yanga katika mchezo wa leo.
Taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa wa Azam fc katika mtandao
wa kijamii wa facebook imesema kuwa;
“Klabu ya Azam FC inawatakia kila la
kheri wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Klabu Bingwa, Dar Young Africans ipate ushindi au sare na
kuweza kuwatoa Al Ahly.”
“Ushindi wa Yanga
leo ni ushindi wa watanzania wote. Mungu Ibariki Yanga, Mungu Ibariki Tanzania”.
Wachezaji waliopo nchini Misri na kufanya mazoezi ya
mwisho leo jioni ni"
Magolikipa: All Mustafa "Barthez",
Juma Kaseja, Deogratias Munish "Dida"
Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar
Joshua, David Luhende, Kelvin Yondani "Cotton", Nadir Haroub
"Cannavaro"
Viungo: Haruna Niyonzima, Saimon Msuva,
Athuman Idd "Chuji", Frank Domayo "Chumvi", Nizar Khalfani
Washambuliaji: Mrisho Ngasa, Said Bahanuzi,
Emmanuel Okwi, Hamis Kizza, Jerson Tegete na Didier Kavumbagu
Timu nzima ya mtandao
huu inawatakia kila la kheri wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika
mashindano ya kimataifa.
Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na watanzania
wachache waliopo Misri, waunganishe nguvu yao pamoja ili kuwavua ubingwa Al
Ahly wakiwa kwao.
Okwi, Ngassa, Kiiza, Kavumbagu, Bahanuzi, Tegete, hakikisheni
mnatumia vizuri nafasi mtakazobahatika kuzipata. Kumbukeni watanzania wapo
nyuma yenu.
`Canavaro` unganisha nguvu katika beki yako. Wewe ni
nahodha, hakikisha unawatia moyo vijana muda wote mtakapokuwa uwanjani.
Niyonzima, Domayo pale katikati chezeni kwa umoja na
wachezaji wenzenu. Pigeni pasi kwa kwenda mbele, hakika mnategemewa sana.
Msilaumiane hata kidogo, peaneni maelekezo kwa busara,
pambaneni mwanzo hadi mwisho. Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu sana, lakini kila
kitu kinawezekana.
Mungu Ibariki Young Africans,
Mungu Ibariki Tanzania .
0 comments:
Post a Comment