Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt Rajabu Rutengwe amewataka wakazi wa mkoa huo kuwasomesha watoto wa kike bila ubaguzi kwa kuwa ukimuelimisha mototo wa kike umeielimisha jamii kubwa.
Dkt Rutengwe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke yaliyofanyika kimkoa katika Tarafa ya Karema Wilaya ya Mpanda na kuhudhuliwa na mamia kwa maelfu ya wanawake na kupambwa na burudani za ngoma na michezo mbalimbali.
Katika hotuba yake hiyo Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kuhakikisha wanawasomesha watoto wa kike hadi mwisho wa upeo wa kielimu sawa na wanavyowasomesha watoto wa kiume.
Pia amewataka wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ili ziweze kuwasaidia katika maisha na kuepukana na hali ya utegemezi.
Akatolea mfano kuwa eneo la mwambao wa ziwa Tanganyika hasa Tarafa ya Karema wamepewa mradi wa Mwalo unaojengwa na serikali ambapo utakapokamilika utatumike vizuri kwa manufaa ya kuwaletea maendeleo.
Amehimiza wananwake wachangamkie mradi huo. Pia akawasisitiza kujitokeza katika kugombea na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii kwa kuwa akina mama wanaweza hata bila kuwezeshwa maadamu tu kujiamini na kujitokeza .
Katika hatua nyingine amewasisitiza kujitokeza kutumia madawati ya jinsia yaliyoanzishwa kwa ajili ya kutoa malalamiko na unyanyaswaji wanao fanyiwa wanawake na watoto majumbani.
Awali katika risala yao wanawake walieleza changamoto wanazokabiliwa nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji kwa ajili kuendeleza miradi yao katika vikundi vya uzalishaji mali.
Waliiomba serikali kuendelea kuwasaidia kwa kuwapa mikopo ya riba nafuu,.
Pia walishauri vyombo vya mikopo kupunguza riba katika mikopo yao ili waweza kukopo.
Naye Mratibu wa Dawati la jinsia kutoka jeshi la polisi Inspekta Vijinia Sodoka amewahamasisha akina mama kujitokeza kutumia dawati hilo kutoa matatizo na unyanyasaji wanaofanyiwa na waume zao majumbani kwani kwa kutoa taarifa wataweza kusaidia kupunguza nap engine kukomesha kabisa hali hiyo.
Hata hivyo alisema pamoja na unyanyasaji kwa akina mama na watoto, nao wanaume wameshauriwa wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao wajitokeze kutoa taarifa polisi ambapo kupitia kitengo cha dawati la jinsia watasaidiwa kuliko kukaa kimya majumbani bila kutolea taarifa vitendo hivyo.
Alieleza kuwa wapo akina baba wananyanyaswa na wake zao kutokana na mfumo uliopo wanaogopa kutoa taarifa, lakini ukweli ni kuwa wanaume nao wananyanyasika kwenye ndoa zao ila wanaogopa kusema na kutolea taarifa vitendo hivyo.
0 comments:
Post a Comment