Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
YANGA sc wanachuana vikali na Azam fc katika mbio za
kuwania mwari wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Mpaka sasa mbio za ubingwa ni wazi na hakuna anayeweza
kutabiri nani anaweza kubeba taji.
Mbeya City nao wanafuata nyuma yao wakiwa na dhamira ya kutwaa ubingwa au kushika
nafasi tatu za juu katika msimamo.
Simba sc wameachwa mbali na hawazungumzwi kabisa katika
kinyang`anyiro cha ubingwa.
Baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi
ya Tanzania Prisons, `Wajelajela` uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam na Azam fc kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT
uwanja wa Mkwakwani Tanga, nafasi mbili za juu zimeonekana kuwa na ushindani
mkubwa.
Kinachosubiriwa kwasasa ni timu moja kupoteza mchezo
ili kuiruhusu nyingine kusogea juu zaidi.
Mpaka sasa Yanga wameshuka dimbani mara 21 na
kujikusanyia pointi 46, huku Vinara Azam fc wakiwa wamecheza mechi 22 na
kujikusanyia pointi 50.
Yanga wana mechi moja ya kiporo dhidi ya Kagera Sugar
aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Wakati timu hizi zikipigana kufa na kupona kuwania
ubingwa, mechi zifuatazo zimebakia kwa kila klabu.
Ukiangalia uzito wa mechi zenyewe, pengine wale wataalamu
wa kubashiri matokeo ndio wakati wao.
Kuna wakati soka linatabiriwa. Huwa ni bahati tu kwa wale wanaopatia utabiri,
lakini mara nyingi matokeo ya mpira wa miguu hupatikana ndani ya dakika 90.
Sababu inayotumiwa na watabiri wengi ni ubora wa
vikosi vya timu zitakazocheza, kuanzia mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla.
Ila mpira wa miguu huwa unaleta matokeo tafauti.
Unaweza kuwa na timu bora na ukapoteza.
Azam fc wamebakiza mechi 4, huku mabingwa watetezi, Yanga wakibakiza mechi
5.
Machi 30 mwaka huu, Azam fc watakuwa wenyeji wa
Simba katika dimba la Taifa.
Mechi hii inatazamiwa kuwa ngumu kwa timu zote kutokana
na mazingira ya timu zote.
Simba sc hawana matumaini ya kutwaa ubingwa, lakini
yawezekana wakaingia uwanjani kushindaa ili kulinda heshima.
Ukiwasikia mashabiki wa Simba sc, wanakiri kabisa
kuwa hawana ujanja msimu huu, lakini bora kutoa pointi tatu kwa Azam fc jumamosi, ila si kwa Yanga
aprili 19.
Sidhani kama benchi la ufundi nalo lina mawazo kama
hayo. Bila shaka kocha Dravko Logarusic ataingia kwa nia ya kupata matokeo ya
ushindi.
Joseph Marius Omog , kocha wa Azam fc ataingia kwa
wembe ule ule anaotumia kuzinyoa klabu za ligi kuu.
Kwanza ataingia kulinda rekodi yao ya kutofungwa
msimu huu katika mechi 22 walizocheza, lakini ataweka mkazo zaidi katika
ushindi kwa kuvuna pointi tatu muhimu.
Kupoteza mechi au kutoa sare hayatakuwa matokeo
salama kwa Azam fc , kwasababu Yanga atakuwa Tanga kukabiliana na Mgambo JKT.
Mechi nyingine iliyobakia kwa Azam fc ni aprili 6
mwaka huu uwanja wa Mabatini mkoani Pwani ambapo watakabiliana na Ruvu Shooting
ya mkoani humo.
Hii mechi itakuwa muhimu zaidi kwa Azam fc, kwasababu
wapinzani wao hawana cha kupoteza.
Hawawazi kushuka daraja wala kutwaa ubingwa. Hivyo `presha`
itakuwa kwa Azam fc kutegemeana na matokeo ya Yanga.
Aprili 13, Azam fc watasafiri mpaka jijini Mbeya
kuwafuata Mbeya city FC katika uwanja wa Sokoine jijini humo.
Hii dhahiri shahiri itakuwa mechi ngumu zaidi kwa Azam
fc kwani Mbeya City ni washindani wao.
Haitakuwa kazi nyepesi kupata matokeo ya ushindi
mbele ya wagonga nyundo hao wa Mbeya, kwasababu hawana rekodi ya kupoteza mchezo
nyumbani kwao.
Baada ya kutoka Mbeya, Azam fc watarudi Chamazi
kupambana na JKT Ruvu ya Fredy Felix Minziro.
Ugumu wa mechi hii utatokana na matokeo ambayo JKT
Ruvu watakuwa nayo mkononi katika mechi nyingine watakazocheza kabla ya kipute
hicho.
JKT Ruvu Wapo katika hatari ya kushuka daraja. Kama kufikia siku ya mechi dhidi ya Azam
watakuwa wanahitaji pointi ili kujisalimisha, basi mchezo utakuwa mgumu kwa
timu zote mbili.
Kama Azam fc watakuwa wamefanya vizuri katika mechi
nyingine zote, bila shaka watakuwa wapo hatua ya mwisho kutangaza ubingwa wao
wa kwanza tangu wapande ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kwa upande wa Yanga, machi 30 watakuwa ugenini
kuwakabili Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
Hii itakuwa mechi ngumu zaidi kwa Mgambo kwasababu
kupoteza tena baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Azam fc, itakuwa ni kujichimbia
kaburi wenyewe.
Hakuna ufanano wa majina na ukongwe katika ligi kati
ya Yanga na Mgambo.Pia timu hizi zina wachezaji wa aina tofauti.
Yanga wanaweza kupewa kura ya ushindi siku hiyo,
lakini soka linachezwa uwanjani kwa dakika 90.
Baada ya kutoka Tanga, aprili 6 mwaka huu,
wanajangwani watakutana na wapigania kukwepa kushuka daraja wengine msimu huu,
JKT Ruvu.
Ugumu wa mechi hiyo utatokana na mazingira ya JKT
Ruvu.
Yanga msimu huu wameshusha vipondo vikubwa kwa timu
nyingi za majeshi.
Bila shaka kipigo cha mabao 7-0 walichokula Ruvu
Shooting na cha mabao 5-0 walichoambulia Prisons vinatosha kukubaliana na hilo.
JKT Ruvu watahitaji kujipanga kwani kwa wakati huo
Yanga watakuwa hawana cha kutafuta zaidi ya ushindi ili kutetea ubingwa wao.
Aprili 9, Yanga wataikaribisha Kagera Sugar katika
dimba la Taifa jijini Dar es saalam.
Kagera
wamekuwa washindani katika ligi kwa misimu kadhaa, lakini msimu huu mambo
hayajawa barabara.
Si Kagera Sugar ya mwaka jana chini ya Abdallah
Kibadeni `King Mputa`. Imekuwa ya kawaida sana. Ila huwezi kuwanyima kura ya kuwaharibia Yanga.
Aprili 13 katika dimba la Sh. Amri Kaluta Abeid
jijini Arusha, Yanga watakuwa na vibonde, JKT Oljoro.
Mpaka kufikia siku hiyo hatima ya Oljoro kubaki au
kushuka itakuwa imefahamika.
Kama watakuwa wameshakata tiketi ya kushuka daraja,
basi kuna uwezekano wa kuwa mechi nyepesi kwa Yaga kwasababu Oljoro watakuwa
hawana cha kufanya zaidi ya kuendelea na safari yao ya kuporomoka.
Mzinga wa mwisho kwa Yanga utakuwa aprili 19 mwaka
huu ambapo watakabiliana na mahasimu wao, Simba Sc.
Hii ni mechi ambayo huwezi kuitabiri kwa kuangali
ubora wa vikosi kuanzia mchezaji mmoja mmoja.
Utayakubali haya ukikumbuka mechi ya mzunguko wa
kwanza ya mabao 3-3, halafu ile ya `Nani Mtani Jembe` ya 3-1.
Katika mechi hizi mbili, nje ya uwanja, Yanga
walikuwa wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuwafunga Simba sc. Lakini haikuwa
hivyo.
Kwa maana hiyo, usemi wa mechi ya Simba na Yanga
haitabiriki, bado una nafasi katika mchezo huu.
Pia inawezekana mchezo huu ukaamua bingwa wa msimu huu, endapo Azam fc watakuwa
na matokeo mazuri au Mbeya City.
0 comments:
Post a Comment